CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) wilayani hapa, kimekutana na wakati
mgumu kwa kuumbuka mbele ya Katibu wa Taifa Itikadi na Uenezi wa chama
hicho, Nape Nnauye ambaye alikuwa mgeni rasmi wakati wa baraza la vijana
la wilaya hiyo lililofanyika Ijumaa.
CCM imeumbuka baada ya vijana wake wilayani hapa kuonesha msimamo wao
ndani ya chama hicho, kwa kususia baraza la vijana lililokuwa
limeandaliwa, ambalo katika hali isiyo ya kawaida liliudhuriwa na wazee
ambao ni pamoja na kina mama, kina baba na watoto.
Baraza hilo lililofanyika kwenye viwanja vya Mashujaa vilivyoko eneo
la Bunazi yalipo makao makuu ya Wilaya Misenyi, vijana wengi wa CCM
walisusia baraza hilo kwa madai ya kutokuwa na imani na serikali iliyoko
chini ya CCM.
Wakati baraza la vijana likiendelea, vijana wengi, hasa ambao ni
wakereketwa wa CCM, walionekana wakizurura ovyo, wakipita maeneo ambayo
baraza lilikuwa likifanyika huku wengine wakiendelea na shughuli zao za
kujipatia kipato.
Vijana waliozungumza na gazeti hili bila kutaja majina yao, waliokutwa
maeneo ya Bunazi karibu kabisa na eneo lilikokuwa linafanyika baraza,
walisema CCM haina mwelekeo, wamechoka nayo kwa kuwa kila siku
inaendelea kuwatelekeza.
Kwa nyakati tofauti, walisema chama hicho kimeshindwa kabisa kulinda
maslahi ya vijana badala yake kimekuwa kikiwatumia kila siku kufanikisha
maslahi yake.
“Mimi ni mkereketwa wa CCM, mbunge wa sasa nimeshiriki kumpigia
kampeni hadi akapita, wengi walioko ndani ya chama wapo kwa ajili ya
kulinda maslahi yao wala si maslahi ya walio nyuma yao,” alisema mmoja
wa vijana.
Kauli za vijana kususia baraza hilo, zilithibitika pale Katibu wa
Umoja wa Vijana CCM wa Wilaya ya Misenyi, Philbert Ngemella aliposema
mbele ya Nnauye kwamba vijana wamesusia baraza hilo kwa madai kwamba
serikali iliyoko chini ya CCM haiwajali na imeshindwa kutafuta namna ya
kuwawezesha kiuchumi.
Aidha, wakati wa baraza hilo, mzee Abdul Mwanandege alimtahadharisha Nape awe makini sana ili CCM isifie kwenye mikono yake.
Alisema CCM ni ya wanachama wote hivyo maamuzi ndani ya chama ni lazima yaende kulingana na matakwa ya wanachama.
Mwanandege alisema mpasuko ulioko ndani ya CCM kwa sasa unatokana na
maamuzi yanayotolewa, ambayo hayaafikiwi na baadhi ya wanachama, na
kuongeza kuwa, ili chama kiendelee kuwa imara kinahitaji umakini zaidi.
Naye Nape akihutubua baraza hilo la vijana alikiri mpasuko mkubwa
ndani ya CCM, akisema ndani ya chama kuna mamluki, ambao ndio chanzo cha
mpasuko.
“Watu hao tunao ndani ya chama na ndio wanatuvuruga ila tutaendelea
kukabiliana nao hata kama chama kitabaki na mtu mmoja, tunataka watu
safi wenye mapenzi ya dhati na chama,” alisema.
Nnauye alisema CCM inaendelea na mkakati wake wa kuwaadabisha wale
inaowabaini kuchangia mpasuko, na kwamba haitamfumbia macho mtu yeyote
atakayeisaliti.
Aliendelea kusema kuwa, CCM haimbembelezi mwanachama yoyote abaki ndani ya chama.
“Nasema anayetaka kuhama ahame, hata kama nitabaki peke yangu chama
kitaendelea kuwepo, CCM si mali ya matajiri, ni mali ya maskini,”
alisema Nape kwa kejeli.
Kauli hiyo ya Nape ilipokelewa kwa hisia tofauti na wanaCCM wachache
walioudhuria baraza hilo, baadhi bila kutaja majina yao, wakisema kwamba
Nape anakimaliza chama kwa kauli zake.
|
No comments:
Post a Comment