Thursday, May 31, 2012

Waliohusika Vurugu Zanzibar Wachukuliwe Hatua

Moja ya kanisa lililochomwa moto katika vurugu hizo likionekana kwa nadani

BAADA ya vurugu na maandamano  na kuchomwa moto baadhi ya makanisa zilizosababishwa na Kikundi cha Uamsho,Serikali imetakiwa kuunda tume ya kukichunguza kikundi hicho chenye mwuelekeo kama Al-Shabab cha nchini Somalia.
Kauli hiyo ilitolewa na Mkurugenzi wa Taasisi ya Kiislam (TIPF), Sadiq Godigodi, wakishirikiana na  mwanaharakati Chifu Msopa jijini Dar es Salaam jana kuwa wanalaani vugurugu zote zilizosababishwa na kikundi hicho.
"Watanzania tunapaswa kuwa makini na Kikundi hiki kwani sisi tukiwa Waislam tunaifahamu vizuri historia ya Al-Shabab ilivyoaanza kwani walianza kama hivi sasa hatutaki kuingiza nchi hii katika matatizo ya kuuwana kama ilivyotokea nchini Rwanda 1994"alisema Godigodi. 
Alisema wanaitaka serikali kukichunguza kikundi hicho kwa kuwa kinakwenda kinyume na malengo yake, kwani kilianzishwa kwa ajili ya kufanya mihadhara, kueleimisha, maadili ya dini, kufanya ibada  na mambo yote anayohitaji Mungu (Alla SW).
Aidha, wanalaani vurugu zote zilizosababishwa na baadhi ya watu wa Uamsho kwa kusema makanisa hayakutendewa haki hata kidogo kwa kuwa kanisa si serikali wala Tume ya Uchaguzi au Chama cha siasa.
Godigodi alikwenda mbali kwa kusema wanawalani wale wote wanaopinga muungano kwani hata Mwenyezi Mungu anawachukia wote wanaotaka kujitenga au kufanya ubaguzi wa aina yeyote ya Dini, Kabila au rangi, kwani Mwenyezi Mungu  aliwawakea misingi ya kuheshimu dini za watu wengine na wale wasiokuwa na dini.
Godigod alisema Waislama wanakishangaa kikundi hicho kwa kufanya mihadhara ya kuleta chuki kwa baadhi ya Waislama wa Zanzibar kama vile kupinga muungano wa Zanzibar na Tanganyika wakati kuna utaratibu  umewekwa wa kutoa maoni kuhusu suala hilo.
Vile vile kuwakataa baadhi ya watu kutoka Bara wanaoishi kuondoka  Visiwani humo kama walivyosoma katika vyombo vya habari (huu ni ubaguzi), na kupinga utoaji wa maoni kuhusu mchakato wa Katiba mpya. 
Hata hivyo, alisema Zanzibar ni Kisiwa chenye idadi kubwa ya waislam na vyama vikubwa vyenye idadi kubwa ya wanachama ambapo vyama hivyo vina ushawishi kwa wananchi mbalimbali.
Alisema baada ya muafaka wa CCM na CUF Wazanzibar wamekuwa kitu kimoja wakishirikiana kwa kila jambo ni dhahiri kwamba kila Mzanzibari anhitaji maisha ya umoja na ushirikiano.
Hata hivyo kuna taarifa kuwa Serikali ya Mapinzi Zanzibar imesimamisha shughuli zote za  Kikundi hicho cha Uamsho.

Kardinari Rugambwa Kupumzishwa Kwa Amani October 2012

 Mwanaharakati wa masuala ya maendeleo ya mkoa wa Kagera Askofu Methodius Kilaini.
 Kanisa kuu la jimbo katoriki la Bukoba ambalo mwili wa Marehemu Kardinari Rugambwa utazikwa mwaka huu, liko katika manispaa ya Bukoba na sasa linafanyiwa ukarabati mkubwa

Picha ya kardinali Laulean Rugambwa enzi za uhai wake.

CCM Balaa Tupu

Katibu wa CCM Wilisoni Mukama

MUKAMA ASEMA KINA MPASUKO MKUBWA KAMA G8, NATO, MAIGE AMLIPUA NAPE, ASEMA NI GAMBA LINALOPASWA KUVULIWA
Amini Yasini, Rufiji na Ahmed Makongo, Kahama
HALI ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), si shwari na Katibu Mkuu wake, Wilson Mukama amekiri kwamba hivi sasa kina mpasuko mkubwa unaotokana na makundi yanayofanana na yale ya Umoja wa Kujihami wa Nchi za Magharibi (Nato) na Umoja wa Mataifa yenye nguvu kubwa kiuchumi duniani (G8).

Wakati mtendaji mkuu huyo wa chama tawala akitoa kauli hiyo, aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige ameibuka na kumshambulia waziwazi, Katibu wa Taifa wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Nape Nnauye akimtuhumu kukiharibu kwa utendaji mbovu, hivyo kutaka ang’olewe haraka akidai kuwa ni gamba.


Nchi zinazounda G8 ni Marekani, Canada, Ufaransa, Ujerumani, Italia, Japan, Russia na Uingereza ambazo pia baadhi yao, ndizo zinazounda Nato, umoja wenye wanachama 28.


Mukama alitoa kauli hiyo juzi wilayani Rufiji wakati akizungumza na umati wa wananchi na wanachama wa chama hicho waliofurika katika Viwanja vya Corecu, Kata ya Kibiti.


Alisema baadhi ya wanachama wa CCM wamekuwa ni wasaka madaraka na wanapokosa huamua kuunda makundi ya uhasama ambayo hawataki kuyavunja pindi mchakato wa kutafuta mgombea unapomalizika.


“Makundi yaliyoundwa tangu 2005 na 2010 yanaendelea kukitafuna chama, wanachama wakinyimwa uongozi wanaanza uhasama, hatufiki malizeni makundi,” alisema.


Alisema makundi hayo pia yako katika Wilaya za Mkuranga na Rufiji, ambako katika ziara yake amebaini mpasuko mkubwa unaotokana na fitina na uhasama miongoni mwa wapenzi na makada wa CCM na kusisitiza kwamba hayafai na ni hatari kwa mustakabali wa chama hicho kikongwe barani Afrika.


“Nikiwa Mkuranga nilitaarifiwa kuwa kuna makundi ya Nato na G8 na sasa nimefika Rufiji nimeyakuta makundi hayo. Jamani makundi hayo ya nini?”

Mukama ambaye aliwahi kushika nafasi mbalimbali za kiutendaji zikiwemo za Ukuu wa Wilaya ya Mafia akimrithi mtangulizi wake Hemedi Mkali, alisema aliwahi kugombea ubunge wa viti vya Taifa kupitia Juwata (iliyokuwa Jumuiya ya Wafanyakazi Tanzania), na aliposhindwa alikubali matokeo.

Alisema Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kusema bila CCM imara nchi yetu itayumba, akimaanisha kuwa hakuna chama mbadala cha kuongoza nchi zaidi yake.


Alitoa mfano wa Chama cha Democrat cha Marekani kwamba wanachama wake hawana kadi, bali mapenzi ya chama yako mioyoni mwao na wanapojiunga hawafanyi hivyo kwa lengo la kusaka madaraka... “Hii ni tofauti kubwa na nchi zetu ambako mtu akijiunga na chama kitu kwanza kufikiria ni kusaka madaraka,” alisema.


