Wednesday, April 18, 2012

MADIWANI MULEBA WAPITISHA BAJETI YA MWAKA WA FEDHA 2012/13

Na Antidius Kalunde
Muleba

MADIWANI wa halmashauri ya wilaya ya Muleba mkoa wa Kagera Wamepitisha bajeti  ya mwaka 2012/13, ambapo zaidi ya shilingi Bilioni 41.1 zinatarajia kukusanywa kutoka vyanzo mbalimbali ikiwemo ruzuku ya serikali.

Bajeti hiyo iliyowasilishwa na mwenyekiti wa halmashauri hiyo ,  George Katomero iliridhiwa na baraza baada ya kujadiliwa kwa siku mbili April 14/15 na hivyo kutoa nafasi kwa wajumbe wa baraza hilo kuifanyia marekebisho katika masuala kadhaa, ikiwemo matumizi ya mapato yanayotokana na nyanzo vya ndani.

Awali akiwasilisha makadirio ya bajeti hiyo Bw. Katomero alisema kati ya fedha hizo zinazotarajiwa kukusanywa huo, zaidi ya bilioni 3.2 zinatokana na vyanzo vya ndani, huku nyingine zikitarajiwa kupatikana kupitia ruzuku ya serikali kuu na wahisani.

Hata hivyo madiwani hao wamekubaliana kwamba kiasi cha shilingi bilioni moja zitumike katika miradi ya maendeleo badala ya milioni 527.1 zilizotengwa awali kwa miradi lengo likiwa kuboresha maisha wa wakazi wa wilaya hiyo.

Mmoja wa madiwani hao, Justus Magongo wa kata ya Muhutwe alisema hakuna sababu ya halmashauri kutegemea kwa kiasi kikubwa fedha za ruzuku zinazotewa na serikali kuu kwa madai kuwa sio za uhakika katika upatikanaji wake, na kuwa wakati mwingine uletwa kwa kuchelewa.

Aidha madiwani hao waliitaka halmashauri kuongeza nguvu katika ukusanyaji wa mapato ili kufikia lengo hasa kutokana na bajeti ya mwaka huu kuwa na ongezeko la takribani shilingi bilioni 15 kutoka  shilingi 26,236,096,906 kwa mwaka 2011/12 hadi kufikia shilingi 41,118,283,893 mwaka 2012/13.




Mwisho

No comments:

Post a Comment