Na Mwandishi wetu
Bukoba
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Buhanga kata ya Buganguzi wilayani
Muleba Nestory Samson(Cuf) aliyedaiwa kumuozesha mwanafunzi wa kidato
cha pili amelipotosha jeshi la polisi mkoani Kagera kwakudai kuwa binti
yake hakuwa na uwezo darasani.
Kwa mujibu wa maelezo yaliyothibitishwa na kamanda wa polisi mkoa
wa Kagera Henry Salewi mzazi huyo amedai binti yake alimweleza kuwa
hawezi kuendelea na masomo na hivyo kuamua kuondoka nyumbani.
Alidai binti yake ambaye pia hakufanya mtihani wa kidato cha pili
mwaka huu alimwambia hayuko tayari kuendelea na masomo na hivyo
kumruhusu kwenda sehemu yoyote na kuacha masomo.
Mbali na mwenyekiti huyo kukana madai ya kumuozesha binti yake
aliyekuwa anasoma kidato cha pili sekondari ya Bukidea alisema mtoto
wake alikwenda kutafuta kazi za ndani jijini Mwanza.
Aidha kamanda Salewi amesema kuwa mwenyekiti huyo baada ya kuibuka
kwa taarifa za kumuozesha mtoto wake alifika na mwanafunzi huyo juzi
katika kituo cha polisi Muleba na kutoa maelezo ya kutokuwa tayari
kuendelea na shule kwa madai ya masomo kuwa magumu.
Mwanafunzi huyo ambaye jina lake linahifadhiwa aliacha masomo mwezi
May huku kukiwa na taarifa za familia pamoja na ndugu wa karibu kufanya
njama za kumtorosha na hivyo kukatisha masomo yake.
Hata hivyo Kamanda Salewi hakusema hatua zitakazochukuliwa endapo
binti huyo ataendelea na msimamo wake kutokana na maelezo aliyoyatoa
kituo cha polisi akiwa na mzazi wake.
Mwisho
No comments:
Post a Comment