Wednesday, May 9, 2012

Uvccm Kagera Inapokosa Imani Na watendaji Wake

Kagera 
 KAMATI ya utekelezaji ya Jumuiya ya Umoja wa vijana wa Chama Cha Mapindizi (CCM) MKoa wa Kagera (UVCCM) imemkataa katibu wa UVCCM wa Wilaya ya Karagwe kutokana na tuhuma za kushindwa kuwajibika kikamilifu katika shughuli za chama.
 
 
Kauli hiyo ilitolewa jana na mwenyekiti wa UVCCM Mkoa huo Deusidedith Katwale wakati akiongea na waandishi wa habari katika ofisi za CCM mkoani humo.
 
Katwale alisema katika kikao cha kamati ya utekelezaji ya UVCCM mkoa kimeridhia kumkataa Lufunjo Nkinda ambaye ni katibu wa UVCCM Wilaya ya Karagwe kutokana na kushindwa kwake kuwajibika na kukiuka maadili ya Chama chao.
 
Alizitaja baadhi ya tuhuma zinazomkabili katibu huyo kuwa ni pamona na ulevi wa kupindukia,uharibifu wa mali za umma,kuomba michango bila mpangilio na kushindwa kuwaheshimu viongozi na mamlaka zilizo juu yake kichama ambapo pia aliongeza kuwa amekuwa akijipa vyeo ambavyo havipo katika chama cha CCM.
 
“Ukweli anamatatizo makubwa kichama, anajiita katibu wa CCM wa Wilaya idara ya Vijana nafasi ambayo haipo kwenye chama wengine anawambia kuwa yeye ni usalama wa Taifa wa CCM jambo ambalo linatutia doa kama chama ”Alisema Katwale.
 
Alisema kuwa kwa mujibu wa taratibu za Chama na Uvccm katibu huyo ameisha kanywa mara tatu na kushindwa kujirekebisha ambapo mara ya nne aliandikiwa barua na Katibu wa Wilaya kwa ajili ya kumkanya na matokeo yake alimjibu katibu huyo wa Wilaya Anatory Nshange kwa barua ya matusi akimtukana jambo ambalo ni kinyume na taratibu za chama na katiba yake.
 
Alisema kuwa Kamati hiyo ya UVCCM mkoa inawaomba Uvccm makao makuu watumie taratibu za uajiri wamchukue mtu wao na kumpeleka wanakotaka.
 
Kwa upande wake katibu huyo anayetuhumiwa Lufunjo alipohojiwa na waandishi wa habari juu ya tuhuma hizo zinazomkabili alisema kuwa hakuna barua yoyote ambayo aliwahi kutumiwa inayomtuhumu juu ya jambo la aina yoyote na kwamba hajawahi kuitwa kwenye kikao chochote kwa mijubu wa taratibu za jumuiya.
 
“Tuhuma hizo si za kweli mimi nimefanya kazi za kiutendaji katika kata zote arobaini za Wilaya ya Karagwe,kukataliwa na kuondolewa kwangu ni majungu ya baadhi ya wanachama wasiokitakia chama mema.
 
Wakati huo huo kamati hiyo imempongeza Mwenyekiti wa CCM Taifa ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Jakaya Mrisho Kikwete kwa usikivu wake na kuteua baraza jipya la mawaziri ambalo wamedai kuwa wanaimani nalo na wameridhika nalo hususani alivyozingatia kuwaingiza vijana katika baraza hilo .
 
mwisho 

No comments:

Post a Comment