Sunday, September 30, 2012

Taswira Kutoka Makuyuni-Monduli

Makuyuni hapa,picha na Monica Maganga akiwa Monduli

Kashfa Nyingine Yaibuka Tanesco


 Na:Fidelis Butahe,Mwananchi

KASHFA mpya imeibuka ndani ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), baada ya kubainika kuwa vikombe vya kufungia nyaya za umeme vyenye thamani ya mamilioni ya fedha vimetelekezwa kutokana na baadhi ya vigogo wa shirika hilo kushindwa kunufaika na mradi huo.

 Habari kutoka ndani ya shirika hilo zinaeleza kuwa vigogo hao wanadaiwa kuvikataa vikombe hivyo kwa maelezo kuwa ni vibovu, baada ya mzabuni kushindwa kuwaona vigogo hao. Wakati vigogo hao wakivikataa vikombe hivyo kwa madai kuwa ni vibovu, taarifa zinaeleza kuwa wataalamu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wamethibitisha kuwa vikombe hivyo ni vizuri na havina matatizo yoyote. Hatua ya Tanesco kupeleka vikombe hivyo kuthibitishwa na wataalamu wa Chuo Kikuu, Kitengo cha Uhandisi ilitokana na mvutano uliokuwapo baada ya vigogo walioshindwa kunufaika na mradi huo kutoa maelezo kuwa vikombe hivyo havina viwango bora. 

Hata hivyo, uchunguzi unaonyesha kuwa licha ya vigogo hao kuvikataa vikombe hivyo zaidi ya 40,000 vyenye thamani ya Sh900 milioni kwa madai kuwa vibovu, tayari shirika hilo limekuwa likivitumia katika nguzo zake zenye umeme mkubwa kwa miaka mingi. Mvutano wa viongozi hao ndani ya shirika hilo, umesababisha mradi wa kukarabati njia za umeme mkubwa bila ya kuzima umeme kwa kuondoa vikombe vilivyochakaa uliokuwa ukifanyika katika mikoa ya Arusha na Kilimanjaro kusimamishwa mapema mwaka huu. 

Baadhi ya wataalamu wa Tanesco wanaeleza kuwa vikombe hivyo kama vitatumika vina uwezo wa kutosheleza mahitaji ya kufunga vikombe vipya katika njia ya umeme mkubwa wa kutoka kwenye mtambo wa kuzalishia umeme wa Kidatu mkoani Morogoro hadi Ubungo jijini Dar es Salaam. Pia, kumalizia ukarabati wa njia ya umeme ya Arusha hadi Moshi mkoani Kilimanjaro iliyositishwa. 

Chanzo chetu kutoka ndani ya Tanesco kinaeleza kuwa vikombe vilivyopo katika njia ya umeme ya Kidatu hadi Ubungo havijabadilishwa kwa miaka mingi hali ambayo inafanya umeme kupotea njiani kwa asilimia nyingi. Kaimu Mkurugenzi Mkuu Mtendaji wa Tanesco, Felschami Mramba alisema kuwa mikataba ndani ya shirika hilo ni mingi na kusisitiza kuwa hawezi kulijibu suala hilo mpaka atakapowasiliana na kitengo cha ununuzi cha shirika hilo. 

“Kwa sasa sina maelezo ya kina ya mikataba, hasa kuhusu suala hilo unaloniuliza, lakini mpaka wiki ijayo nitakuwa nimefuatilia na kupata jibu sahihi,” alisema Mramba. Kwa upande wake Naibu Waziri wa Nishati na Madini anayeshughulika Nishati, George Simbachawene alisema suala hilo halijafika kwake.

 Simbachawene alisisitiza: “Mambo yanayofika katika ofisi yangu huwa kama malalamiko yanayoletwa na watu kutoka Tanesco na sehemu nyingine. Nikiyapata naanza kufuatilia ili kujua nini kinaendelea.” Alisema kuwa Tanesco ni shirika linalojitegemea katika utendaji wake wa kazi na ndiyo maana lina bodi yake, ambayo hukaa na kupanga mambo mbalimbali ya kufanya.

