Aidan Mhando
SIKU
moja baada ya Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema) Zitto Kabwe
kutangaza nia ya kugombea urais mwaka 2015, kauli hiyo imewachanganya
watendaji wakuu wa chama hicho, Mwenyekiti Freeman Mbowe na Katibu Mkuu
Dk Willibrod Slaa.
Wakati Dk
Slaa akikosoa hatua hiyo na kusema sio wakati mwafaka sasa kuzungumzia
urais, Mbowe amesema hana tatizo na Zitto kutangaza nia hiyo sasa kwa
kuwa ni haki yake, lakini akahoji haraka ya kutangaza dhamira hiyo.
Hata hivyo,
kwa nyakati tofauti viongozi hao wamemshauri Zitto kufuata taratibu za
chama kama anataka kufikia malengo yake hayo ya kutaka kuwania nafasi
hiyo ya juu kabisa ya uongozi wa taifa.
Kauli ya Dk Slaa
Akizungumzia
uamuzi huo wa Zitto kutangaza dhamira hiyo, Dk Slaa alisema suala la
urais sio muhimu kwa sasa kwani chama kinaangalia ushindi kwenye
uchaguzi mdogo wa Jimbo la Arumeru Mashariki.
"Naomba
niseme hivi, sasa urais sio ‘issue’ (suala). Chama kinaangalia uchaguzi
wa Arumeru Mashariki, muda wa kuzungumzia urais ukifika, tutasema,"
alisema Dk slaa na kuongeza:
“…Naomba
mtambue kwamba tunakabiliwa na suala kubwa la uchaguzi huku Arumeru kwa
hiyo sasa siwezi kuzungumzia suala la urais, hili sio wakati wake sasa.”
Hata hivyo
alimshauri Zitto kufuata taratibu kama ana nia ya kugombea urais na
kufafanua kwamba, chama kina utaratibu wake na ndicho chenye uamuzi wa
mwisho.
“Chadema
ina utaratibu wake kwa kila jambo, kama Zitto ametangaza kugombea urais
2015 huo ni uamuzi wake binafsi. Lakini mimi kama kiongozi wa chama
sioni kama urais ni jambo la kujadili wakati huu.
“Ikifika wakati wakujadili masuala ya urais, tutafanya hivyo kwa undani lakini, sio kwa sasa kwani wakati wake haujafika.”
Mbowe
Kwa upande wake Mwenyekiti Mbowe, alisema kila mtu ana busara na haki zake katika kuamua jambo na hii, ni busara yake Zitto.
Lakini,
Mbowe alionyesha kushangazwa na Zitto kutangaza nia hiyo sasa wakati
ambao chama kinawaza na kufikiria uchaguzi wa Arumeru Mashariki.
Mbowe
alisema haoni tatizo Zitto kutangaza sasa nia ya kuutaka urais kwa kuwa
ni uamuzi na haki yake kwasababu kila mwanachama wa Chadema ana haki ya
kuamua jambo analolitaka ili mradi afuate taratibu.
“Sioni kama
Zitto ana tatizo lolote la kutangaza sasa kwamba mwaka 2015 anataka
kugombea urais kwani ni haki ya kila mtu kugombea nafasi hiyo,” alisema
Mbowe
Hata hivyo,
alifafanua kwamba pamoja na Zitto kutangaza nia, wakati wa kuwania
nafasi hiyo ndani ya chama ukifika wanachama wa Chadema ndio watakaotoa
uamuzi wa nani anafaa.Soma zaidi www.mwananchi.co.tz
No comments:
Post a Comment