Katibu wa CCM Wilisoni Mukama
MUKAMA ASEMA KINA MPASUKO MKUBWA KAMA G8, NATO, MAIGE AMLIPUA NAPE, ASEMA NI GAMBA LINALOPASWA KUVULIWA
Amini Yasini, Rufiji na Ahmed Makongo, Kahama
HALI ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), si shwari na Katibu Mkuu wake,
Wilson Mukama amekiri kwamba hivi sasa kina mpasuko mkubwa unaotokana
na makundi yanayofanana na yale ya Umoja wa Kujihami wa Nchi za
Magharibi (Nato) na Umoja wa Mataifa yenye nguvu kubwa kiuchumi duniani
(G8).
Wakati mtendaji mkuu huyo wa chama tawala akitoa kauli hiyo, aliyekuwa
Waziri wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige ameibuka na kumshambulia
waziwazi, Katibu wa Taifa wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Nape
Nnauye akimtuhumu kukiharibu kwa utendaji mbovu, hivyo kutaka ang’olewe
haraka akidai kuwa ni gamba.
Nchi zinazounda G8 ni Marekani, Canada, Ufaransa, Ujerumani, Italia,
Japan, Russia na Uingereza ambazo pia baadhi yao, ndizo zinazounda
Nato, umoja wenye wanachama 28.
Mukama alitoa kauli hiyo juzi wilayani Rufiji wakati akizungumza na
umati wa wananchi na wanachama wa chama hicho waliofurika katika
Viwanja vya Corecu, Kata ya Kibiti.
Alisema baadhi ya wanachama wa CCM wamekuwa ni wasaka madaraka na
wanapokosa huamua kuunda makundi ya uhasama ambayo hawataki kuyavunja
pindi mchakato wa kutafuta mgombea unapomalizika.
“Makundi yaliyoundwa tangu 2005 na 2010 yanaendelea kukitafuna chama,
wanachama wakinyimwa uongozi wanaanza uhasama, hatufiki malizeni
makundi,” alisema.
Alisema makundi hayo pia yako katika Wilaya za Mkuranga na Rufiji,
ambako katika ziara yake amebaini mpasuko mkubwa unaotokana na fitina
na uhasama miongoni mwa wapenzi na makada wa CCM na kusisitiza kwamba
hayafai na ni hatari kwa mustakabali wa chama hicho kikongwe barani
Afrika.
“Nikiwa Mkuranga nilitaarifiwa kuwa kuna makundi ya Nato na G8 na sasa
nimefika Rufiji nimeyakuta makundi hayo. Jamani makundi hayo ya nini?”
Mukama ambaye aliwahi kushika nafasi mbalimbali za kiutendaji zikiwemo
za Ukuu wa Wilaya ya Mafia akimrithi mtangulizi wake Hemedi Mkali,
alisema aliwahi kugombea ubunge wa viti vya Taifa kupitia Juwata
(iliyokuwa Jumuiya ya Wafanyakazi Tanzania), na aliposhindwa alikubali
matokeo.
Alisema Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kusema bila CCM
imara nchi yetu itayumba, akimaanisha kuwa hakuna chama mbadala cha
kuongoza nchi zaidi yake.
Alitoa mfano wa Chama cha Democrat cha Marekani kwamba wanachama wake
hawana kadi, bali mapenzi ya chama yako mioyoni mwao na wanapojiunga
hawafanyi hivyo kwa lengo la kusaka madaraka... “Hii ni tofauti kubwa
na nchi zetu ambako mtu akijiunga na chama kitu kwanza kufikiria ni
kusaka madaraka,” alisema.
Alisema chama hicho kina mkakati madhubuti wa kupambana na watu wachache wanaotaka kukimiliki wakitumia nguvu ya fedha.
Alisema baadhi ya wanachama wa kawaida wamejiona kuwa hawana nafasi
katika chama chao wakiamini kuwa kimetekwa na wenye fedha na kuongeza
kwamba mwanachama wa kawaida hawezi kuongoza bila rushwa.
“Hapana! Chama chetu hakitakubali hali hiyo. Ni hatari sana kwa
mustakabali wa chama chetu na nchi yetu,” alisema na kuongeza kuwa
wanachama wa kawaida wanatakiwa kugombea hata kama hawana fedha.
Alisema chama kipo katika uchaguzi wake wa ndani na kuwataka wanachama
kufanya uamuzi sahihi wa kuchagua viongozi waadilifu wasiotumia rushwa,
kwani kufanya hivyo kunaweza kusababisha kuingia watu katika uongozi
waliotoa rushwa.
Katika mikutano yake hiyo, Mukama alitamba kuwa chama chake hakitishwi
na wapita njia akimaanisha wapinzani wanaodai kuwa hakijafanya kitu.
Alisema CCM ni chama makini na sikivu katika kusikiliza kero za
wananchi akitamba kwamba kimejenga Daraja la Mkapa ambalo limekuwa
kiunganishi kati ya Mikoa ya Lindi, Mtwara na Dar es Salaam na umeme wa
gesi unaotoka kusini ambao wananchi wa Rufiji wananufaika nao kwa
sasa.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Rufiji, Mrisho Matimbwa alisema katika
uchaguzi uliopita wa chama hicho kulikuwa na makundi mawili, ya Bush na
Al Qaeda ambayo kwa sasa yamekufa na kubakia mpasuko katika
halmashauri kuu ambako aliahidi kuutatua.
