Sunday, September 2, 2012

Mauaji Ya Daud Mwangosi: Mkurugenzi wa Vilabu Vya Waandishi Wa Habari Aongea...




 ( Huu ni mchango wa Bw. Karsan kwenye Facebook ya Mjengwa)
Watanzania wenzangu,nachukua fursa hii kuwajulisheni kuwa sisi viongozi wa UTPC,tunakichukulia kitendo hiki katika daraja ya aina yake na katu hatutanyamaza kama baadhi watu wanavyodhani.Hili ni shambulio la kwanza katika historia ya tasnia
ya habari Tanzania ambapo mwandishi wa habari anakufa mikononi mwa mwa maafisa wa umma,anauawa akiwa kazini.Sasa kwanza tumemtuma Rais wetu Kenneth Simbaya aende huko kulikotokea tukio hili na kufanya uchunguzi ambao utatupa picha kamili na ataileta taarifa hiyo kwenye kikao cha Bodi ya Wakurugenzi wa UTPC kitakachofanyika trh 5 sep.Kwenye kikao hicho tutatoa msimamo juu ya jambo hili.Kwa sasa nnawaomba Wastanzania wenzangu,waandishi wenzangu tutulie,lakini nawaambia Hamkani si shwari tena tena.
Wakatabahu,
Abubakar Karsan
Mkurugenzi Mtendaji
Union of Tanzania Press Club
Reactions::

Magazeti Leo Jumatatu

Sitta: Elimu Na Afya Bure Inawezekana



Edwin Mjwahuzi, Kagera
WAZIRI wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta amesema Serikali kutoa huduma ya Elimu na Afya bure inawezekana ikiwa tu mianya ya rushwa na ufisadi itadhibitiwa ipasavyo na wananchi wataweza kunufaika na rasilimali zilizopo nchini.

Sitta alisema ni lazima turudi kwenye misingi ya uadilifu, kujali wanyonge, kukataa rushwa na kukataa ufisadi wa aina yoyote ndipo tutaweza kukusanya na kuinua uchumi wa kutosha na kulipana mishahara mizuri, kumlipa pensheni mzee na kutoa huduma hizo bure.

Aliyasema hayo alipokaribishwa katika mkutano wa akinamama wajane kutoka wilayani Karagwe na Kyelwa mkoani Kagera na kuwashirikisha wazee wa Wilaya hizo uliofanyika katika ukumbi uliopo katika ofisi za CCM wilayani Karagwe.

Sitta alisema itakuwa ndoto za kupata huduma hizo bure kama nchi haitafanikiwa kuziba mianya yote ya rushwa na wananchi wataendelea kupiga kelele wakitaka kupatiwa huduma hizo bila ya mafanikio.

“Ningependa kuwaambia wananchi, najua karibu wote tunataka utoaji wa huduma ya afya, elimu ya kuanzi msingi mpaka elimu ya juu kuwa bure, ndugu zangu katika hali ambayo hata huduma ya afya ya kawaida haipatikani ni mtihani mkubwa kwa kutoa elimu ya bure,” alisema.

Aliongeza, “Hatuwezi kuwa na nchi ina kila kitu, tunayo makaa ya mawe, maziwa, mito, bahari, madini, gesi, mbuga za wanyama, Mlima Kilimanjaro na tuna hekta za kilimo zaidi ya milioni 88, tunataka Watanzania muamke na muache kushabikia rushwa ndogo ndogo tuingie katika utamaduni unaotuwezesha kujenga heshima ya nchi yetu kwa kujali uongozi ulionyooka na wenye uhadilifu.”

Sitta alisema wananchi wasiwe na ndoto ya maisha bora kwa kila mtanzania ikiwa rushwa na ufisadi utaendelea kutawala na kufumbiwa macho.

"Ndugu zangu hatuwezi kupata maisha bora kama kiwango cha rushwa, ufisadi na dhuluma kikiwa hivi hivi tunavyokiona hivi sasa, kwa sababu Serikali ilileta utoaji pembejeo kwa kutumia vocha sasa tutaendelea vipi kama vocha zenyewe zinachakachuliwa?" alihoji.

“Iwapo tutadhibiti mianya ya ufisadi na rushwa, nchi yetu itainuka na kuweza kuwasaidia wazee wetu, wajane, watoto yatima kwa kuwapatia huduma nyingi nzuri, ilimpadi tu ufisadi unatakiwa kupigwa vita kuanzia chini huku,” alisema Sitta.

