MKUU
wa Mkoa wa Mbeya Bw. Abbas Kandoro, amesema mafisadi wanaoiba dawa za
Serikali, kuzipeleka kwenye maduka ya watu binafsi na kusababisha uhaba
mkubwa wa dawa katika Bohari Kuu (MSD), hawawezi kuvumiliwa.
Bw.
Kandoro aliyasema hayo mjini Mbeya wakati akifungua warsha ya siku moja
iliyoshirikisha wadau wa MSD kutoka mikoa ya Singida, Dodoma, Iringa na
Njombe.
Alisema
Serikali imekuwa ikishuhudia uhaba mkubwa wa dawa uliopo MSD wakati
maduka binafsi yanauza dawa za Serikali ambazo haziruhusiwi kuuzwa
katika maduka hayo.
“Kimsingi
Serikali inatumia mabilioni ya fedha kuhakikisha MSD inakuwa na dawa za
kutosha ambazo zitasambazwa katika hospitali ili ziweze kuwasaidia
Watanzania,” alisema.
Aliongeza
kuwa, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii inapaswa kufanya uchunguzi
katika maduka binafsi kubaini mafisadi wa dawa ili wakamatwe na
kufikishwa kwenye vyombo vya sheria iwe fundisho kwa watu wengine wenye
tabia hiyo.
Bw.
Kandoro alisema tabia ya wizi wa dawa unafanywa na watu wasio na nia
njema na uchumi wa nchi ambao unategemea watu wenye nguvu na afya bora
hivyo kinachotakiwa kufanya uchunguzi ili kuwabaini watu wanaofanya
ufisadi wa kuiba dawa MSD.
“Nawaonya
wauzaji dawa katika maduka binafsi kuacha tabia ya kuuza dawa
zilizopita muda wake, kitendo hiki ni sawa na uuaji kwani matumizi yake
ni sawa na sumu mwilini hivyo kusababisha madhara makubwa kwa mtumiaji
kiafya,” alisema.
Kwa
upande wake, Mkurugenzi wa Huduma za Kanda, Bw. Cosmas Mwaifwani,
alisema MSD imejipanga kuhakikisha inawahudumia Watanzania kwa kiwango
stahiki na kukidhi mahitaji yao.
Alisema
katika mpango wa muda mfupi, wamejipanga kuhakikisha wanakuwa na
utaratibu wa kufikisha dawa hadi vituo vya afya kwa ajili ya kumaliza
tatizo la upungufu na upatikanaji wa dawa.
Aliongeza kuwa, mawakala wamekuwa wakichelewa kupeleka maombi ya dawa MSD hivyo kusababisha zisipatikane kwa wakati.
Na Charles Mwakipesile, Mbeya
picha na joseph mwaisango
No comments:
Post a Comment