Alisema chama hicho kina mkakati madhubuti wa kupambana na watu wachache wanaotaka kukimiliki wakitumia nguvu ya fedha.


Alisema baadhi ya wanachama wa kawaida wamejiona kuwa hawana nafasi katika chama chao wakiamini kuwa kimetekwa na wenye fedha na kuongeza kwamba mwanachama wa kawaida hawezi kuongoza bila rushwa.


“Hapana! Chama chetu hakitakubali hali hiyo. Ni hatari sana kwa mustakabali wa chama chetu na nchi yetu,” alisema na kuongeza kuwa wanachama wa kawaida wanatakiwa kugombea hata kama hawana fedha.


Alisema chama kipo katika uchaguzi wake wa ndani na kuwataka wanachama kufanya uamuzi sahihi wa kuchagua viongozi waadilifu wasiotumia rushwa, kwani kufanya hivyo kunaweza kusababisha kuingia watu katika uongozi waliotoa rushwa.


Katika mikutano yake hiyo, Mukama alitamba kuwa chama chake hakitishwi na wapita njia akimaanisha wapinzani wanaodai kuwa hakijafanya kitu.


Alisema CCM ni chama makini na sikivu katika kusikiliza kero za wananchi akitamba kwamba kimejenga Daraja la Mkapa ambalo limekuwa kiunganishi kati ya Mikoa ya Lindi, Mtwara na Dar es Salaam na umeme wa gesi unaotoka kusini ambao wananchi wa Rufiji wananufaika nao kwa sasa.


Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Rufiji, Mrisho Matimbwa alisema katika uchaguzi uliopita wa chama hicho kulikuwa na makundi mawili, ya Bush na Al Qaeda ambayo kwa sasa yamekufa na kubakia mpasuko katika halmashauri kuu ambako aliahidi kuutatua.


Maige na Nape


Akizindua matawi mawili ya wakereketwa wajasiriamali wa CCM katika Kijiji cha Isaka, Kahama, Shinyanga, Maige ambaye ni Mbunge wa Msalala alimtaka Nape kuacha tabia yake ya kutoa kauli ambazo kwa namna moja au nyingine zinaelekea kukidhoofisha chama.


Alimtaka kupima utendaji wake tangu alipoishika nafasi hiyo ya Itikadi na Uenezi na kujiuliza ni wanachama wangapi wameingia ndani ya chama hicho.


Alisema sasa hivi kuna wimbi kubwa la wanachama wa chama hicho kuhama na kukimbilia upinzani na kusema ni wajibu wa Nape kupima na kuona kuwa kazi ya itikadi na uenezi haiwezi na kwani hajui wajibu wake akisema ni mtu wa kumhurumia.


Maige alisema mbali ya kushindwa kuzuia wimbi la wanachama kukihama CCM pia hapaswi kuvumiliwa kutokana na kauli yake kwamba hata kama wanachama watahama wote na akabaki yeye (Nape) peke yake, haitakufa. Alisema kauli hiyo haikijengi chama, bali kuchochea makundi ambayo yanaweza kukibomoa.


Alisema akiwa mwana CCM anaona kwamba sasa hivi Nape amekuwa hafanyi kazi ya uenezi na kukirejeshea haiba na mvuto ambao umepotea kwa wananchi na kwamba, kazi anayoifanya sasa ni kukuza makundi na kusema ovyo.


Aliendelea kumshambulia Nape kwa maneno akisema amejenga jeuri, kiburi, dharau na ulevi wa madaraka huku akidai kwamba kitendo cha CCM kupoteza wanachama zaidi ya 10,000 kwa wakati mmoja mkoani Arusha na sehemu nyingine wanachama 3,000 ni ishara ya hatari lakini, Nape amekuwa akiwaita wanaohama kwamba ni mzigo.


“Huyu Nape ni lazima atupishe. amekifanya chama kama mali yake, yeye ndiye mwenye jukumu la kueneza sera za chama na kutafuta wanachama wapya, lakini ndiyo kwanza anasema waachwe waondoke, Chadema wanatamba kila siku yeye hajali, huyu nasema ni gamba ni bora atupishe,” alisema.


Baada ya mashambulizi hayo, Maige alijitetea kwamba maneno yake dhidi ya Nape yasitafsiriwe kama ni kuulilia uwaziri: “Ni uchungu nilionao kwa chama changu kuona kila siku zinavyokwenda ndivyo tunavyopoteza idadi kubwa ya wanachama, tuliyemkabidhi jukumu la uenezi anasema hajali, sasa huyu si atupishe mapema kabla mambo hayajaharibika?”


“Nikuombe Mwenyekiti wa CCM Mkoa mzee wangu, Mgeja (Hamis), nafikiri ninyi wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec ya CCM) mnapaswa kuchukua hatua haraka juu ya Nape... huyu sasa ni tatizo. Chama kitawafia hivihivi mkiona, avuliwe gamba maana tukisubiri ajivue atatuchelewesha, CCM ni wanachama si Nape.”

Wakati Maige akitoa maneno hayo, Mgeja alikuwa ameinamisha kichwa chake chini huku mikono ikiwa kichwani, lakini wana CCM na wananchi wengine walikuwa wakishangilia.

Aidha, Maige aliwalaumu viongozi wa CCM katika ngazi ya wilaya na kata ambao wamekuwa na tabia ya kutowatembelea wananchi katika maeneo yao kusikiliza kero zao wakisubiri mpaka viongozi wa kitaifa ndipo na wao wajitokeze.


“Jamani inakuwaje kiongozi mwenezi wa CCM kata ama wilaya anakaa kimya kabisa hakuna kazi yoyote anayoifanya! Viongozi wa aina hii wasipewe nafasi kabisa katika uchaguzi ujao. Tupate safu ya viongozi wenye kukifia chama chetu.”


“Maana kama watu wanakuja na Operesheni Sangara hakuna anayesimama kujibu, Operesheni Vua Gamba Vaa Gwanda hakuna aliyewajibu wala CCM haijatafuta operesheni yoyote ile kukabiliana nao, sasa wameanza Operesheni Movement For Change (M4C), sisi na Nape wetu kimya tunawaangalia tu wanazoa wanachama. Tuwe makini chagueni viongozi wenye uchungu na chama,” alisema Maige.


Alipotakiwa kuzungumzia tuhuma hizo za Maige, Nape alisema: “Nasubiri taarifa rasmi ya chama na nikiyakuta hayo nitajibu. CCM ina taratibu zake katika utendaji wake wa kazi. Katika taratibu hizo, ziara zote za viongozi wetu zinaandikiwa taarifa ambayo lazima zipite kwangu. Hayo unayosema yakinifikia, nitayajibu lakini siwezi kuzungumza bila hakika kwamba amesema.”

Kikwete Alipofungua Mkutano Wa AFDB Arusha

 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr.Jakaya Mrisho Kikwete akifungua mkutano wa 47 wa mwaka wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) jana mjini Arusha
 Rais wa Serikali ya Jamhuri ya Ivory Cost Dr. Alassane Ouattara (kushoto) akibadilishana mawazo na Rais wa wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) Dr.Donald Kaberuka(kulia) wakati wa sherehe za ufunguzi wa  mkutano wa 47 wa mwaka wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) jana mjini Arusha .