 “Wakati mwingine wizara inaingilia utendaji wa Tanesco kama tunaona kuna mambo hayaendi sawa, ila hili la ununuzi kwa kweli sijui kwa sababu halijafika ofisini kwangu kama lalamiko,” alisema Simbachawene na kushauri kuwa atafutwe Mramba. Hoja ya kuvikataa vikombe hivyo ambayo imekuwa ikitolewa na baadhi ya vigogo hao wa Tanesco ni kwamba vikombe hivyo ni vizito na nguzo haziwezi kuvibeba, vibovu na kwamba havifai katika ule utaratibu wa kufanya matengenezo bila kuzima umeme. Tanesco imekuwa ikikumbwa na kashfa mbalimbali zikiwamo matumizi mabaya ya fedha za shirika kwa baadhi ya maofisa kutumia zabuni kujinufaisha. Hivi karibuni Mkurugenzi Mkuu Mtendaji wa Shirika hilo, Mhandisi William Mhando alisimamishwa kazi na Bodi ya Wakurugenzi ya shirika hilo.

 Taarifa iliyotolewa na Bodi ya Wakurugenzi ilieleza kuwa Mhando alisimamishwa kazi pamoja na watendaji wakuu wengine wa Tanesco ili kupisha uchunguzi wa tuhuma za ubadhirifu na matumizi mabaya ya madaraka. 

 Viongozi wengine wa Tanesco waliosimamishwa kazi ni Naibu Mkurugenzi Mtendaji Huduma za Shirika, Robert Shemhilu, Ofisa Mkuu wa Fedha, Lusekelo Kassanga na Meneja Mwandamizi wa Ununuzi, Haruni Mattambo. 
Matatizo mengine ambayo yanadaiwa kuikumba Tanesco ni pamoja na uchakavu wa mitambo ya Tanesco, hujuma za miundombinu na kuingiwa kwa mikataba mibovu 
 Chanzo: http://www.mwananchi.co.tz/habari

MagazetiReactions::

Friday, September 28, 2012


HakiElimu Wazindua Matangazo Kuhamasisha Elimu Ya AwaliNa Joachim Mushi, Thehabari.com

 TAASISI ya HakiElimu imezindua matangazo mapya ya redio na televisheni ikiwa ni kampeni ya kuhamasisha jamii na Serikali juu ya umuhimu wa elimu ya awali kwa watoto kabla ya kujiunga na darasa la kwanza.

 Uzinduzi huo umefanyika leo jijini Dar es Salaam katika Ofisi za HakiElimu na kuhudhuriwa na baadhi ya walimu na wanafunzi wa awali, waandishi wa habari, wadau mbalimbali wa sekta ya elimu, pamoja na malezi na makuzi ya watoto. Akizungumza katika uzinduzi huo Mkurugenzi Mtendaji wa HakiElimu, Bi. Elizabeth Missokia alisema shirika hilo lemeamua kuzindua kampeni hiyo iliyopewa jina la “Boresha Elimu ya Chekechea” lengo kuu likiwa ni kuitaka Serikali itimize ahadi na wajibu wake wa kutoa elimu bora kwa wanafunzi wote wa elimu ya awali. 

Mkurugenzi huyo alisema elimu ya awali kwa mtoto ni muhimu sana katika kujenga msingi imara kielimu na endapo elimu hiyo itatolewa kikamilifu, inakuwa ni msingi imara kwa mtoto katika elimu yake ya baadae na pia elimu hiyo ni muhimu kwa maendeleo ya mtoto kimwili, kiakili na kimaadili. “Katika Sera ya Elimu na mafunzo ya mwaka 1995 Serikali inaonesha umuhimu wa elimu ya awali, inapotamka; ‘Tafiti kadhaa zilizofanyika nchini katika miaka ya 1980 zilibaini kuwa watoto waliopitia elimu ya awali huwa na mafanikio makubwa zaidi wanapoanza darasa la kwanza. 

Kutokana na kutambua umuhimu huu, Serikali iliamua kuingiza Elimu ya Awali kwa watoto wenye umri wa miaka 5 na 6 kwenye mfumo rasmi wa elimu na kila shule ya msingi inapaswa kuwa na madarasa ya Elimu ya Awali’,” alisema Missokia. Alisema kabla ya uzinduzi wa kampeni hii HakiElimu imefanya tafiti katika sehemu mbalimbali nchini na kubaini hali ya utoaji wa elimu ya awali na mazingira yake inatia huruma kwani elimu hiyo inavyotolewa katika mazingira yasiyofaa jambo ambalo linachangia kushuka kwa kiwango cha elimu nchini. “Kama ilivyo katika elimu ya msingi na ile ya sekondari, elimu ya awali imegubikwa na changamoto nyingi. Baadhi ya changamoto hizi ni upungufu mkubwa wa vyumba vya madarasa, unaosababisha mrundikano mkubwa katika madarasa, ukosefu mkubwa wa walimu wenye taaluma ya elimu ya awali pamoja na vifaa vya kufundishia. 