Sitta pia aliwaomba wajane hao na wazee kupita kila mahali na kuwashaui wananchi wao wakiwemo na wana CCM kuwa makini wa watu wanaojitokeza kuwania nafasi mbalimbali za kisiasa na kiserikali wasije wakafanya makosa kuwaweka watu wenye nia mbaya na nchi hii kwa kujali matumbo yao na familia zao.

“Sasa hivi hata kule bungeni mnaona baadhi ya mawaziri, anatokea mtu amekuwa waziri ndani ya miaka 2 au chini ya hapo unasikia kanunua nyumba Mikocheni ya mabilioni, haiwezekani na wala haingii akilini hakuwa waziri wa wananchi huyu ameingia kuchuma tu,” alisema.

Waziri Sitta amemaliza juzi ziara ya kiserikali ya siku tano mkoani humo alipokuwa akiangalia miradi mbalimbali inayohusiana na muingiliano wa uchumi na kijamii kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC). 
Gazeti Mwananchi jumapili
Reactions::

Sitta Ajibu Kombora La Dkt.Slaa

Nimesikitishwa na kauli za jazba na mwangwi wa kiwewe za Mhe Dr. W Slaa alipokuwa Iringa juzi hadi kuniita mnafiki, mwongo, mtu wa hatari n.k Hali hii inatia mashaka juu ya uwezo wa kiongozi huyo wa kisiasa kuhimili kukosolewa ambayo ni sifa muhimu ya maisha ya mwanasiasa yeyote hususani anapojinadi  kuwa anaweza kuchukua madaraka ya kuiongoza nchi.
Kauli zisizo na staha alizozitoa Dr Slaa dhidi yangu kama vile sifai hata uongozi wa kata zinadhihirisha mambo mawili:
-Dr Slaa ni dicteta. Hana uvumilivu. Ana hulka ya kujiskia kwamba mawazo yake hayapingwi.
-Ni mzushi asiyeogopa kusema na kupindisha mantiki ya jambo ili tu kushinda hoja. Iweje mtu aliyenibembeleza nigombee uraisi kupitia chama chake mwaka juzi leo aseme sifai kuongoza hata kata kwasababu tu nimetamka ukweli juu ya udhaifu wa chama chake cha siasa?
Niliyoyasema pale Karagwe majuzi katika uchambuzi wangu wa vyama vya siasa nchini ni kwamba CHADEMA wamekuwa hodari wa kukosoa na kuishambulia CCM na serikali zake lakini wanasau kuwa ili wawe mbadala kwa kuiongoza nchi hawana budi kurutubisha safu yao ya uongozi nawe na watu wakutosha kuweza kushika madaraka ya ngazi mbalimbali za uongozi wa Taifa. Kuukataa ukweli kwamba safu ya uongozi wa CHADEMA ni nyembamba ni kujidanganya tu.Kupita mikoani kutangaza kwamba matatizo yote ya wananchi yanatokana na CCM ni kazi rahisi na ina mvuto wake kisiasa lakini mwanasiasa makini hana budi kwenda mbele zaidi ya hapo. Hana budi kutuambia wapiga kura mipango ya chama chake inayoeleweka na inayotekelezeka na iliyo makini kukabiliana na changamoto mbalimbali za maendeleo ya nchi. Ahadi za alinacha za tiba bure, elimu bure bila kuonyesha vyanzo halisi vya mapato ni porojo tu. Kusema kwamba raslimali za nchi kama vile gesi asilia, madini, makaa ya mawe, utalii zinatosha kuondoa umaskini ni nadharia tupu ambayo uhalisia wake hauna budi kubainishwa kwa mikakati dhahiri na thabiti ya kiutawala (uendeshaji) inayoweza kuchuma utajiri huo kwa ufanisi, kwa uendelevu na kwa faida ya wengi 1. Kuhusu mwenyekiti Mh Mbowe – MB

Katika hotuba yangu sikukejeli uzoefu wa Mhe Mbowe, wala sijasema Mhe Mbowe ni mcheza disko. Niliuchambua wasifu wa viongozi wa CHADEMA na kutamka uzoefu  wa Mhe Mbowe katika vitega uchumi vya burudani hii siyo kudharau bali ni kutamka ukweli tu.Huwezi kuuelezea wasifu wa Mhe Mbowe bila kuelezea mchango wake mkubwa katika tasnia ya burudani.Mmoja wa maraisi maarufu wa marekani (USA)alikuwa ni mcheza sinema Ronald Reagan.Na hapa Tanzania tulikuwa na mzee R. Kawawa ambaye alianzia katika tasnia ya uigizaji, kwa hiyo Mhe Mbowe au Dr.W. Slaa anaweza akawa Rais wetu kwa maana ya kupigiwa kura za uchaguzi wa demokrasia.Kumudu au kutoyamudu madaraka hayo ni suala tofauti. Tathmini yangu ilihusu safu nzima ya uongozi wa CHADEMA kwa ujumla wao.Ni safu nyembamba mno.

