Na Mwandishi Wetu
MFUKO
wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) umevishauri vituo vinavyotoa huduma
kwa wanachama wake ambavyo vimetenga maeneo maalum, kuhakisha vinatoa
huduma hiyo kwa wazee katika maeneo hayo ili kuwaepusha na usumbufu
wakati wa kupata huduma za matibabu.
Rai
hiyo imekuwa ikitolewa kwa nyakati tofauti na Mkurugenzi Mkuu wa
Mfuko huo, Emanuel Humba wakati wa kutembelea hospitali, vituo vya
afya na zahanati zilizosajiriwa na Mfuko huo kwa lengo la kujionea
huduma zinazotolewa kwa wanachama wake.
"Lazima
tuwaenzi wazee wetu, wamefanya kazi kubwa ya kuifikisha nchi hii hapa
ilipo hivyo kama Mfuko tungependa kuona mahali wanapotibiwa wanachama
wetu na wazee wetu nao wapate huduma mahali hapo...si vyema kuona
wakitaabika wakati wa kupata matibabu," alisema Humba.
Aliwataka
watoa huduma kuhakikisha wanatumia fursa mbalimbali zinazotolewa na
NHIF kuboresha huduma za matibabu kwa kuwa na vifaa vya kisasa, dawa na
kuboresha mazingira ya vituo hivyo.
"Mfuko
wa Taifa wa Bima ya Afya unatoa fursa ya mikopo ya vifaa tiba na
ukarabati wa majengo ambao unalenga moja kwa moja kuboresha huduma za
matibabu kwa wanachama wetu na wananchi kwa ujumla hivyo ni vyema wazee
wetu nao wakapewa heshima kubwa wakati wa kupata matibabu,"alisema
Humba.
Wakati
huo huo, Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya ameushauri
Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya kuongeza nguvu katika utoaji wa elimu ya
afya kwa wananchi ili kupunguza gharama za matibabu.
Amesema
elimu ya afya itasaidia wanachama na wananchi kwa ujumla kuepukana na
maradhi ambayo yanagharimu fedha nyingi kwa ajili ya matibabu.
"Yapo
maradhi yanayotokana na mtindo wa maisha kama kisukari, shinikizo la
damu ambayo yanaweza kuepukika kwa wanachama wenu kupata elimu tu ya
namna ya kula, kufanya mazoezi na mambo mengine,"alisema Manyanya.
Mfuko
wa Taifa wa Bima ya Afya, hivi karibuni umeendesha mikutano ya wadau
wake katika mikoa mbalimbali nchini,ambayo kwa pamoja wameazimia
kuifanya agenda ya Bima ya Afya kuwa ya kudumu.
Kutoka Fullshangwe
No comments:
Post a Comment