Na Mwandishi Wetu
Bukoba
VIONGOZI ngazi ya juu na wakisiasa wametakiwa kutoa ushirikiano kwa
watendaji wa vijiji na kata ili kufanikisha shughuli nyingi za maendeleo
ya jamii kukamilika kwa wakati.
Ushauri huo,umetolewa na
watendaji wa vijiji na kata ndani ya halmashauri ya wilaya ya
Bukoba,waliokuwa wakihudhuria semina ya kikazi ili kuwawezesha kutambua
na kufuata wajibu wao katika shughuli zao za
kila siku iliyofanyika katika vituo viwili vya Maruku na Lyamahoro.
Watendaji
hao walibainisha kuwa shughuli zao hasa za kuhimiza na kukusanya
michango zinakuwa ngumu na kuonekana kuleta kero kwa jamii kutokana na
baadhi ya viongozi wa kisiasa kuitisha mikutano yao na kuanza kupokea
kero za wananchi kwa madai wao ni watetezi,hivyo na kusababisha zoezi la
kuimiza maendeleo kwenda kwa kusuasua.
"Tatizo kuu la jamii yetu
kutohudhuria mikutano ya hadhara ni kutokana na wanasiasa wetu,kufika
katrika mikutano yao na kuomba kusikiliza kero za wananchi,na mwisho
kuwataka wananchi kutokubali lolote linalohusu masuala ya maendeleo hasa
kuchangia"alisema Abdallah Rwabigimbo,afisa mtendaji kata Katoma.
Alisema
kuwa mara nyingi jamii inawaona watumishi hawa kama ni sehemu ya
kuwanyanyasa,jambo ambalo si kweli na linawafanya kuishi kwa mashaka juu
ya maisha yao ya kila siku,na kusababisha jamii kuacha kuhudhuria
mikutano pale wanapoitisha juu ya kupewa taarifa juu ya mapato na
matumizi.
Hata hivyo,wameomba serikali kuangalia ni jinsi gani
itaweza kuwapatia motisha viongozi wao wa kuchaguliwa yaani wenyeviti wa
vitongoji ili kuwezesha kazi zao kufanyanyika vizuri na kwa ushirikiano
mwema.
"Serikali iangalie jinsi gani inaweza kuwapatia motisha
wenyeviti wa vitongoji ili kuharakisha shughuli za maendeleo,kwani
wakati mwingine shughuli zetu zinakwama kutokana na
viongozi hawa kutokuwa na mwamko kutokana na majukumu yao"alisema
William Buberwa,afisa mtendaji kata Buhendangabo.
Kwa upande wake
mratibu wa semina hiyo Philimon Magesa,ambaye pia ni afisa utumishi wa
halmashauri ya wilaya Bukoba,aliwaasa watendaji hao kufuata sheria
zilizopo hasa wakati wa kufanya shughuli zao za ulinzi na amani katika
maeneo yao huku wakifatilia sana kanuni za maadili ya kazi.
Magesa
alisema kuwa lengo kuu la semina hiyo,kuwapatia mafunzo watendaji hawa
kufuata taratibu mbalimbali zilizo ndani ya kazi zao za kila siku na
mada kuu ikiwa ni kufuata misingi ya utawala bora.
Semina hiyo
iliyoendeshwa na mwezeshaji Venance Shilingi,kutoka chuo kikuu cha
Mzumbe iliwashirikisha jumla ya washiriki 120 wakiwa watendaji wa vijiji
na kata ikiwa kata 29 na vijiji 94 vilivyo ndani ya halmashauri ya
wilaya ya Bukoba.
MWISHO
No comments:
Post a Comment