Tuesday, May 29, 2012

Washauriwa Kuwakataa Wanaonunua Madaraka




Na Ashura Jumapili,

 Bukoba

WAKAZI wa mkoani Kagera wameshauriwa kuepuka viongozi wanaotumia fedha kununua madaraka kwa kuwa hawana msaada katika jamii.

Badala yake wananchi hao wametakiwa wajiandae kwenye uchaguzi ujao wa Serikali za Mitaa kukipigia kura Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kuanzia ngazi ya vitongoji .

Ushauri huo ulitolewa jana na Mbunge wa Viti Maalumu Conchestera Rwamlaza (CHADEMA) alipowahutubia wakazi wa mkoa huo na viunga vyake kwenye viwanja vya Kemondo.

“Wahaya wenzangu tumekuwa wabovu kiasi hicho kwa kupewa chumvi, vitambaa vya kufunga kichwani?’’ alihoji mbunge huyo.

Alisema taifa linahitaji kuongozwa na chama chenye nguvu na mwelekeo wa kuleta mageuzi ya maendeleo na siyo kingine isipokuwa CHADEMA.

“Ukitaka kujua hali ni mbaya anzia kwenye familia, biashara na ajira hiyo ndio serikali tuliyoiweka madarakani… hatuwezi kujikunyata, tutakuwa waoga hadi lini?” alihoji.

Mjumbe wa mkutano mkuu wa chama hicho Ignas Karashani kutoka Mkoa mpya wa Geita, aliyewataka vijana wa Kemondo kuacha woga katika kutetea haki zao huku akisema CHADEMA si chama cha msimu.

Mwisho

No comments:

Post a Comment