Mzee Leopord Rwizandekwe mkazi wa kijiji cha Katendaguro Tarafa ya Kiziba Wilaya ya Missenyi Mkoani Kagera ambaye mwaka 1965 alitaka kumng'oa mwalimu Nyerere kabla ya jina lake kuenguliwa na vikao vya Chama akisalimiana na Katibu wa Itikadi na uenezi wa CCM ngazi ya Taifa Nape Nnauye aliyetembelea wilaya hiyo wiki iliyopita
Vijana wa Bukoba wamvaa Nape
TAMKO LA VIJANA WA BUKOBA MJINI WAISHIO DAR ES SALAAM
Ujio wa Nape: Kagera Tumedharauliwa na Uzalendo Umedhihakiwa
Tumejaribu kutafakari kwa
kina juu ya nini hasa kilimsukuma Nape kufika Kagera na kushiriki
mazishi ya muasisi wa TAA, mzalendo na mpigania uhuru aliyetelekezwa na
Taifa lake, Dr. Vedasto Kyaruzi na bado ki-ukweli hatujapata majibu.
Tunapata
shida kujua dhima ya safari ya Nape kwa kuwa shughuli hasa alizozifanya
akiwa Kagera zina kinzana kimaadili na kitamaduni na maombolezo ya
misiba ya Kiafrika na hasa misiba ya Kihaya.
Mjumbe
aliyetumwa mahsusi toka mbali kupeleka pole kwenye msiba hategemewi
atumie muda wake mwingi majukwaani kufanya siasa, tena katika mazingira
ya ugenini. Lakini mpita njia ambaye amefahamishwa tukio na akahiari
kufika msibani, akiendelea na shughuli zake si ajabu hata kidogo.
Nape aliingia Bukoba tarehe 25/05/2012. Na ni uungwana kukiri kuwa alifika Kashai-Matopeni msibani kutoa salamu za pole. Lakini baada ya hapo alielekea Missenyi ambako tunaarifiwa alikuwa na mikutano ya hadhara.
Watanzania
mtakumbuka vema kuwa katika mikutano hiyo ndiko Nape alitoa kauli ya
kutokuwa tayari kukabidhi nchi kwa wahuni! Labda ili Watanzania muweze
kupima vema uelewa na akili za Nape, tuwafahamishe kuwa Missenyi ndiko
iliko Kyaka na ambako maziko ya Dr. Kyaruzi yamefanyika.
Tunashindwa kuelewa, hiyo mikutano ilikuwa safisha njia ya mazishi au inahusiana vipi na mtu aliyepeleka ujumbe wa maombolezo?
Linalochanganya
zaidi ni hili la Jumamosi tarehe 26/05/2012. Hii ndiyo siku ambayo Dr.
Kyaruzi alipumzishwa rasmi kaburini alale kwa amani. Lakini kwa Nape
akiwa Kyaka hii ilikuwa siku maalumu ya kutangaza operation yake mpya ya
kisiasa “Vua Gamba, vua Gwanda, Vaa Uzalendo”.
Katika
hili, ukiachilia ukinzani wa matukio kimaadili na kitamaduni, tunapata
mishangao mingine; hivi Nape alikwenda Kyaka kuzika au kuzindua
operation ya kisiasa? Na Je, huyu kijana anahubiri uzalendo upi?
usiokuwa na utamaduni, Uzalendo wa kuwatelekeza na kushindwa kuwaenzi
watu waliopigania uhuru wa nchi hii?
Kama
huo ndiyo uzalendo anaohubiri Nape, basi hauhitaji operation wala
kampeni maana tayari tunao magwiji. Na hapo kwa tafsiri hii, ujio wake
na matukio yake kwenye maeneo ya msiba vinanapata maana halisi.
Katika Taarifa ya Uchaguzi mdogo wa Arumeru Mashariki, Chama
Tawala kimearifiwa kuwa moja ya kosa lililofanyika ni kumteua mgombea
ambaye mila hazikuwa zinampa fursa na tafsiri njema kufanya shughuli
kama ya siasa katika muda mfupi baada ya msiba wa Baba yake.
Ikiwa
kosa hili la Kitamaduni limechangia Chama kupoteza Jimbo, basi pia
chama kiwe tayari kwa makosa ya Nape kupoteza zaidi zaidi ya Kijiji cha
Burifani na Kata nzima ya kyaka. Na hatutoshangaa iwapo Nape au Taasisi
iliyomtuma ikishindwa kuomba radhi!
