Friday, April 13, 2012

NILIPOKUTANA NA GAZETI HILI LEO NIMEOGOPA AJINYONGA......

 

NIPASHE:LEMA APEWA CHOPA KIJENGA CHADEMA



Na Sharon Sauwa
12th April 2012

Aliyekuwa Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimempatia aliyekuwa Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, helikopta na vifaa vingine kuzunguka nchi nzima kuhamasisha wananchi kukiunga mkono chama hicho, wakati huu ambapo anasubiri maamuzi ya Mahakama ya Rufaa kuhusu kuenguliwa ubunge wake.
Hayo yalisemwa jana na Mwenyekiti wa Chama hicho, Freeman Mbowe, alipokuwa akihutubia umati wa watu uliofurika katika uwanja wa Barafu mjini hapa.
Mbowe alisema Lema amevuliwa ubunge katika hali ya kutatanisha, lakini wanaamini kuwa haki itatendeka kutoka kwa majaji wa Mahakama ya Rufaa watakapoisikiliza rufaa yao.
Alisema iwapo Mahakama ya Rufaa itabariki maamuzi ya Mahakama Kuu, watakwenda katika uchaguzi na wanaamini kuwa watashinda kwa kishindo.
“Ninajua mna hamu ya kusikia kuhusiana na mbunge wenu Lema, (wananchi wanaitikia ndiyo), tumempatia kazi maalum kwa kumpa helikopta, muziki mkubwa na matarumbeta,” alisema.
“Anakwenda kuamsha ari ya mageuzi nchini, hakuna kulala hadi kieleweke. Wangejua ni balaa kwa hili walilolifanya wangemuacha bungeni,” aliongeza Mbowe huku akishangiliwa na umati wa watu.
Aidha, Mbowe alisema mara baada ya kumalizika kwa Mkutano wa Saba wa Bunge, wabunge wote wa chama chake watakwenda mjini Mwanza kuandaa maandamano makubwa ambayo yatalenga kupinga unyanyasaji unaodaiwa kufanywa na polisi kwa wabunge wao wawili.
Wabunge hao ni Mbunge wa Ukerewe, Salvatory Machemli na Mbunge wa Ilemela, Highness Kiwia walipigwa mapanga usiku wa kuamkia Aprili Mosi mwaka huu, wakati walipokuwa wakisambaza mawakala wa chama hicho katika uchaguzi wa udiwani Kata ya Kirumba.
Kwa upande wake, Mbunge mteule wa Arumeru Mashariiki, Joshua Nassari, alifananisha kitendo cha kumuengua ubunge wa Lema na kuchaguliwa kwake kuwa ni sawa na kuzuia mkuki bungeni na kuingiza bunduki aina ya SMG.
Alisema wabunge wa Chadema ambao yeye ameongeza nguvu, wamedhamiria kuirudisha nchi mahali ambapo Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere, aliiacha na kuwataka wananchi kuwaombea ujasiri ili waweze kutekeleza majukumu yao.
Alisema hawezi kuingia bungeni na kupiga makofi wakati akinamama wanajifungulia katika mazingira mabaya na wanafunzi wanaendelea kukaa chini.
“Arumeru ina shida, CCM wanaleta magari manne yamejaa maji ya kuwasha, Arumeru wanashida ya magari ya kubebea wagonjwa wao wanaleta magari, wananiapisha kesho (leo) ngoma inaanza, hivyo hakuna kulala mpaka kieleweke,” alisema Nassari huku akishangiliwa na wananchi kwa kumuita ‘dogo janja’.
Mbunge wa Ubungo, John Mnyika, alisema hawako tayari kuuziwa mbuzi katika gunia katika suala la uandaji wa katiba mpya.
Alisema kuwa chama chake kitachambua wasifu wa wajumbe wa Tume ya Kuandaa katiba Mpya na kuuweka hadharani ili watu waweze kufahamu.
Mkurugenzi wa Mambo ya Bunge wa chama hicho, John Mrema, alisema iwapo ripoti ya ukaguzi wa hesabu wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), haitawekwa wazi bungeni katika mkutano huu, wao wataiweka hadharani ili umma uweze kufahamu kilichomo ndani ya ripoti hiyo.

No comments:

Post a Comment