Rais wa wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) Dr.Donald Kaberuka akihutubia wakati wa sherehe za ufunguzi wa  mkutano wa 47 wa mwaka wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) jana mjini Arusha .
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr.Jakaya Mrisho Kikwete(kulia) akibadilishana mawazo na Waziri wa Fedha Dr. William Mgimwa (kushoto)  wakati wa sherehe za ufunguzi wa  mkutano wa 47 wa mwaka wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) jana mjini Arusha .

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr.Jakaya Mrisho Kikwete (kushoto) akipongezwa na Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AFDB) Dr. Donald Kaberuka (kulia) mara baada ya kumaliza kutoa hotuba ya ufunguzi wa  mkutano wa 47 wa mwaka wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) jana mjini Arusha . Katikati ni Rais wa Serikali ya Jamhuri ya Ivory Cost Dr. Alassane Ouattara.

 Picha na Tiganya Vincent-MAELEZO-Arusha

Wednesday, May 30, 2012

Pinda Awatembeza Wakuu Wa Mikoa Na Wilaya Katika Mradi wake wa Nyuki

 WaziriMkuu, Mizengo Pinda akitoa maelezo kuhusu kifaa maalum kinachotumika kukamuwa asali kutoka kwenye masega wakati Wakuu wa Mikoa na Wilya pamoja na Makatibu Tawala wa Mikoa walipotembelea mradi wake wa ufugaji nyuki,eneola Zuzu Dodoma, May 29,2012.(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
 Wakuu wa Mikoa na Wilaya pamoja na Makatibu Tawala wa Mikoa wakitembelea mradi wa ufugaji nyuki katika Shamba la Waziri Mkuu, Mizengo Pinda lililopo eneo la Zuzu Dodoma May 29,2012. Viongozi hao wako Dodoma kwa semina. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Wakuu wa Mikoa na Wilaya pamoja na Makatibu Tawala wa Mikoa wakitembelea mradi wa ufugaji nyuki katika Shamba la Waziri Mkuu, Mizengo Pinda lililopo eneo la Zuzu Dodoma May 29,2012. Viongozi hao wako Dodoma kwa semina. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Tuesday, May 29, 2012

Vijana Wamvaa Nape


Mzee Leopord Rwizandekwe mkazi wa kijiji cha Katendaguro Tarafa ya Kiziba Wilaya ya Missenyi Mkoani Kagera ambaye mwaka 1965 alitaka kumng'oa mwalimu Nyerere kabla ya jina lake kuenguliwa na vikao vya Chama akisalimiana na Katibu wa Itikadi na uenezi wa CCM ngazi ya Taifa Nape Nnauye aliyetembelea wilaya hiyo wiki iliyopitaVijana wa Bukoba wamvaa Nape

TAMKO LA VIJANA WA BUKOBA MJINI WAISHIO DAR ES SALAAM
Ujio wa Nape: Kagera Tumedharauliwa na Uzalendo Umedhihakiwa
Tumejaribu kutafakari  kwa kina juu ya nini hasa kilimsukuma Nape kufika Kagera na kushiriki mazishi ya muasisi wa TAA, mzalendo na mpigania uhuru aliyetelekezwa na Taifa lake, Dr. Vedasto Kyaruzi  na bado ki-ukweli hatujapata majibu.
Tunapata shida kujua dhima ya safari ya Nape kwa kuwa shughuli hasa alizozifanya akiwa Kagera zina kinzana kimaadili na kitamaduni na maombolezo ya misiba ya Kiafrika na hasa misiba ya Kihaya.
Mjumbe aliyetumwa mahsusi toka mbali kupeleka pole kwenye msiba hategemewi atumie muda wake mwingi majukwaani kufanya siasa, tena katika mazingira ya ugenini. Lakini mpita njia ambaye amefahamishwa tukio na akahiari kufika msibani, akiendelea na shughuli zake si ajabu hata kidogo.
Nape aliingia Bukoba tarehe 25/05/2012. Na ni uungwana kukiri kuwa alifika Kashai-Matopeni msibani kutoa salamu za pole.  Lakini baada ya hapo alielekea Missenyi ambako tunaarifiwa alikuwa na mikutano ya hadhara.
Watanzania mtakumbuka vema kuwa katika mikutano hiyo ndiko Nape alitoa kauli ya kutokuwa tayari kukabidhi nchi kwa wahuni! Labda ili Watanzania muweze kupima vema uelewa na akili za Nape, tuwafahamishe kuwa Missenyi ndiko iliko Kyaka na ambako maziko ya Dr. Kyaruzi yamefanyika.
Tunashindwa kuelewa, hiyo mikutano ilikuwa safisha njia ya mazishi au inahusiana vipi na mtu aliyepeleka ujumbe wa maombolezo?
Linalochanganya zaidi ni hili la Jumamosi tarehe 26/05/2012. Hii ndiyo siku ambayo Dr. Kyaruzi alipumzishwa rasmi kaburini alale kwa amani. Lakini kwa Nape akiwa Kyaka hii ilikuwa siku maalumu ya kutangaza operation yake mpya ya kisiasa “Vua Gamba, vua Gwanda, Vaa Uzalendo”.
Katika hili, ukiachilia ukinzani wa matukio kimaadili na kitamaduni, tunapata mishangao mingine; hivi Nape alikwenda Kyaka kuzika au kuzindua operation ya kisiasa? Na Je, huyu kijana anahubiri uzalendo upi? usiokuwa na utamaduni, Uzalendo wa kuwatelekeza na kushindwa kuwaenzi watu waliopigania uhuru wa nchi hii?
Kama huo ndiyo uzalendo anaohubiri Nape, basi hauhitaji operation wala kampeni maana tayari tunao magwiji. Na hapo kwa tafsiri hii, ujio wake na matukio yake kwenye maeneo ya msiba vinanapata maana halisi.
Katika Taarifa ya Uchaguzi mdogo wa Arumeru Mashariki,  Chama Tawala kimearifiwa kuwa moja ya kosa lililofanyika ni kumteua mgombea ambaye mila hazikuwa zinampa fursa na tafsiri njema kufanya shughuli kama ya siasa  katika muda mfupi baada ya msiba wa Baba yake.
Ikiwa kosa hili la Kitamaduni limechangia Chama kupoteza Jimbo, basi pia chama kiwe tayari kwa makosa ya Nape kupoteza zaidi zaidi ya Kijiji cha Burifani na Kata nzima ya kyaka. Na hatutoshangaa iwapo Nape au Taasisi iliyomtuma ikishindwa kuomba radhi!
Mbali na vioja vya Nape hapo juu, kwa wasifu wa marehemu Dr. Kyaruzi, kila mmoja atakubaliana nasi kuwa Taasisi yoyote (iwe dola au chama) kuwakilishwa na mtu wa ngazi ya Nape ni dharau ya hali ya juu na ichukuliwe ni dhihaka si kwa jamii iliyostaharabika tu, bali hata kwa watu walipendao Taifa lao na kuuenzi Uzalendo. Inakuwa vigumu kuamini kuwa pamoja na ugumu wa ratiba, Rais alikosa muwakilishi makini wa hadhi inayobeba uzito sawia na mchango wa Dr. Kyaruzi katika Taifa hili.
Tukio hili linaleta hisia za ubaguzi wa Taasisi za dola na chama katika kutoa uzito kwenye majanga, matatizo na misiba ya watu wa Taifa hili. Ni majuzi tu Taifa lilipotelewa na Mcheza Sinema nguli ambaye hapo awali hakuwahi kupata heshima yoyote ya Kitaifa.
Lakini tuliona jinsi viongozi wa Serikali na Chama walivyohamia msibani na Serikali kujipa jukumu la kuubeba msiba na shughuli za maziko. Haikupita muda, Rais akiwa ziarani Marekani, Rais wa Malawi alifariki duniani. Pamoja na uchovu wa safari tulimwona Rais akiingia nchini na kutoka kuwahi mazishi ya Rais wa nchi jirani.
Kulingana na umuhimu wa msiba huu, Rais hakusubiri hata atatue matatizo makubwa yaliyokuwa yanaikabili serikali yake kiasi cha kutishiwa kuanguka. Lakini pia ni kawaida kusoma taarifa za Rais anazoandika katika mitandao ya kijamii kila anapokuwa njiani kuelekea kwenye misiba ya watu wa kawaida walioko katika maeneo mbalimbali Jijini Dar es Salaam. 
Hili linatuongezea huzuni na kutuongoza kuamini kuwa misiba ya watu wa maeneo nje na Dar es Salaam haigusi hisia za Rais hata kama ni ya Watu waliotoa mchango mkubwa kwa Taifa hili.
Haya yaliyotokea kwa Dr. Kyaruzi alimanusura yatokee pia kwenye msiba wa MKUU wa Majeshi Mstaafu Jenerali  Ernest Mwita Kyaro. Huyu alikufa siku chache baada ya mazishi ya Kanumba na msiba wake ulikosa sura ya Kitaifa. Isingekuwa kelele za wana-Mitandao ya Kijamii (MyKj) na wahandishi wa habari, hata Bunge lisingesimama kwa dakika moja kutoa salamu.
Tabia hii ya kutelekeza wazalendo wa Taifa hili inaonekana kumea kwa kasi. Na uthaminisho wa serikali kwa watu wa Dar es Salaam unaonekana kuwa juu kuliko wa wale walioko nje ya Dar es Salaam.
Kwa Tamko hili tunamtaka Nape Nnauye, Katibu Mwenezi wa CCM kama kweli alikuja kuwakilisha Taasisi yoyote katika msiba wa Dr. Kyaruzi, basi aiombe radhi jamii yetu kwa dharau kubwa aliyoonyesha katika msiba huu. Na kama alikuwa mpita njia tu, basi atujuze ili Jamii na historia ya Taifa imwandike rasmi Dr. Kyaruzi kama muasisi wa TAA na mzalendo aliyepigania uhuru wa Taifa lake ambaye hakuenziwa wakati wa uhai wake na hata mazishi yake hayakuhudhuriwa na mwakilishi wa Kitaifa.
Na mwisho tunamtaka Rais wa Jamhuri ya Tanzania kama Taasisi awe Rais wa Watanzania wote; wa Dar es Salaam na Mikoani.
Asiye na utamaduni ni mtumwa. Tanzania ni moja
Imetolewa na:
Erick Mwemezi Kimasha
Mhamasishaji Jamii Mkuu
Vijana wa Bukoba Mjini Waishio Dar es Salaam
Barua Pepe:       ekimasha@ksgroup.co.tz
Simu:           0713-177-372