Aidha, kutokuwepo na tofauti ya kimadarasa katika elimu ya awali (yaani watoto wa umri wa miaka 5 na miaka 6 kusoma katika darasa moja), na wingi wa masomo pia ni changamoto,” alisema. Aidha aliongeza kuwa licha ya Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa, katika makadirio na matumizi ya wizara yake ya mwaka 2012/13, kukiri kuwa Serikali imetoa mwongozo kwa kila shule ya Msingi kuwa na darasa la Elimu ya Awali, lenye madawati yanayolingana na hali ya watoto wa elimu hiyo, kujenga vyoo kwa ajili ya watoto wa Elimu ya Awali wasiingiliane na wale wa shule za msingi, lakini bado kuna mapungufu makubwa katika utekelezaji wake. 

 "Baada ya kuona madhara ya kukosa elimu bora ya awali kwa watoto wetu, HakiElimu inatoa wito kwa watanzania wote nchini wenye mapenzi mema na maendeleo ya taifa letu kuungana nasi katika kampeni hii kwa njia zifuatazo; Kuhimiza wananchi wote wenye watoto wenye umri wa kuandikishwa shule za awali wafanye hivyo kwa wingi. Kuna baadhi ya sehemu inaripotiwa wazazi bado hawajaelewa umuhimu wa kuwapeleka watoto katika madarasa haya ya awali. "Kuwabana viongozi wetu tuliowachagua kuanzia mwenyekiti wa mtaa, diwani na Wabunge wetuwanachukua hatua kukabiliana na changamoto zilizopo ili kufanikisha Elimu bora ya Awali kwa watoto wetu. Wananchi kuandika barua kwenye magazeti mbalimbali hapa nchini zikielezea hali ya elimu ya awali inavyotolewa katika maeneo mliyopo.

" HakiElimu imeshauri barua zinazoandaliwa na wananchi kuzituma moja kwa moja kwa Wahariri wa magazeti wanayoyasoma kupitia anuani zilizopo katika gazeti husika, au wanaweza kuzituma kupitia sanduku la barua 79401 Dar es Salaam zikiwa na kichwa cha habari ‘BORESHA CHEKECHEA’, ambapo HakiElimu itafanya kazi ya kuzipeleka katika magazeti mbalimbali nchini. Aidha, ili kuchagiza mafanikio katika sekta ya elimu, HakiElimu imeandaa vipindi vya radio katika mikoa ya Morogoro, Mbeya, Tabora, Tanga, Kagera, Dodoma na Mara ambavyo vitatoa nafasi ya Marafiki wa Elimu kujadili jinsi gani elimu ya awali inaweza kuboreshwa. 

 Hata hivyo kwa Watanzania wanaotumia mtandao wa 'Internet' wanaweza kushiriki kampeni hii kwa kutembelea; www.facebook.com/hakielimu, www.twitter.com/hakielimu, www.hakielimu.blogspot.com na kuangalia matangazo mapya waweza kutembelea YouTube kupitia www.youtube.com/hakielimutz

  Habari hii imeandaliwa na mtandao wa www.thehabari.com
Reactions::

Taarifa TFF Kwa Vyombo Vya Habari

Release No. 157 TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI Septemba 28, 2012

 TFF YATOA ITC KWA WACHEZAJI WANNE Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limetoa Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC) kwa wachezaji wanne waliokuwa wakichezea timu mbalimbali nchini. Wachezaji hao ni Tony Ndolo aliyejiunga na KCC ya Uganda kutoka Toto Africans, Felix Amech Stanley aliyekwenda Bahla ya Oman kutoka Coastal Union, Ernest Boakye kutoka Yanga aliyejiunga na Tripoli Athletics Club ya Lebanon na Derrick Walulya aliyerejea URA ya Uganda kutoka Simba. 15 WACHUKUA FOMU UCHAGUZI TWFA Wanamichezo 15 wamechukua fomu kuwania nafasi mbalimbali za uongozi kwenye Chama cha Mpira wa Miguu wa Wanawake Tanzania (TWFA) utakaofanyika mwanzoni mwa mwezi ujao. Waliochukua fomu za kuwania uenyekiti ni Lina Kessy, Isabellah Kapera na Joan Minja.

 Nafasi ya Makamu Mwenyekiti imeombwa na Roseleen Kisiwa pekee wakati Katibu Mkuu ni Amina Karuma na Cecilia Makafu. Macky Mhango pia ni mwombaji pekee aliyeomba nafasi ya Katibu Msaidizi. Waombaji watatu wa nafasi ya mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ni Furaha Francis, Juliet Mndeme na Zena Chande. Nafasi ya Mhazini nayo ina mwombaji mmoja tu ambaye ni Rose Msamila. Sophia Charles, Rahim Maguza, Telephonia Temba na Jasmin Badar Soud wao wanaomba nafasi ya ujumbe wa Kamati ya Utendaji ya chama hicho kwenye uchaguzi huo ambao utaendeshwa na Kamati ya Uchaguzi ya TWFA chini ya Ombeni Zavalla. 

