Na Mwandishi wetu
Bukoba
MABADILIKO ya tabia nchi
nchini Tanzania yameathiri sekta mbalimbali za maendeleo, ikiwemo ukosefu wa umeme
wa uhakika na mafuriko hali inayohitaji nguvu za pamoja ili kuokoa maisha ya
watanzania na dunia kwa ujumla.
Mkurugenzi mtendaji wa
nchi za Afrika juu ya mabadiliko ya tabia nchi (APCCC) Edward Munaaba
alisema hayo mjini Bukoba wakati wa mkutano wa asasi zisizo za kiserikali
zinazojihusisha na mabadiliko ya tabia nchi kutoka mikoa mitano.
Mkutano huo ulilenga kukusanya
maoni juu ya mkakati wa taifa wa mabadiliko ya tabia nchi, ambapo ulizishirikisha
asasi mbalimbali kutoka mikoa ya Mwanza, Mara, Shinyanga, Kigoma na Kagera.
Alisema kutokana
na mabadiliko ya tabia nchi, takribani wizara zote za serikali zimeathirika na
kupelekea wananchi na jamii kwa ujumla wakiwemo wanyama na mimea kupata madhara
makubwa.
Akitolea mfano katika wizara
ya nishati na madini alisema tatizo la kukosekana kwa umeme wa kutosha hapa
nchini kwa siku za karibuni limesababishwa na kupungua kwa maji katika mabwawa
ya kuzalishia nishati hiyo ya umeme.
Kwa mujibu wa mkurugenzi
huyo utafiti uliofanywa na jukwaa la asasi zisizo za serikali zinazojihusisha
na mabadiliko ya tabia nchi ulibaini kuwa kina cha maji katika ziwa Victoria
kimepungua kwa kiasi kikubwa, huku tatizo hilo likiathiri zaidi sekta ya uvuvi.
Alisema ni bora kila mwananchi
nchini kutambua hadhari za mabadiliko ya tabia nchi na kuchukua hatua za
kukabiliana na tatizo hilo kunusuru uchumi wa taifa na maisha ya wananchi na
viumbe vingine.
Wakitoa maoni juu ya mkakati
huo wadau wa mazingira walisema inatakiwa kila sekta kuweka tahadhari mapema
juu dhana ya mabadiliko ya tabia nchi katika mipango yote ya maendeleo kutokana
na kile walichodai kuwa dhana hiyo bado haijapewa kipaumbele.
Walisema umaskini wa
kipato kwa watanzania wengi ndio unasababisha huaribifu wa mazingira, ambapo
walisema asilimia kubwa ya wananchi wanaedelea kukata miti kwa ajili ya
matumizi mbalimbali kutokana na kukusa fedha za kutumia nishati mbadala wakitoa
mfano nishati ya jua na upepo.
Mwisho
No comments:
Post a Comment