Ofisa Wa Benki Ya Posta Nchini Aongea Na Wafanya Biashara Bukoba


Ofisa mkuu wa benki ya posta nchini,Sabasaba Moshinga akiongea na baadhi ya wafanyabiashara wa mkoa wa Kagera.


Ofisa mkuu mtendaji wa benki ya posta CEO, Sabasaba Moshingo akiongea na wafanyabiashara wa mkoa wa Kagera.

 Meneja wa shirika la posta wa mkoa wa Kagera kulia alikuwa ni miongoni mwa walioudhuria kikao cha CEO wa benki ya posta nchini.
 Baadhi ya wafanyabiashara wa mkoa wa kagera.
 Moshingo katika picha ya pamoja na baadhi ya watendaji wa TRA na benki ya posta.
Leonard Shija meneja wa mmoa wa Kagera wa mamlaka ya mapato (TRA)akimpokea ofisa mkuu mtendaji wa benki ya posta nchini Sabasaba Mashingo alipofika ofisini kwake, alisifu mahusiano yaliyopo kati nya TRA na benki ya Posta.PICHA NA AUDAX MTIGANZI

Faru wa JK wang’oa vigogo maliasili

WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki ameanza kutekeleza kwa vitendo kauli yake ya kuisafisha Idara ya Wanyamapori baada ya kuwasimamisha kazi wakurugenzi wanne na askari 28 wa Hifadhi ya Taifa Serengeti, Mara ili kupisha uchunguzi wa tukio la kuuawa kwa faru wawili na kung’olewa pembe.

Faru hao ni miongoni mwa watano ambao Rais Jakaya Kikwete aliwapokea wakitokea Afrika Kusini, Mei 21, 2010 lakini Desemba 21, mwaka huo faru dume aitwaye george aliuawa na pembe zake zilinaswa Mwanza. Faru wengine wanne walipewa majina ya cleo, ethna, lunnar na dume pekee aliyebaki, benj.

Wakati akipokea faru hao waliogharimu Sh7.5 bilioni kuanzia ununuzi hadi kuwasafirisha hadi nchini, Rais Kikwete alisema: “Afrika Kusini imeongeza uwezo kwa Tanzania kwa kuleta faru hao weusi na ongezeko hilo ni la manufaa kwa taifa. Hivyo, tutaimarisha huduma zao na ulinzi utakuwa wa kipekee zaidi yangu mimi.”

Lakini tofauti na ulinzi huo alioahidi Rais, kumekuwa na taarifa za kuawa kwa faru wengine wawili hivi karibuni na mamlaka husika zikaficha tukio hilo hadi liliporipotiwa na vyombo vya habari. Takwimu zinaonyesha tangu mwishoni mwa 2009 hadi Desemba 2010, faru 15 wamekwishauawa.

Balozi Kagasheki alisema jana kwamba amechukua hatua hiyo kutokana na wakurugenzi hao kukaa kimya baada ya tukio hilo na askari hao wakidaiwa kukiuka mkataba wao wa ajira ambao unawataka watoe ulinzi kwa wanyamapori.

“Mkataba wao upo wazi kuwa wanapaswa kuwalinda wanyamapori hao na lolote linalowapata liwapate na wao pia, lakini wanyama wameuawa mwezi mzima umepita na wiki mbili baadaye gazeti linaandika ndipo Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (Tanapa), wanachukua hatua,” alisema.

Waziri Kagasheki pia alisema wahusika hao wameundiwa tume huru ambayo itafanya kazi ndani ya siku 60 na watakaobainika kuhusika kwa namna moja au nyingine, watachukuliwa hatua zaidi za kisheria na wale ambao watathibitika kuwa hawahusiki taratibu nyingine zitafuatwa.