MKUTANO VODACOM, KLABU ZA LIGI KUU Klabu za Ligi Kuu na mdhamini wa ligi hiyo kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom zimekutana jana (Septemba 27 mwaka huu) jijini Dar es Salaam.

 Mazungumzo yalilenga kipengele ya upekee (exclusivity) kilichopo kwenye mkataba wa udhamini ambacho kitaendelea kuwepo. Klabu zilikuwa zimeomba kwa mdhamini kuangalia uwezekano wa kukiondoa. Pande hizo zimekubaliana kuunda kamati ya pamoja kwa ajili ya kuitafutia kila klabu mdhamini binafsi kwa lengo la kuhakikisha zinashiriki kikamilifu katika ligi hiyo. Klabu zote zimeshapata vifaa kutoka kwa Vodacom ukiondoa African Lyon ambayo ilitarajia kuchukua vifaa hivyo leo kutoka kwa mdhamini wa ligi hiyo. 

MCHAKATO WA UCHAGUZI WA VIONGOZI TAFCA Mchakato wa uchaguzi wa viongozi wa Chama cha Makocha wa Mpira wa Miguu Tanzania (TAFCA) unaanza rasmi Septemba 30 mwaka huu kwa uchukuaji fomu kwa wagombea. Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TAFCA, Ramadhan Mambosasa, fomu kwa waombaji uongozi zitaanza kutolewa Septemba 30 mwaka huu, na mwisho wa kuchukua na kurudisha fomu hizo ni Oktoba 4 mwaka huu. 

Fomu hizo zinapatikana ofisi za TAFCA zilizopo Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam kuanzia saa 3 asubuhi hadi saa 10 alasiri. Ada ya fomu kwa waombaji wa nafasi za Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti, Katibu Mkuu na Katibu Msaidizi ni sh. 200,000. Nafasi zilizobaki za Mhazini, mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na wajumbe wa Kamati ya Utendaji, ada ya fomu ni sh. 100,000. Uchaguzi wa TAFCA umepangwa kufanyika Novemba 10 mwaka huu. Boniface Wambura Ofisa Habari Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
Reactions::

Apendekeza Sanaa Na Utamaduni Vitambuliwe Kikatiba


NA MAGRETH KINABO – MAELEZO, BAGAMOYO 

 WASANII wamepewa changamoto ya kujitokeza kwa wingi katika kutoa maoni juu ya uundaji wa Katiba mpya ili fani yao iweze kutambulika kisheria. Kauli hiyo imetolewa jana na Mkurugenzi Idara ya Mfuko wa Uwezeshaji wa Baraza la Sanaa la Taifa(BASATA), Charles Malimba wakati akitoa mada kuhusu Sanaa ya Utamaduni na dhana ya Tasnia ya Ubunifu inavyoweza kuleta ajira kwa vijana wa Tanzania katika Tamasha la 31 la Sanaa na Utamaduni linaloendelea kwenye uwanja wa Taasisi ya Sanaa na Utamaduni(Tasuba), Bagamoyo, mkoani Pwani. 

Alisema kuna haja ya wasanii kujitokeza katika kutoa maoni juu ya Katiba mpya ili itambuena kutoa kipaumbele mambo mbalimbali katika sekta ya sanaa na utamaduni. 

Aidha Malimba aliongeza kuwa wakati umefika kuwa Katiba itamke sanaa na utamaduni kazi , pia kuwepo na viwango vya malipo kisheria kwa kuwa sekta hiyo inavyoweza kuchangia mapato kwa serikali. Malimba alitaka vyuo vinavyofundisha sanaa utamaduni nchini kutunza kumbukumbu za fani hizo na kuurithisha ili kuepusha kupotea kwa utamaduni wa Mtanzania , huku akiwataka wanafunzi wa fani hizo kusoma kwa bidii na kuitekeleza ili kuweza kuwasaidia wengine na kuifanya sekta hiyo kuwa ajira. 

Naye mhitimu wa chuo hicho wa mwaka 2010, Nyenyembe Jacoub na Baraka Matitu walisema ili kuweza kukuza sanaa na utamaduni kuna umuhimu wa kuanzisha shule maalum kuanzia chekechea hadi elimu ya juu. Akijibu hoja hiyo, Malimba alisema ni changamoto kwa wadau mbalimbali binafsi kuanzisha shule hizo kama ilivyo kwa zingine kwa kuwa suala hilo halina kipingamizi, huku akisisitiza suala la utunzaji wa sanaa na utamaduni ni wajibu wa kila wanajamii. 