Maige na Nape
Akizindua matawi mawili ya wakereketwa wajasiriamali wa CCM katika
Kijiji cha Isaka, Kahama, Shinyanga, Maige ambaye ni Mbunge wa Msalala
alimtaka Nape kuacha tabia yake ya kutoa kauli ambazo kwa namna moja au
nyingine zinaelekea kukidhoofisha chama.
Alimtaka kupima utendaji wake tangu alipoishika nafasi hiyo ya Itikadi
na Uenezi na kujiuliza ni wanachama wangapi wameingia ndani ya chama
hicho.
Alisema sasa hivi kuna wimbi kubwa la wanachama wa chama hicho kuhama
na kukimbilia upinzani na kusema ni wajibu wa Nape kupima na kuona kuwa
kazi ya itikadi na uenezi haiwezi na kwani hajui wajibu wake akisema
ni mtu wa kumhurumia.
Maige alisema mbali ya kushindwa kuzuia wimbi la wanachama kukihama CCM
pia hapaswi kuvumiliwa kutokana na kauli yake kwamba hata kama
wanachama watahama wote na akabaki yeye (Nape) peke yake, haitakufa.
Alisema kauli hiyo haikijengi chama, bali kuchochea makundi ambayo
yanaweza kukibomoa.
Alisema akiwa mwana CCM anaona kwamba sasa hivi Nape amekuwa hafanyi
kazi ya uenezi na kukirejeshea haiba na mvuto ambao umepotea kwa
wananchi na kwamba, kazi anayoifanya sasa ni kukuza makundi na kusema
ovyo.
Aliendelea kumshambulia Nape kwa maneno akisema amejenga jeuri, kiburi,
dharau na ulevi wa madaraka huku akidai kwamba kitendo cha CCM
kupoteza wanachama zaidi ya 10,000 kwa wakati mmoja mkoani Arusha na
sehemu nyingine wanachama 3,000 ni ishara ya hatari lakini, Nape
amekuwa akiwaita wanaohama kwamba ni mzigo.
“Huyu Nape ni lazima atupishe. amekifanya chama kama mali yake, yeye
ndiye mwenye jukumu la kueneza sera za chama na kutafuta wanachama
wapya, lakini ndiyo kwanza anasema waachwe waondoke, Chadema wanatamba
kila siku yeye hajali, huyu nasema ni gamba ni bora atupishe,” alisema.
Baada ya mashambulizi hayo, Maige alijitetea kwamba maneno yake dhidi
ya Nape yasitafsiriwe kama ni kuulilia uwaziri: “Ni uchungu nilionao
kwa chama changu kuona kila siku zinavyokwenda ndivyo tunavyopoteza
idadi kubwa ya wanachama, tuliyemkabidhi jukumu la uenezi anasema
hajali, sasa huyu si atupishe mapema kabla mambo hayajaharibika?”
“Nikuombe Mwenyekiti wa CCM Mkoa mzee wangu, Mgeja (Hamis), nafikiri
ninyi wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec ya CCM) mnapaswa
kuchukua hatua haraka juu ya Nape... huyu sasa ni tatizo. Chama
kitawafia hivihivi mkiona, avuliwe gamba maana tukisubiri ajivue
atatuchelewesha, CCM ni wanachama si Nape.”
Wakati Maige akitoa maneno hayo, Mgeja alikuwa ameinamisha kichwa chake
chini huku mikono ikiwa kichwani, lakini wana CCM na wananchi wengine
walikuwa wakishangilia.
Aidha, Maige aliwalaumu viongozi wa CCM katika ngazi ya wilaya na kata
ambao wamekuwa na tabia ya kutowatembelea wananchi katika maeneo yao
kusikiliza kero zao wakisubiri mpaka viongozi wa kitaifa ndipo na wao
wajitokeze.
“Jamani inakuwaje kiongozi mwenezi wa CCM kata ama wilaya anakaa kimya
kabisa hakuna kazi yoyote anayoifanya! Viongozi wa aina hii wasipewe
nafasi kabisa katika uchaguzi ujao. Tupate safu ya viongozi wenye
kukifia chama chetu.”
“Maana kama watu wanakuja na Operesheni Sangara hakuna anayesimama
kujibu, Operesheni Vua Gamba Vaa Gwanda hakuna aliyewajibu wala CCM
haijatafuta operesheni yoyote ile kukabiliana nao, sasa wameanza
Operesheni Movement For Change (M4C), sisi na Nape wetu kimya
tunawaangalia tu wanazoa wanachama. Tuwe makini chagueni viongozi wenye
uchungu na chama,” alisema Maige.
Alipotakiwa kuzungumzia tuhuma hizo za Maige, Nape alisema: “Nasubiri
taarifa rasmi ya chama na nikiyakuta hayo nitajibu. CCM ina taratibu
zake katika utendaji wake wa kazi. Katika taratibu hizo, ziara zote za
viongozi wetu zinaandikiwa taarifa ambayo lazima zipite kwangu. Hayo
unayosema yakinifikia, nitayajibu lakini siwezi kuzungumza bila hakika
kwamba amesema.”
No comments:
Post a Comment