Aliwataja wakurugenzi ambao wamesimamisha kazi kuwa ni Kaimu Mkurugenzi wa Uhifadhi, Justine Hando, Mkurugenzi wa Intelejensia katika Wizara hiyo, Emmly Kisamo, Mkurugenzi wa Hifadhi ya Serengeti, Mtango Mtahiko na Mkurugenzi Mratibu wa Mradi wa faru, Mafuru Nyamalumbati.

Alisema anachukua hatua hizo ambazo ni tofauti na utaratibu wa kawaida kutokana na kukithiri kwa vitendo vya ovyo ambavyo vinaichafua wizara yake.

“Kwanza niliwauliza baada ya kupatikana kwa habari za kuuawa kwa faru hao walichukua hatua gani? Jibu likawa tumewapa siku 14 wajieleze,” alisema Kagasheki na kuongeza kuwa watendaji hao wakamwambia kuwa maelezo hayo yasiporidhisha hatua itakayofuata ni kuundwa tume.

Kagasheki alifafanua kwamba alipohoji muda wa utendaji wa tume hiyo, aliambiwa ni siku 60 jambo ambalo alilikataa na kuchukua uamuzi wa kuwasimamisha ili kupisha uchunguzi huo na kudai kuwa watendaji hao kama wangeachwa wangeweza kuwa na athari zaidi kwa hifadhi na wanyamapori.

Alisema wizara yake haiwezi kufanya kazi kwa woga na kusema yupo vitani akiahidi kupambana kuondoa uozo unaodaiwa kuigubika.

Alisema anajua kuwa kuna mtandao wa ujangili ndani na nje ya nchi ambao una fedha nyingi lakini akasema hatarudi nyuma… “Faru ni moja kati ya viumbe hai ambavyo vipo hatarini kutoweka hivyo kilichotokea hakivumiliki.”

Alisema kuwa mara baada ya kuandikwa kwa habari hizo, walikwenda hadi eneo la tukio na kukuta miili ya wanyama hao wakiwa wameondolewa pembe zao na jirani kukiwa na maganda ya risasi… “Tumewakuta mama na mwanaye wameuawa na pembe zao kuondolewa. Inasikitisha sana.”

Mei 21 akizungumza Dar es Salaam katika uzinduzi wa Bodi ya Ushauri ya Wizara ya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Balozi Kagasheki alionya kwamba angeifumua Idara hiyo ya Wanyamapori huku akipiga marufuku usafirishaji wanyama hai nje ya nchi.

Alisema kama idara hiyo itasimamiwa vizuri kukusanya mapato, inaweza kusaidia kupunguza matatizo ya wananchi.

Jk Ampokea Rais Wa Ivory Coast Jana


Rais Jakaya Mrisho Kikwete akimpokea Rais Allasane Ouattara uwanja wa ndege wa Kimataifa wa  Kilimanjaro jijini Arusha leo, akiwa ni mmoja wa wageni mashuhuri kuhudhuria mkutano wa afDB. Picha na IKULU

Magazeti MagazetiMeya Amtishia Mwandishi Wa Habari

Na Mwandishi Wetu
Bukoba

MEYA wa halmashauri ya manispaa ya Bukoba Anatory Amani ameanza kuwatishia amani waandishi wa habari walioko mkoani Kagera wanaojaribu kueleza ukweli juu ya  miradi ya maendeleo ambayo manispaa hiyo inataka kuitekeleza na kwa kushirikiana na wabia.

Katika hali isiyo ya kawaida meya huyo alimkwida tai mwandishi wa habari wa gazeti la Mtanzania,  Audax Mutiganzi na mfukuza ofisini kwake kwa kumsukuma nje kwa nguvu, alikuwa ameandama na ofisa mkuu mtendaji wa benki ya posta nchini Sabasaba Moshingo aliyekuwa kwenye ziara ya siku mbili mkoani Kagera.

"Toka, toka, toka ofisini kwangu sikutaki unatuandika vibaya wewe ni mtu mbaya kwetu hatukutaki kabisa na kamwe utawahi kukanyaga ofisini kwangu, toka nje ya ufisi yangu maramoja" alisema hiyo huku akinyanyuka kwenye kiti chake na kumkwida mwandishi tai na kumsukuma nje na kufunga mlango kwa nguvu.

Amani alimfukuza mwandishi huyo kwa madai kuwa anaandika habari mbaya zinazohusiana na manispaa hiyo hasa zinazohusina na miradi ya iliyoghubikwa na utata hasa kwa upande wa kanuni na sheria za manunuzi ambayo ni pamojan na ya ujenzi wa soko kuu na wa upimaji wa viwanja.

Meya huyo kabla ya kumfukuza mwandishi huyo alitoa maelekezo kwa kaimu Mkurugenzi wa manispaa ya Bukoba, Steven Nimziirwa alimweleze meneja wa Benki ya posta Maduhu Makoye amueleze mwandishi huyo asiingie kwenye ofisi ya Meya huyo kwa madai hataki kukutana naye.

Nimziirwa alifanya kama alivyoagizwa na meya wake, mwandishi huyo pamoja na taarifa hiyo alikaa kimya akaendelea kutekeleza wajibu wake wa kukusanya taarifa za matukio ya ziara ya ofisa mkuu mtendaji wa benki ya posta nchini.

Mwandishi baada ya kufanyiwa unyama huo na meya alienda moja kwa moja  hadi kituo cha polisi kutoa taarifa juu ya  tukio hilo yenye kumbukumbu namba BU/RB/3161/2012, taarifa hiyo ilifunguliwa kituo kikuu cha polisi.

Meya huyo amekuwa na tabia ya kuwatishia waandishi wa habari, hivi karibuni aliwatishia waandishi wa habari wa kituo cha radio Kasibante kilichoko mkoani Kagera kwa madai ya kuhoji miradi inayotekelezwa na manispaa kwa kushirikiana na wabia.

Amani alipotafutwa ili athibitishe malalamiko yaliyotolewa na mwandishi wa habari simu yake ilikuwa inaita bila kupokelewa, alitumiwa ujumbe mbalimbali wa maandishi kwenye simu yake na waandishi wa habari lakini alikataa kuujubu.

Hivi karibuni gazeti ka Mtanzania lilikuwa likifuatilia kwa karibu miradi ya maendeleo ambayo manispaa inataka kuitekeleza kwa kushirikiana na wabia, gazeti hili lilikuwa linaelezea ukikwaji wa taratibu za manunuzi za kuiteua kampuni ya OGM mwandisi mshauri wa mradi wa ujenzi wa soko kuu la Bukoba.

Katika mradi huo kampuni ya OGM ambayo inadaiwa kutokuwa na sifa za kuufanyia mradi huo usanifu itachota zaidi ya milioni 590.

Mwisho

Washauriwa Kuwakataa Wanaonunua Madaraka
Na Ashura Jumapili,

 Bukoba

WAKAZI wa mkoani Kagera wameshauriwa kuepuka viongozi wanaotumia fedha kununua madaraka kwa kuwa hawana msaada katika jamii.

Badala yake wananchi hao wametakiwa wajiandae kwenye uchaguzi ujao wa Serikali za Mitaa kukipigia kura Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kuanzia ngazi ya vitongoji .