Baadhi ya wasanii waliomba serikali iweke mikakati ya kuweza kuwasaidia wasanii hususan wale wachanga ili kuweza kukuza vipaji vyao, kwa kuwa vingi vinaanzishwa lakini vinashindwa kuendelea kwa kukosa wafadhili.

Taarifa Ya CHADEMA Kwa Vyombo Vya Habari


         TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

KAMATI za Utendaji za Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) katika Wilaya ya Nyamagana na Ilemela katika vikao tofauti kwa kushirikiana na kamati za madiwani katika kila wilaya husika, zimekamilisha mchakato wa kupata wagombea wa nafasi za umeya na naibu meya, Halmashauri ya Jiji la Mwanza na Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela. 

Kamati ya Utendaji ya Wilaya pamoja na madiwani wa CHADEMA Wilaya ya Nyamagana walimteua aliyekuwa Naibu Meya kabla, Diwani wa Kata ya Maina, Charles Chibara kuwa mgombea wa Umeya Halmashauri ya Jiji la Mwanza. Kwa upande wa Ilemela, kikao cha Kamati ya Utendaji pamoja na madiwani wa wilaya hiyo walimteua Diwani wa Kata ya Nyamanoro, Abubakar Kapera kuwa mgombea wa Umeya Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela. Kikao hicho cha Utendaji na madiwani wa CHADEMA Wilaya ya Ilemela, pia kilimteua Diwani wa Kirumba, Danny Kahungu kuwa mgombea wa nafasi ya Unaibu Meya Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela. 

 Vikao hivyo tofauti vya uchaguzi vilivyoketi kwa mujibu wa katiba, kanuni na taratibu za chama chini ya usimamizi wa Ofisi ya Katibu Mkuu wa CHADEMA, vilihusisha wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya Wilaya na madiwani katika eneo husika. Itakumbukwa kuwa katika kutafuta namna bora ya kusimamia vyema utendaji wa chama katika Halmashauri ya Jiji la Mwanza ambayo ilikuwa ni halmashauri pekee nchini iliyokuwa ikihusisha wilaya mbili, yaani Nyamagana na Ilemela, Baraza Kuu la CHADEMA liliamua kuwa masuala yote yanayohusu jiji hilo yasimamiwe na Ofisi ya Katibu Mkuu. Utekelezaji wa maamuzi hayo ya kikatiba, ulianza siku nyingi, ikiwemo kusimamia uchaguzi wa Meya wa Jiji la Mwanza mapema baada ya uchaguzi mkuu mwaka 2010. 

Wakati huo huo Kamati ya Utendaji ya Wilaya Nyamagana imekubali kumwachia kugombea nafasi ya Unaibu Meya wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Diwani wa Mirongo Daudi Mkama, katika uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika Septemba 28, 2012. Aidha, kutokana na vurugu zilizosababishwa na kundi la watu waliovamia na kuvuruga kikao cha uteuzi wa mgombea wa Umeya na Naibu Meya wa Manispaa ya Ilemela hivi karibuni, uongozi wa CHADEMA Wilaya umefungua kesi polisi kwa jalada lenye namba MZN/RB/8226/2012, kwa ajili ya hatua za kisheria.

 Imetolewa leo Septemba 27, 2012, Dar es Salaam; Tumaini Makene Ofisa Habari wa CHADEMA

.


Thursday, September 27, 2012

JK

JK: Afungua Mkutano Wa Kimataifa Wa African Green Revolution Mjini Arusha

Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akizungumza na
Mwenyekiti wa Alliance for a Green Revolution in Africa Dkt.Kofi Annan(kushoto) pamoja na Mkurugenzi wa Bill and Melinda Gates, Bibi Melinda Gates wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Kimataifa wa” Africa  Green Revolution Forum 2012,” uliofanyika katika ukumbi wa Ngurdoto mountain Lodge mjini Arusha.
Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akitoa hotuba yake ya ufunguzi wa mkutano wa Kimataifa wa”African Green Revoultionmjni Arusha.

Zitto: Ubunge sasa basi Na: Frank Sanga na Anthony Kayanda, Kigoma, MWANANCHI.