Mbali
na vioja vya Nape hapo juu, kwa wasifu wa marehemu Dr. Kyaruzi, kila
mmoja atakubaliana nasi kuwa Taasisi yoyote (iwe dola au chama)
kuwakilishwa na mtu wa ngazi ya Nape ni dharau ya hali ya juu na
ichukuliwe ni dhihaka si kwa jamii iliyostaharabika tu, bali hata kwa
watu walipendao Taifa lao na kuuenzi Uzalendo. Inakuwa vigumu kuamini
kuwa pamoja na ugumu wa ratiba, Rais alikosa muwakilishi makini wa hadhi
inayobeba uzito sawia na mchango wa Dr. Kyaruzi katika Taifa hili.
Tukio
hili linaleta hisia za ubaguzi wa Taasisi za dola na chama katika kutoa
uzito kwenye majanga, matatizo na misiba ya watu wa Taifa hili. Ni
majuzi tu Taifa lilipotelewa na Mcheza Sinema nguli ambaye hapo awali
hakuwahi kupata heshima yoyote ya Kitaifa.
Lakini
tuliona jinsi viongozi wa Serikali na Chama walivyohamia msibani na
Serikali kujipa jukumu la kuubeba msiba na shughuli za maziko. Haikupita
muda, Rais akiwa ziarani Marekani, Rais wa Malawi alifariki duniani.
Pamoja na uchovu wa safari tulimwona Rais akiingia nchini na kutoka
kuwahi mazishi ya Rais wa nchi jirani.
Kulingana
na umuhimu wa msiba huu, Rais hakusubiri hata atatue matatizo makubwa
yaliyokuwa yanaikabili serikali yake kiasi cha kutishiwa kuanguka.
Lakini pia ni kawaida kusoma taarifa za Rais anazoandika katika mitandao
ya kijamii kila anapokuwa njiani kuelekea kwenye misiba ya watu wa
kawaida walioko katika maeneo mbalimbali Jijini Dar es Salaam.
Hili
linatuongezea huzuni na kutuongoza kuamini kuwa misiba ya watu wa
maeneo nje na Dar es Salaam haigusi hisia za Rais hata kama ni ya Watu
waliotoa mchango mkubwa kwa Taifa hili.
Haya
yaliyotokea kwa Dr. Kyaruzi alimanusura yatokee pia kwenye msiba wa MKUU
wa Majeshi Mstaafu Jenerali Ernest Mwita Kyaro. Huyu alikufa siku
chache baada ya mazishi ya Kanumba na msiba wake ulikosa sura ya
Kitaifa. Isingekuwa kelele za wana-Mitandao ya Kijamii (MyKj) na
wahandishi wa habari, hata Bunge lisingesimama kwa dakika moja kutoa
salamu.
Tabia
hii ya kutelekeza wazalendo wa Taifa hili inaonekana kumea kwa kasi. Na
uthaminisho wa serikali kwa watu wa Dar es Salaam unaonekana kuwa juu
kuliko wa wale walioko nje ya Dar es Salaam.
Kwa
Tamko hili tunamtaka Nape Nnauye, Katibu Mwenezi wa CCM kama kweli
alikuja kuwakilisha Taasisi yoyote katika msiba wa Dr. Kyaruzi, basi
aiombe radhi jamii yetu kwa dharau kubwa aliyoonyesha katika msiba huu.
Na kama alikuwa mpita njia tu, basi atujuze ili Jamii na historia ya
Taifa imwandike rasmi Dr. Kyaruzi kama muasisi wa TAA na mzalendo
aliyepigania uhuru wa Taifa lake ambaye hakuenziwa wakati wa uhai wake
na hata mazishi yake hayakuhudhuriwa na mwakilishi wa Kitaifa.
Na mwisho tunamtaka Rais wa Jamhuri ya Tanzania kama Taasisi awe Rais wa Watanzania wote; wa Dar es Salaam na Mikoani.
Asiye na utamaduni ni mtumwa. Tanzania ni moja
Imetolewa na:
Erick Mwemezi Kimasha
Mhamasishaji Jamii Mkuu
Vijana wa Bukoba Mjini Waishio Dar es Salaam
Barua Pepe: ekimasha@ksgroup.co.tz
Simu: 0713-177-372
No comments:
Post a Comment