Ushauri huo ulitolewa jana na Mbunge wa Viti Maalumu Conchestera Rwamlaza (CHADEMA) alipowahutubia wakazi wa mkoa huo na viunga vyake kwenye viwanja vya Kemondo.

“Wahaya wenzangu tumekuwa wabovu kiasi hicho kwa kupewa chumvi, vitambaa vya kufunga kichwani?’’ alihoji mbunge huyo.

Alisema taifa linahitaji kuongozwa na chama chenye nguvu na mwelekeo wa kuleta mageuzi ya maendeleo na siyo kingine isipokuwa CHADEMA.

“Ukitaka kujua hali ni mbaya anzia kwenye familia, biashara na ajira hiyo ndio serikali tuliyoiweka madarakani… hatuwezi kujikunyata, tutakuwa waoga hadi lini?” alihoji.

Mjumbe wa mkutano mkuu wa chama hicho Ignas Karashani kutoka Mkoa mpya wa Geita, aliyewataka vijana wa Kemondo kuacha woga katika kutetea haki zao huku akisema CHADEMA si chama cha msimu.

Mwisho

Madiwani Wilayani Missenyi Watimuliwa Katika Jengo La Saccos

CHAMA Cha Mapinduzi(CCM)kimewataka madiwani wa Wilaya ya Missenyi Mkoani Kagera wanaotumia majengo ya vyama vya kuweka na kukopa(Saccos)kama ofisi zao kuondoka katika majengo hayo.

Agizo hilo lilitolewa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho Nape Nnauye siku ya Ijumaa baada ya kupokea malalamiko ya Umoja wa Vijana wa chama hicho(UVCCM)waliodai baadhi ya madiwani wamegeuza majengo ya Saccos kwa ajili ya matumizi ya ofisi zao.
Nape alikuwa Wilayani humo kufungua Baraza la vijana wa UVCCM ambalo pia lilihudhuriwa na wanachama wa chama hicho na viongozi mbalimbali huku kukiwa na mwitikio mdogo wa vijana.
Nape aliwataka madiwani hao kujenga ofisi zao na kuwa wanatakiwa kuondoka katika majengo hayo na kuwa wasisubiri vijana waendelee kulalamikia suala hilo linaloathiri ukuaji wa vyama hivyo.
"Madiwani jengeni ofisi zenu acheni zifanye kazi ya Saccos,kama madiwani mliweza kushawishi wapiga kura wakawachagua tushawishi pia tukujengee ofisi"alisema Nape
Aidha Nape alisema endapo madiwani hao wataendelea kutumia majengo ya Saccos kama ofisi zao wanaweza pia kuhatarisha ukuaji  na lengo zuri la kuanzisha wa vyama hivyo vya kuweka na kukopa.
Awali Katibu wa UVCCM Wilayani Missenyi Philbert Ngemera katika taarifa yake kwa Nape alisema majengo ya Saccos yalioyengwa kila Kata na aliyekuwa mbunge wa Jimbo hilo Dk Diodorus Kamara yametekwa na baadhi ya madiwani na kuzifanya kuwa ofisi zao.
Pia alihainisha changamoto mbalimbali zinazowakabiri vijana  kuwa ni pamoja na upandaji holela wa bidhaa na vijana kukimbia chama hicho kwa madai ya kutowajali huku wakiendelea kuwa na maisha magumu.
Aidha alisema katika baadhi ya maeneo wamekosa vijana wakujitokeza kugombea uongozi kwa kile alichodai ni wengi wao kukosa sifa na kuwa hadi sasa vijana 178 wamekimbia chama hicho na kuhamia Chadema idadi aliyosema ni ndogo ikilinganishwa na vijana wengi wanaoendelea kuiunga mkono CCM.
Kaatika hotuba yake pia Nape aliwaeleza vijana kuwa wana nafasi ya kuchagua viongozi wanaofaa kukiimarisha chama na kuwa wasikubari kurubuniwa hasa katika kipindi hikia mbacho CCM inaendelea na uchaguzi wa ndani.
Mbali na kusema kuwa mageuzi ni lazima ndani ya chama hicho ili kuendana na wakati pia alisema hata wakuu wa Wilaya walioteuliwa hivi karibuni chama kimewaeleza wasifanye mchezo katika maeneo yao kwani nyumbani kwao ni CCM.
Kwa mujibu wa Nape wakuu hao wa wilaya wanatakiwa kufanya kazi kwa masirahi ya chama na kuongeza kuwa ikitokea chama kingine kinachukua dola nacho kinachagua viongozi wake.

Monday, May 28, 2012

Taarifa Kamili Juu Ya Maamuzi Ya Kesi Ya Lulu Juni 16

Msanii wa filamu nchini Elizabeth Michael a.k.a Lulu akiwa Mahakamani mapena leo wakati alipofika kusikiliza mashtaka yake yanayomkabili kuhusiana na tuhuma za mauaji ya msanii mwenzake,Marehemu Steven Kanumba Lulu akiwa mahakamani hapo.Lulu akiwasili Mahakamani hapo.


Mahakama Kuu kanda ya Dar es salaam imepanga kutatoa uamuzi juu ya umri wa msanii wa filamu nchini Elizabeth Michael maarufu kwa jina la Lulu anayekabiliwa na kesi ya mauaji ya msanii mwenzake Steven Kanumba Aprili 7 mwaka huu.

Jaji Fauz Twaib leo alisikiliza mapingamizi ya mawakili wa serikali kuhusiana na maombi ya mawakili wanaomtetea Lulu waliyowasilisha mahakamani hapo kuiomba korti hiyo aidha ichunguze umri wa Lulu anayedai ana miaka 17 au iamuru mahakama ya kisutu kuchunguza.

Baada ya kuwasilishwa maombi hayo leo ilikuwa ni siku ya kusikilizwa maombi mahakamani ambapo wakili Shadrack Kimaro wa Serikali alipinga vikali maombi hayo kuwepo mahakamani hapo akidai kuwa hayakustahili kuwepo na badala yake yatupwe.

Alidai walichofanya ni kinyume cha sheria ilipaswa wakate rufaa kwasababu maombi yalishafika mahakama ya kisutu inakosikilizwa kesi hiyo na kutolewa maamuzi hivyo haikuwa sahihi kufungua maombi mapya wakati sio maombi mapya.

Aliwashauri mawakili wa Lulu aidha kukata rufaa maamuzi ya Kisutu au kuomba maamuzi yale kufanyiwa mapitio. Hata hivyo alidai kifungu cha sheria kilichotumika kuwasilisha maombi hayo sio sahihi ilipaswa kitumike kifungu ambacho kitaipa mamlaka korti hiyo kusikiliza maombi.

Mawakili wa Lulu, Furgence Masawe, Peter Kibatala na Kennedy Fungamtama hawakukubaliana na hayo,ambapo Fungamtama aliiomba mahakama kupokea maombi yao na kutolea uamuzi kwasababu ndiko maombi yao yanakotakiwa kupelekwa.

Aliusoma upya uamuzi uliotolewa Kisutu na kudai kuwa haukuwa uamuzi bali maelekezo ya mahakama na wao wamefata maamuzi hayo yaliyowataka kuwasilisha maombi yoyote Mahakama Kuu kwasababu mahakama ile haina mamlaka ya kusikiliza kesi ya mauaji.