MBUNGE wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe amesema hana mpango wa kugombea ubunge mwaka 2015 badala yake anajipanga kuwania urais. Zitto alisema hayo jana alipozungumza na wananchi katika mjadala ulioandaliwa na asasi ya kiraia ya Meza ya Duara uliokuwa unafanyika maeneo ya Soko la Mwanga, mjini Kigoma. Zaidi ya watu 200, ambao walihudhuria katika mjadala huo wa wazi walimuuliza maswali mbalimbali mbunge huyo, huku mmoja akigusia kuhusu tetesi za mara kwamba Zitto anataka kugombea urais katika uchaguzi ujao.

 “Nimefanya kazi kubwa katika kazi yangu ya ubunge, nimeleta mabadiliko mengi kuanzia bungeni mpaka jimboni. Nadhani inatosha na hata nikiongezewa miaka mingine sitaweza kufanya yale yaliyonishinda katika kipindi cha miaka kumi. “Kama Mungu ataniweka mpaka mwaka 2015, sitagombea ubunge tena kwa sababu kazi niliyofanya inatosha. Natangaza rasmi kuwa nitagombea urais kupitia chama changu cha Chadema, bila kusababisha msuguano wowote na sitaki kuingia katika historia ya kurudisha nyuma harakati za upinzani kushika dola,” alisema Zitto.

 “Nataka kuleta changamoto mpya, nitawaeleza watu wa chama changu nia hiyo na nitatoa hoja za msingi. Hata kama sitapata ridhaa yao, lakini huo ndio msimamo wangu. “Iwapo chama kikiona sistahili au sifai, nitakubaliana na uamuzi huo. Watu wengi wanadhani urais ni cheo, hawajui kuwa ni nafasi ambayo inakufanya ufanye vitu ambavyo ni vikubwa na vya maendeleo kwa wananchi.” Atangaza kugombea urais Katika hatua nyingine Zitto alisema ana mpango wa kuwania urais kupitia Chadema katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015. “Kwanza nataka niwahakikishia watu wa Kigoma msiwe wanyonge…mna uwezo wa kutoa rais wa nchi hii,” Zitto alianza kujibu swali hilo na kuendelea. 

Hata hivyo Zitto alipoulizwa baadaye na Mwananchi kuwa mwaka 2015 atakuwa na miaka 39, hivyo kukosa sifa ya kugombea urais kwa mujibu wa katiba alijibu; “Nadhani nina uwezo wa kuwa rais, sidhani kama Katiba inaweza kumzuia mtu mwenye uwezo asigombee na ndio maana ninaamini kuwa kipengele cha kuwa na miaka 40 kitabadilishwa katika katiba mpya.”

 “Nchi za Kidemokrasia lazima vyama vibadilishane utawala wa kuongoza nchi kama ilivyo katika nchi za Ghana na Zambia. Tanzania inatakiwa kuiga mfano wa nchi hizo,” alisema Zitto Katika kukazia hilo, Zitto alisema anashangazwa na umaskini uliopo Tanzania wakati mwaka 1976 uchumi wake ulikuwa sawa na nchi ya Malaysia, lakini mpaka kufikia mwaka 2001, Malaysia ilipunguza idadi ya watu wanaoishi chini ya dola moja kutoka asilimia 56 mpaka kufikia asilimia tatu huku Tanzania ikipunguza kutoka 51 mpaka 46. Katika hatua nyingine, Zitto alikana kuwa, Chadema ni chama cha udini, ukanda, ukabila ila akasisitiza kuwa ni chama cha kitaifa. 

 “Ndugu zangu naomba mnielewe, Chadema si chama cha ukabila, ukanda wala udini bali ni chama cha kitaifa. Hizo ni propaganda za wapinzani wetu,” alisema Zitto baada ya kuulizwa na mmoja wa washiriki kuhusu tuhuma za chama hicho kuwa cha Kikanda.

 “CCM imewahi kudai CUF ni chama cha Waislamu, na sasa wanasema Chadema ni chama cha Wakristo, sasa wao CCM ni chama cha wapagani au cha watu gani?” Alihoji Zitto. Alisema ili kuthibitisha kuwa Chadema si chama cha Kikanda, matokeo ya urais wa mwaka 2010, Dk Wilbroad Slaa aliongoza dhidi ya wagombea urais wengine kwa kupata kura nyingi katika Jimbo la Manyovu mkoani Kigoma na hivyo kufanya kupata asilimia nyingi kuliko sehemu yoyote Tanzania. 

