Monday, May 28, 2012

Na Mwandishi wetu 
Bukoba

IMEELEZWA kuwa sababu kuu inayosababisha kuwepo malalamiko mengi vijijini hususani kwa wananchi,inatokana na viongozi wengi kutozingatia misingi ya utawala bora katika ngazi zao za uongozi.

Hayo yalibainishwa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya Bukoba Kapten mstaafu Dauda Kateme, wakati akitoa nasaha za ufunguzi wa semina kwa wenyeviti wa vijiji wapatao 92 kutoka vijiji vilivyo ndani ya halmashauri hiyo.

Kapteni mstaafu Kateme,alibainisha kuwepo malalamiko mengi kwa wananchi,huku akitaja sababu kuu ni viongozi wao kutowashirikisha katika maamuzi,kutoitisha mikutano ya hadhara ili wananchi kufahamu juu ya shughuli za maendeleo yao kijijini.

Alitaja kuwa malalamiko mengi vijijini ni juu ya ugawaji wa ardhi ya kijiji,malalamiko yanayoelekezwa moja kwa moja kwa viongozi wa vijiji,na kuwataka viongozi hao kuacha tabia ya kujichukulia maamuzi ya kuuza ardhi ya vijiji vyao.

Alisema kisheria mwenyemamlaka ya kugawa ardhi kwa mtu ni mkutano mkuu wa kijiji,nao unacho kiwango ambacho haupaswi kufikia maamuzi ya kugawa ardhi mpaka mamlaka husika za halmashauri,jambo ambalo kwa sasa linaenda kinyume kwa kila kijiji kuhusishwa na kugawa ardhi kiholela.

Kateme aliwaomba wenyeviti hao kutoka vijiji 92 kufichueni watendaji wa kata wanaoenda kinyume na maadili ya kazi yao,kwa kutafuna michango ya wananchi hasa katika kuchangia vyumba vya madarasa.

Vile vile aliwashauri kushirikiana na wananchi kuibua miradi ya wananchi,kusimamia maendeleo ya elimu katika vijiji vyao kwa kushirikiana na wakuu wa shule waliomo katika mazingira yao.

"Kamati za shule ziko chini yenu,ombeni wakuu wa shule wawaelezee juu ya maendeleo ya elimu katika mikutano ya wananchi,waambie watendaji wa vijiji wasome ripoti za mapato na matumizi katika mikutano ya wananchi"alisema.

Kwa upande wake mratibu wa semina hiyo Philimon  Magesa, ambaye pia ni afisa utumishi halmashauri ya wilaya Bukoba,alisema mafunzo haya ni mwendelezo wa kuwapatia viongozi hawa kujua misingi ya utawala bora katika uongozi wa serikali za mitaa.

Magesa alisema kuwa mafunzo hayo yalianzia kwa madiwani wa halmashauri,watendaji wa kata na vijiji na kuwafikia wenyeviti wa vijiji lengo kuu likiwa kuwapatia uwezo wa kuendesha shughuli zote za serikali,ikizingatiwa kuwa serikali ngazi ya kijijindicho kitovu cha utawala bora.

Mafunzo hayo yaliyoendeshwa kwa siku mbili katika vituo vya Maruku na Lyamahoro,huku akiendeshwa na mwezeshaji Gabinus Nkwera ambaye pia ni mhadhiri msaidizi taasisi ya uhasibu Tanzania(TIA)yalionekana kueleweka kwa wahusika kwani waliutaka uongozi wa halmashauri ya wilaya kuacha tabia ya kuwahamisha watendaji wanaokuwa wakituhumiwa kutafuna michango ya wananchi na baadala yake halmashauri iwe inawashirikisha viongozi hao wakati wa uhamisho huo ili kuwmbana mtumisha na aweze kurejesha mali za wananchi.

MWISHO

No comments:

Post a Comment