Baada ya kusikiliza mabishano hayo ya kisheria mahakama hiyo imepanga kutoa maamuzi Juni 16 mwaka huu

Vurugu Zanzibar:Mabaki Ya Kanisa Lililochomwa moto
Kanisa la Mpendae. Picha  zote na mjumbe wa jukwaa la Mjengwablog aliye Unguja.

Magazeti MagazetiNape Akihutubia Wilayani missenyi

UVCCM wamtosa Nape Missenyi

na Audax Mutiganzi, Misenyi

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) wilayani hapa, kimekutana na wakati mgumu kwa kuumbuka mbele ya Katibu wa Taifa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Nape Nnauye ambaye alikuwa mgeni rasmi wakati wa baraza la vijana la wilaya hiyo lililofanyika Ijumaa.
CCM imeumbuka baada ya vijana wake wilayani hapa kuonesha msimamo wao ndani ya chama hicho, kwa kususia baraza la vijana lililokuwa limeandaliwa, ambalo katika hali isiyo ya kawaida liliudhuriwa na wazee ambao ni pamoja na kina mama, kina baba na watoto.
Baraza hilo lililofanyika kwenye viwanja vya Mashujaa vilivyoko eneo la Bunazi yalipo makao makuu ya Wilaya Misenyi, vijana wengi wa CCM walisusia baraza hilo kwa madai ya kutokuwa na imani na serikali iliyoko chini ya CCM.
Wakati baraza la vijana likiendelea, vijana wengi, hasa ambao ni wakereketwa wa CCM, walionekana wakizurura ovyo, wakipita maeneo ambayo baraza lilikuwa likifanyika huku wengine wakiendelea na shughuli zao za kujipatia kipato.
Vijana waliozungumza na gazeti hili bila kutaja majina yao, waliokutwa maeneo ya Bunazi karibu kabisa na eneo lilikokuwa linafanyika baraza, walisema CCM haina mwelekeo, wamechoka nayo kwa kuwa kila siku inaendelea kuwatelekeza.
Kwa nyakati tofauti, walisema chama hicho kimeshindwa kabisa kulinda maslahi ya vijana badala yake kimekuwa kikiwatumia kila siku kufanikisha maslahi yake.
“Mimi ni mkereketwa wa CCM, mbunge wa sasa nimeshiriki kumpigia kampeni hadi akapita, wengi walioko ndani ya chama wapo kwa ajili ya kulinda maslahi yao wala si maslahi ya walio nyuma yao,” alisema mmoja wa vijana.
Kauli za vijana kususia baraza hilo, zilithibitika pale Katibu wa Umoja wa Vijana CCM wa Wilaya ya Misenyi, Philbert Ngemella aliposema mbele ya Nnauye kwamba vijana wamesusia baraza hilo kwa madai kwamba serikali iliyoko chini ya CCM haiwajali na imeshindwa kutafuta namna ya kuwawezesha kiuchumi.
Aidha, wakati wa baraza hilo, mzee Abdul Mwanandege alimtahadharisha Nape awe makini sana ili CCM isifie kwenye mikono yake.
Alisema CCM ni ya wanachama wote hivyo maamuzi ndani ya chama ni lazima yaende kulingana na matakwa ya wanachama.
Mwanandege alisema mpasuko ulioko ndani ya CCM kwa sasa unatokana na maamuzi yanayotolewa, ambayo hayaafikiwi na baadhi ya wanachama, na kuongeza kuwa, ili chama kiendelee kuwa imara kinahitaji umakini zaidi.
Naye Nape akihutubua baraza hilo la vijana alikiri mpasuko mkubwa ndani ya CCM, akisema ndani ya chama kuna mamluki, ambao ndio chanzo cha mpasuko.
“Watu hao tunao ndani ya chama na ndio wanatuvuruga ila tutaendelea kukabiliana nao hata kama chama kitabaki na mtu mmoja, tunataka watu safi wenye mapenzi ya dhati na chama,” alisema.
Nnauye alisema CCM inaendelea na mkakati wake wa kuwaadabisha wale inaowabaini kuchangia mpasuko, na kwamba haitamfumbia macho mtu yeyote atakayeisaliti.
Aliendelea kusema kuwa, CCM haimbembelezi mwanachama yoyote abaki ndani ya chama.
“Nasema anayetaka kuhama ahame, hata kama nitabaki peke yangu chama kitaendelea kuwepo, CCM si mali ya matajiri, ni mali ya maskini,” alisema Nape kwa kejeli.
Kauli hiyo ya Nape ilipokelewa kwa hisia tofauti na wanaCCM wachache walioudhuria baraza hilo, baadhi bila kutaja majina yao, wakisema kwamba Nape anakimaliza chama kwa kauli zake.


Na Mwandishi wetu 
Bukoba

IMEELEZWA kuwa sababu kuu inayosababisha kuwepo malalamiko mengi vijijini hususani kwa wananchi,inatokana na viongozi wengi kutozingatia misingi ya utawala bora katika ngazi zao za uongozi.

Hayo yalibainishwa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya Bukoba Kapten mstaafu Dauda Kateme, wakati akitoa nasaha za ufunguzi wa semina kwa wenyeviti wa vijiji wapatao 92 kutoka vijiji vilivyo ndani ya halmashauri hiyo.

Kapteni mstaafu Kateme,alibainisha kuwepo malalamiko mengi kwa wananchi,huku akitaja sababu kuu ni viongozi wao kutowashirikisha katika maamuzi,kutoitisha mikutano ya hadhara ili wananchi kufahamu juu ya shughuli za maendeleo yao kijijini.

Alitaja kuwa malalamiko mengi vijijini ni juu ya ugawaji wa ardhi ya kijiji,malalamiko yanayoelekezwa moja kwa moja kwa viongozi wa vijiji,na kuwataka viongozi hao kuacha tabia ya kujichukulia maamuzi ya kuuza ardhi ya vijiji vyao.

Alisema kisheria mwenyemamlaka ya kugawa ardhi kwa mtu ni mkutano mkuu wa kijiji,nao unacho kiwango ambacho haupaswi kufikia maamuzi ya kugawa ardhi mpaka mamlaka husika za halmashauri,jambo ambalo kwa sasa linaenda kinyume kwa kila kijiji kuhusishwa na kugawa ardhi kiholela.

Kateme aliwaomba wenyeviti hao kutoka vijiji 92 kufichueni watendaji wa kata wanaoenda kinyume na maadili ya kazi yao,kwa kutafuna michango ya wananchi hasa katika kuchangia vyumba vya madarasa.

Vile vile aliwashauri kushirikiana na wananchi kuibua miradi ya wananchi,kusimamia maendeleo ya elimu katika vijiji vyao kwa kushirikiana na wakuu wa shule waliomo katika mazingira yao.

"Kamati za shule ziko chini yenu,ombeni wakuu wa shule wawaelezee juu ya maendeleo ya elimu katika mikutano ya wananchi,waambie watendaji wa vijiji wasome ripoti za mapato na matumizi katika mikutano ya wananchi"alisema.

