TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Hivi
karibuni chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kilielezea kile
ilichoeleza kuwa ni kutishwa na wimbi la mauaji yanayotishia amani ya
nchi kikidai kuwa jumla ya wanachama wake 15 wameuawa katika wilaya ya
Igunga peke yake.
Madai
hayo ya CHADEMA, pamoja na wanachama wengine na mashabiki wao,
yalitolewa na Mwenyekiti wa chama hicho Freeman Mbowe, ambaye alidai
kuwa mauaji hayo yana mkono wa serikali ya CCM, ambayo kwa madai yao
imeona wazi kuwa upepo wa kisiasa umekiendea vibaya na sasa kinataka
kujiimarisha katika utawala kwa kuua watu wanaoipinga.
Akifungua
kikao cha Baraza Kuu la chama hicho jijini Dar es Salaam Aprili 29
mwaku huu mwenyekiti huyo alifafanua kuwa mbali na kuuawa kwa watu
wanne kwa pamoja na juzi kifo cha mwenyekiti wao wa tawi huko Arumeru
mkoani Arusha, jumla ya wanachama wake 15 wameuawa katika wilaya ya
Igunga peke yake tangu kumalizika kwa uchaguzi mdogo wa jimbo hilo
mwaka jana.
Mbowe
katika maelezo yake alijaribu katika maeneo kadhaa kuihusisha CCM na
au serikali yake katika matukio kadhaa yaliyowakabili baadhi ya
wanachama na viongozi wa Chadema katika maeneo mbalimbali nchini
likiwemo lile la Mbunge Highness Kiwia ambaye Suala lake bado Lipo
mikononi mwa vyombo Vya dola likishughulikiwa.
Katika
sehemu kubwa ya maelezo ya Ndg. Mbowe amejitahidi kuonesha kuwa mauaji
yote yaliyoikabili na yatakayokuwa yakiikabili Chadema kupitia wafuasi
wake yanafanyika kisiasa, Jambo ambalo ni la uzushi, kwani Halina
ushahidi wa kisheria hata kimazingira, wa Moja kwa Moja unaoondosha
ujinai au makosa hayo, na kuwa ni makosa yanayolenga muktadha wa
kisiasa.
Huku
akitaka kuuaminisha umma kuwa huo ndio ukweli, Ndg. Mbowe amesisitiza
kuwa hilo lime kuwa likitekelezwa na CCM kwa lengo la kuwatisha
wananchi kujiunga na chama hicho hoja ambayo haina msingi wowote wa
kiutafiti.
Hivyo
CCM kwa kutambua kuwa Suala la mauaji linabeba Kosa la jinai, na kwa
kuwa Ndg. Mbowe ameshutumu Moja kwa Moja CCM na serikali yake
kuihusisha na mauaji hayo, ni vema sasa nasi tukatoa msimamo wetu dhidi
ya tuhuma, hiyo.
Kwanza,
si busara hata kidogo kuihusisha CCM katika matukio hayo, kwani
uchunguzi unaofanywa na vyombo vya dola umeshindwa mpaka sasa kuhusisha
matukio hayo na siasa, badala ya kuyahusisha na makosa ya jinai ambayo
hufanywa na watu kwa malengo tofauti na yale ambayo Ndg. Mbowe anataka
kuwaaminisha watu.
Pili,
CCM haijawai, haiwezi, na haitakuja fanya jambo lolote lenye lengo la
kuvuruga Amani na Usalama wenye utulivu ndani ya taifa letu, hivyo
uzushi na usingiziaji uliofanywa na Mtu Kama Ndg. Mbowe, si vema
kuuacha kimya, badala yake nimetumia wasaa Huu muhimu Kujibu, na kutoa
ufafanuzi ili Kuupa umma wa watanzania habari sahihi.
Ni
aibu kwa Chama kama Chadema kujitahidi kwa nguvu zote kujaribu kuficha
ukweli wa mauaji yanayotoa roho za watanzania wenzetu kwa kuyapa sura
ya kisiasa. Hizi ni juhudi za makusudi za kutaka kuficha ukweli wa
kinachotokea.
Ni
aibu kwa chama kama Chadema kujaribu kutumia mauaji mabaya kama haya
kutafuta mtaji wa kisiasa. Huku ni kuonyesha jinsi gani wamefilisika
kisiasa mpaka wanafikia mahali pa kuamini kuwa wanaweza kutumia
chochote kama mtaji wa kisiasa, vikiwemo vifo vya watanzania wenzetu.
Huku si kufilisika tu ila kwakweli ni unyama unaotakiwa kulaaniwa na
kila muungwana.
Nape Moses Nnauye
Chama Cha Mapinduzi
Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi CCM
No comments:
Post a Comment