 Chanzo: http://www.mwananchi.co.tz/habari

Arusha Kwa Waka Moto Wafanyabiashara Wavamia Maeneo Kwa NguvuNa: Mahmoud Ahmad, Arusha
 
Wafanyabiashara wadogo almaarufu Machinga, wakiwa wamevamia eneo lililopo pembezoni mwa soko la Kilombero na kuvunja uzio na kujigaiya maeneo hayo kwa ajili ya Biashara. kwani eneo hilo ambalo lipo kwenye mgogoro kati ya halmashauri ya jiji la Arusha na mfanyabiashara mmoja wa jijini hapa, kwenye mahakama ya biashara hajajulikana hatima ya kesi hiyo lakini wafanyabiashara hao teyari wameshavamia eneo hilo. 
 Pichani ni wafanyabiashara hao wakiwa kwenye shughuli mbali mbali za kuandaa eneo hilo kwa ajili ya biashara na wengine teyari wamshapanga katika eneo hilo kama walivyokutwa na kamera yetu jijini Arusha leo Asubuhi

Maisha Yanaendelea

Kihesa Kilolo,Iringa.
Reactions::

Magazeti Leo Alhamisi

Reactions::

Monday, September 24, 2012

Watendaji Wa Kata Na Vijiji Karagwe Walalamikiwa

Enzi zile Kanali Mstaafu Fabian Massawe akiwa Mkuu wa Wilaya ya Karagwe,kabla ya kupanda daraja na kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera.Hapa alikuwa akikabidhi trekta lililotolewa na Rais Jakaya Kikwete kwa wananchi wa Wilaya hiyo

Phinias Bashaya,Karagwe
BAADHI ya wananchi wa Wilaya ya Karagwe wamewalalamikia maofisa watendaji wa vijiji na kata kwa kuwatoza zaidi ya shilingi 30,000 kama gharama za kuandikiwa barua za utambulisho kwenda katika ofisi na taasisi mbalimbali.
Adha hiyo imewakumba zaidi wananchi wanaohitaji barua za utambulisho kutoka kwa maofisa hao ili waweze kupewa malipo ya fidia ya kupisha ujenzi wa barabaraya kiwango cha lami kutoka Kyaka hadi Bugene.
Kwa mujibu wa maelezo ya baadhi ya wananchi ambao tayari wametozwa kiasi hicho cha fedha,walisema huojiwa kwanza kama wametoa michango ya ujenzi wa shule za sekondari za Kata na Zahanati kabla ya kunadikiwa barua za utambulisho.
Walisema mwananchi anayeshindwa kuonyesha stakabadhi za michango mbambali hulazimika kutozwa kuanzia shilingi elfu thelathini ili aweze kuandikiwa barua ya kumtambulisha ili apewe malipo yake.
Pia wananchi wanaohitaji barua za utambulisho kwa ajili ya kuwadhamini ndugu zao katika vituo vya polisi,mahakama na wanaotaka kufungua akaunti za akiba katika Benki hutakiwa kuonyesha stakabadhi za michango au kulipa kiasi icho cha fedha vinginevyo hapewi barua ya utambulisho.
“Hii ni aina mpya ya ufisadi nimeandikiwa barua ya utambulisho na Mtendaji wa Kata baada ya kulipa kiasi cha shilingi elfu thelathini nilihitaji kwenda kumdhamini ndugu yangu kituo cha Polisi”alisema mmoja wa wananchi kutoka Kata ya Bugene.
Baadhi ya wananchi waliolalamika walikiri kuwa hawajawahi kutoa michango ya shughuli za maendeleo kwa zaidi ya mwaka huku wakidai kuwa kiasi cha fedha wanayotozwa ni kubwa mno huku wakionyesha wasiwasi wa matumizi ya fedha hizo pamoja na kuwa wanapewa stakabadhi za malipo.
Pamoja na walalamikaji kuomba majina yao yahifadhiwe kwa hofu ya kupata msukosuko baadaye,mmoja wa wakazi wa Kijiji cha Kishao Justus Daniel alisema utaraibu huo unatumika katika Kata nyingi za Wilaya hiyo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa halmashauri ya Wilaya ya Karagwe Bosco Ndunguru alisema suala la kutoza wananchi fedha kwa ajili ya kuandikiwa barua halipo na kuwataka walalamikaji wafike ofisini kwake na kumtajia majina ya wahusika ili aweze kuwachukulia hatua.
Alisema yuko tayari kurudishia fedha za wananchi endapo watendaji wanaohusika na tuhuma hizo watajulikana  na kuwa ofisi yake iko tayari kuidhinisha barua hizo bila malipo kwani wanalipwa mshahara kwa ajili ya kuwatumikia wananchi.