Kwa upande wake mratibu wa semina hiyo Philimon  Magesa, ambaye pia ni afisa utumishi halmashauri ya wilaya Bukoba,alisema mafunzo haya ni mwendelezo wa kuwapatia viongozi hawa kujua misingi ya utawala bora katika uongozi wa serikali za mitaa.

Magesa alisema kuwa mafunzo hayo yalianzia kwa madiwani wa halmashauri,watendaji wa kata na vijiji na kuwafikia wenyeviti wa vijiji lengo kuu likiwa kuwapatia uwezo wa kuendesha shughuli zote za serikali,ikizingatiwa kuwa serikali ngazi ya kijijindicho kitovu cha utawala bora.

Mafunzo hayo yaliyoendeshwa kwa siku mbili katika vituo vya Maruku na Lyamahoro,huku akiendeshwa na mwezeshaji Gabinus Nkwera ambaye pia ni mhadhiri msaidizi taasisi ya uhasibu Tanzania(TIA)yalionekana kueleweka kwa wahusika kwani waliutaka uongozi wa halmashauri ya wilaya kuacha tabia ya kuwahamisha watendaji wanaokuwa wakituhumiwa kutafuna michango ya wananchi na baadala yake halmashauri iwe inawashirikisha viongozi hao wakati wa uhamisho huo ili kuwmbana mtumisha na aweze kurejesha mali za wananchi.

MWISHO

Sunday, May 27, 2012

People's Power

 Mnyika katika viwanja vya Jangwani wiki iliyopita kama kawaida ya CHADEMA
Wanaume Kazini,hawa ni waandishi wa habari wakichukua matukio katika mkutano mkubwa wa Chadema katika viwanja vya Jangwani Dar es Salaam

Taarifa Ya Serikali Ya Mapinduzi Ya Zanzibar

 Mohammed Aboud Mohammed,  Waziri wa Nchi,  Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Zanzibar.
---
Itakumbukwa kwamba tarehe 25 Aprili, 2012 Kamati Maalumu ya Mawaziri ilikutana na viongozi wa jumuiya ya Uamsho, Maimamu na Masheikh kuzungumzia hali iliyojitokeza nchini katika kufanya mihadhara ambayo ilikuwa inaashiria uvunjifu wa amani.

Katika kikao hicho Serikali iliwataka Viongozi hao wanapofanya mihadhara na mikutano inayohusu masuala ya maoni ya katiba wafuate taratibu zilizowekwa kisheria.

Aidha, Serikali iliwasihi viongozi hao kuepuka matumizi ya lugha na vitendo vinavyoashiria uvunjifu wa amani katika nchi yetu na iliwataka pale ambapo wana maoni yoyote kuhusu Serikali wafuate taratibu zilizowekwa na Serikali itakuwa tayari kuzungumza nao ili kuwa na mustakabali mwema katika nchi yetu.

Vile vile, kupitia taarifa maalumu ya Serikali iliyotolewa Aprili-Mei mwaka huu, Serikali ilieleza wazi kwamba tume ya marekebisho ya katiba imezinduliwa rasmi na kuwataka wananchi, taasisi na vikundi mbali mbali nchini vyenye nia ya kutaka kuelimisha umma kuhusu marekebisho ya katiba kufuata muongozo wa sheria namba 8 ya mwaka jana kama ilivyorekebishwa na sheria namba 2 ya mwaka huu 2012.

Kwenda kinyume na sheria hii ni kosa la jinai na hivyo iliwataka Wananchi wote kujiepusha na vitendo vyote vinavyokwenda kinyume na matakwa ya sheria.

Ndugu Wananchi, mbali na juhudi hizo za Serikali, bado wapo watu wachache wasioitakia mema nchi yetu na umoja uliopo wanaendeleza kwa makusudi vitendo vya kuvunja taratibu za sheria jambo ambalo limepelekea Jeshi la Polisi kuchukua hatua za kisheria.

Ndugu Wananchi, Serikali imesikitishwa na vitendo vilivyojitokeza vya vurugu na uvunjifu wa amani ambavyo vimeelezwa kwa kina na Jeshi la Polisi iliyotolewa mapema leo tarehe 25.05.2012 na Kamishna wa Polisi Zanzibar.

Kutokana na hali hiyo, Serikali inawahakikishia Wananchi wote kwamba itaendelea kudhibiti vitendo vyovyote vya uvunjifu wa sheria vinavyoashiria kuondolea nchi yetu amani na utulivu uliopo.

Ndugu Wananchi, Serikali inawahakikishia Wananchi kwamba Jeshi la Polisi litaendelea kuchukua hatua zifaazo ili kuwahakikishia usalama wa raia na mali zao unakuwepo na hali inaendelea kuwa shuwari, amani na utulivu.

Ndugu Wananchi, bado Serikali inasisitiza na kuwaomba wananchi wote waunge mkono juhudi za Serikali na kuacha kabisa kujiingiza katika vitendo ambavyo vinaashiria uvunjifu wa amani na utulivu katika nchi yetu.

Hivyo, tunawaomba Wananchi waendelee na shughuli zao kama kawaida na Serikali itaendelea kuwahakikishia usalama wao.

Aidha, Serikali inawaomba wazazi kuwadhibiti vijana wao wasijiingize katika vitendo viovu na vurugu kwani Jeshi la Polisi na Vikosi vyote vya Ulinzi na Usalama vitakuwa macho kupambana na vurugu hizo na vitendo vyote vya uvunjifu wa amani.

Kwa madhumuni ya kudhibiti amani na utulivu na usalama wa Wananchi wetu, Serikali katika kipindi hiki itachukua hatua zifuatazo:
  1. Inakataza mikusanyiko ya aina mbalimbali, maandamano, na mihadhara ya aina mbalimbali ambayo haijapata kibali cha Serikali.
  2. Serikali inaliagiza Jeshi la Polisi kuwatafuta na kuwafikisha katika vyombo vya sheria wale wote waliohusika na kufanya fujo zilizotokea katika maeneo mbali mbali ya Zanzibar
  3. Serikali inakemea vikali vitendo vyote vya hujuma na uharibifu wa amali zilizofanywa katika taasisi za umma, dini na mali za watu binafsi.
  4. Serikali inawapa pole Wananchi na Taasisi zilizoathirika na vurugu hizo na kuwahakikishia kuwa hatua kali zitachukuliwa dhidi ya wale wote waliohusika katika kadhia hiyo.

Na mwisho, tunawaomba wananchi kushirikiana na Serikali kwa kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi pale ambapo itaonekana zipo dalili za uvunjifu wa amani katika maeneo yao.

Ahsanteni.

Nawashukuru kwa kunisikiliza.


Mohammed Aboud Mohammed, 
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, 
Zanzibar.
 Jamani Jamani Tumuogope mungu

Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG) liliopo mtaa wa Kariakoo mjini Unguja limechomwa moto jana usiku wa kuamkia leo na watu wasiojulikana.
(Picha/Zanzibar Yetu)
Gari la Kiongozi wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG) Bishop Dickoson Maganga lililochomwa moto na watu wasiojulikana usiku wa jana katika eneo la Kariakoo nje ya kanisa hilo ambapo uharibifu wote unaelezwa kuwa umegharimu shilingi millioni 120.