Faru wa JK wang’oa vigogo maliasili
WAZIRI
wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki ameanza kutekeleza kwa
vitendo kauli yake ya kuisafisha Idara ya Wanyamapori baada ya
kuwasimamisha kazi wakurugenzi wanne na askari 28 wa Hifadhi ya Taifa
Serengeti, Mara ili kupisha uchunguzi wa tukio la kuuawa kwa faru wawili
na kung’olewa pembe.
Faru
hao ni miongoni mwa watano ambao Rais Jakaya Kikwete aliwapokea
wakitokea Afrika Kusini, Mei 21, 2010 lakini Desemba 21, mwaka huo faru
dume aitwaye george aliuawa na pembe zake zilinaswa Mwanza. Faru wengine
wanne walipewa majina ya cleo, ethna, lunnar na dume pekee aliyebaki,
benj.
Wakati
akipokea faru hao waliogharimu Sh7.5 bilioni kuanzia ununuzi hadi
kuwasafirisha hadi nchini, Rais Kikwete alisema: “Afrika Kusini
imeongeza uwezo kwa Tanzania kwa kuleta faru hao weusi na ongezeko hilo
ni la manufaa kwa taifa. Hivyo, tutaimarisha huduma zao na ulinzi
utakuwa wa kipekee zaidi yangu mimi.”
Lakini
tofauti na ulinzi huo alioahidi Rais, kumekuwa na taarifa za kuawa kwa
faru wengine wawili hivi karibuni na mamlaka husika zikaficha tukio hilo
hadi liliporipotiwa na vyombo vya habari. Takwimu zinaonyesha tangu
mwishoni mwa 2009 hadi Desemba 2010, faru 15 wamekwishauawa.
Balozi
Kagasheki alisema jana kwamba amechukua hatua hiyo kutokana na
wakurugenzi hao kukaa kimya baada ya tukio hilo na askari hao wakidaiwa
kukiuka mkataba wao wa ajira ambao unawataka watoe ulinzi kwa
wanyamapori.
“Mkataba
wao upo wazi kuwa wanapaswa kuwalinda wanyamapori hao na lolote
linalowapata liwapate na wao pia, lakini wanyama wameuawa mwezi mzima
umepita na wiki mbili baadaye gazeti linaandika ndipo Mamlaka ya Hifadhi
za Taifa (Tanapa), wanachukua hatua,” alisema.
Waziri
Kagasheki pia alisema wahusika hao wameundiwa tume huru ambayo itafanya
kazi ndani ya siku 60 na watakaobainika kuhusika kwa namna moja au
nyingine, watachukuliwa hatua zaidi za kisheria na wale ambao
watathibitika kuwa hawahusiki taratibu nyingine zitafuatwa.
Aliwataja
wakurugenzi ambao wamesimamisha kazi kuwa ni Kaimu Mkurugenzi wa
Uhifadhi, Justine Hando, Mkurugenzi wa Intelejensia katika Wizara hiyo,
Emmly Kisamo, Mkurugenzi wa Hifadhi ya Serengeti, Mtango Mtahiko na
Mkurugenzi Mratibu wa Mradi wa faru, Mafuru Nyamalumbati.
Alisema
anachukua hatua hizo ambazo ni tofauti na utaratibu wa kawaida kutokana
na kukithiri kwa vitendo vya ovyo ambavyo vinaichafua wizara yake.
“Kwanza
niliwauliza baada ya kupatikana kwa habari za kuuawa kwa faru hao
walichukua hatua gani? Jibu likawa tumewapa siku 14 wajieleze,” alisema
Kagasheki na kuongeza kuwa watendaji hao wakamwambia kuwa maelezo hayo
yasiporidhisha hatua itakayofuata ni kuundwa tume.
Kagasheki
alifafanua kwamba alipohoji muda wa utendaji wa tume hiyo, aliambiwa ni
siku 60 jambo ambalo alilikataa na kuchukua uamuzi wa kuwasimamisha ili
kupisha uchunguzi huo na kudai kuwa watendaji hao kama wangeachwa
wangeweza kuwa na athari zaidi kwa hifadhi na wanyamapori.
Alisema wizara yake haiwezi kufanya kazi kwa woga na kusema yupo vitani akiahidi kupambana kuondoa uozo unaodaiwa kuigubika.
Alisema
anajua kuwa kuna mtandao wa ujangili ndani na nje ya nchi ambao una
fedha nyingi lakini akasema hatarudi nyuma… “Faru ni moja kati ya viumbe
hai ambavyo vipo hatarini kutoweka hivyo kilichotokea hakivumiliki.”
Alisema
kuwa mara baada ya kuandikwa kwa habari hizo, walikwenda hadi eneo la
tukio na kukuta miili ya wanyama hao wakiwa wameondolewa pembe zao na
jirani kukiwa na maganda ya risasi… “Tumewakuta mama na mwanaye wameuawa
na pembe zao kuondolewa. Inasikitisha sana.”
Mei
21 akizungumza Dar es Salaam katika uzinduzi wa Bodi ya Ushauri ya
Wizara ya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Balozi Kagasheki
alionya kwamba angeifumua Idara hiyo ya Wanyamapori huku akipiga
marufuku usafirishaji wanyama hai nje ya nchi.
Alisema kama idara hiyo itasimamiwa vizuri kukusanya mapato, inaweza kusaidia kupunguza matatizo ya wananchi.
No comments:
Post a Comment