Maisha yanaendelea

Dr Migiro Afungua mkutano Wa Serikali Za mitaa Jijini Arusha

Naibu Katibu Mkuu aliyemaliza muda wake,Dr Asha-Rose Migiro(wa nne kulia)akiwa katika picha ya pamoja na viongozi mbalimbali kwenye picha ya pamoja baada ya kufungua mkutano wa mawaziri wa serikali za mitaa wa Afrika Mashariki mjini Arusha.
Viongozi mbalimbali wakiwa kwenye mkutano wa mawaziri wa serikali za mitaa wa Afrika Mashariki kwenye hoteli ya Impala mjini Arusha
Naibu Katibu Mkuu aliyemaliza muda wake,Dr Asha-Rose Migiro(wa tatu kushoto)akisalimiana na Afisa elimu Manispaa ya Arusha,Omary Mkombole mara baada ya kuwasili kufungua mkutano wa mawaziri wa serikali za mitaa wa Afrika Mashariki mjini Arusha.

UN Announces Commitment To support Anti-corruption Efforts to Tanzania.

Representative from United Nations in Tanzania.

Director General of Prevention and Combating of Corruption Bureau (PCCB) Dr. Edward Hosea speaking at the stakeholders meeting to validate the Evaluation Report of national Anti-Corruption Strategy and Action Plan (NASCAP) II where he said this process is a solid commitment from the Government, The Private Sector, Civil Society and Development Partners to collectively share the responsibility of tackling the challenges of corruption at its root cause.
Photo by Zainul A. Mzige

Jeshi La Kenya Lakiri Kuua Wasomali Sita Kwa Risasi


JESHI la Kenya limekiri kuwa mwanajeshi wake mmoja amefyatua risasi na kuwaua raia sita wa Somalia juzi. Pamoja na hayo jeshi hilo limesema linafanya uchunguzi na mara baada ya uchunguzi litachukua hatua zinazostahili kwa muhusika. 

Taarifa kutoka nchini Somalia zinasema tukio hilo lilitokea katika Kijiji cha Janaay Abdalla, ambacho kiko umbali wa kilomita sita kutoka Mji wa Kismayo ambao umekuwa ngome kubwa ya wapiganaji wa Al Shabaab. Msemaji wa Jeshi la Kenya, Kanali Cyrus Oguna alikana madai kuwa mauaji hayo yalifanywa kwa maksudi na kuelezea kuwa wanajeshi wake walivamiwa na wanamgambo hao ambao waliwaua wanajeshi wawili wa Kenya. 

Hapo awali Ujumbe wa Umoja wa Afrika wa kudumisha amani nchini Somalia AMISOM, ulisema utachunguza mauaji hayo. Msemaji wa kikosi cha Somalia, Mohemmed Hirsi, alisema mauaji hayo yalitokea wakati Jeshi la Kenya lilipovamiwa na wapiganaji wa Al Shabaab takriban kilomita sitini kutoka kwa ngome kubwa ya kundi hilo. Msemaji wa AMISOM kanali Adi Aden amesema wakati ukweli wa kesi hiyo utakapojulikana watachukua hatua. Msemaji huyo aliongeza kuwa wanajeshi wa Kenya waliwafyatulia risasi wanaume hao waliokuwa wameketi nje ya duka moja katika Kijiji cha Janaay Cabdalla. Wanajeshi wa Kenya na wale wa Somalia awali walivamiwa na wapiganaji wa Al Shebaab huku ripoti zikisema kuwa pande hizo mbili, zilipata majeruhi. 

Kwa mujibu wa msemaji huyo, wanakijiji waliouawa ambao ni wanaume saba hawakuwa wanamgambo bali raia wa kawaida. Taarifa zaidi zinasema kuwa wanaume hao walikuwa wamepiga foleni kununua sukari.Aidha msemaji wa jeshi la Muungano wa Afrika nchini Somalia, (AMISOM) alisema kuwa hawezi kuthibitisha tukio hilo, lakini madai hayo yatachunguzwa. 

Wanajeshi wa Somalia wakiungwa mkono na wale wa Uganda na Kenya pamoja na vikosi vingine kutoka nchi tofauti za Afrika, wanakaribia kuuzingira mji wa Kismayo, na ili waweze kufanikiwa katika kuuteka mjihuo, wanachi wa pale watahitaji kushirikiana nao. Wanajeshi wa Kenya wamewahi kutuhumiwa kwa kuwaua raia wakati wakifanya mashambulizi katika maeneo ya Al Shabaab. Shirika la kuwahudumia wakimbizi UNHCR linakadiria takriban wakimbizi 10,000 wameutoroka mji wa Kismayo katika kipindi cha wiki moja iliyopita. 

             Chanzo -BBC

Maisha Yanaendelea