2. Kujiunga na CHADEMA

Kama alivyosema Dr. Slaa Chadema walifanya jitihada ya kunishawishi niingie CHADEMA 2010 na niwe mgombea wao wa Urais. Jambo hili nililitafakari na kutafuta ushauri kwa watu wangu wa karibu na nikabaini kwamba:-
-CHADEMA wana migawanyiko yao ya uongozi tena ni ya hatari kwasababu ni ya kikanda za nchi – yaani nani anatoka wapi.
-Kutokana na yaliomo katika ilani yao ya uchaguzi 2010 – 2015 nilibaini mambo ya kiitikadi ambayo siyakubali kama vile sera ya majimbo. Sera ya majimbo inawezekana katika nchi ambazo ni tajiri na pia isiyo na tofauti kubwa ya hali ya maisha baina ya kanda mbalimbali za nchi kama vile Marekani (USA). Kuleta majimbo Tanzania ambako kuna tofauti kubwa za kimaendeleo baina ya Kaskazini, Mashariki, kati, Kusini na Magharibi ni kusababisha nchi ichanike vipande vipande. Huduma bure za elimu kuanzia chekechea hadi chuo kikuu na huduma bure za afya kwa wote ni ndoto na ni ghilba kwa wananchi. Isitoshe siamini kwamba kazi ya Serikali yoyote Duniani ni kuwalea Wananchi kwa umaskini huku ukiwaahidi huduma za bure badala ya kuwaendeleza wajitume na waongeze kipato ili wamudu gharama za maisha. Kwa hiyo nisingeweza kuwa mgombea Uraisi ndani ya chama ambacho itikadi zake za msingi sikubaliani nazo.
Baada ya hapo nisingeweza eti baada ya uchaguzi Mkuu niombe kugombea Uspika kupitia chama cha CHADEMA.
3. Kuhusu CCJ
Kama ilivyo kawaida kwa vyama vya siasa kutafuta wagombea bora, CCJ ni miongoni mwa vyama vilivyonifuata mimi na baadhi ya wanasiasa wakati wa maandilizi ya uchaguzi mkuu. jambo hili si la siri wala la ajabu na Nimelizungumza hili mara nyingi. Isitokee katika mfumo wa vyama vingi vya siasa mtu kutoka chama kumoja cha siasa na kujiunga na chama kingine haiwezi kusemwa kuwa ni uhaini. Na kama Ningeridhika na mambo yao ningejiunga na CCJ mwaka 2010 lakini sikufanya hivyo. Pia ni uzushi usio na msingi kunihusisha na uanzishaji wa chama hicho. Waanzilishi wa chama hicho cha siasa wanajulikana na wapo hai, ni haki ya kikatiba ya kila Mtanzania kuanzisha au kujiunga Binafsi na chama chochote cha siasa.
4. Madai mengine
Eti nilitamka kwamba ningehamia chadema na Wabunge wa CCM 55 ni porojo za Dr. Slaa kama ulivyo usemi ningeihama CCM siku chache kabla ya kuvunjwa Bunge la 9.
Inashangaza kwa Dr Slaa kukejeli uendeshaji wa bunge la 9 ambalo ndilo lililowapa fursa watu kama yeye kujulikana na kujipatia umaarufu.
Haya madai ya mimi nikiwa Spika kukwamisha uchunguzi wa Meremeta na Richmond ni kutokana na hisia tu za chuki. Taratibu za Kibunge hazimwezeshi Spika kuwa Dikteta anayeamua nini kijadiliwe na nini kisijadiliwe. Yote yapo katika kanunu za Bunge. Maamuzi ya Bunge si lazima yawe ni ya Spika.
Kuhusu ofisi ya Mbunge jimboni Urambo mahasimu wangu ndani ya CCM na nje yake wameng’ang’ania kwa makusudi maalum kuiita ofisi ile kuwa ni ya Spika. Michoro yake na gharama zake hata ukijumuisha samani haifikii tarakimu za ajabu wanazotaja mahasimu wangu kujenga hoja istoshe ofisi hiyo haina maslahi yeyote binafsi kwangu Aidha viongozi wengine waliofikia hadhi za juu mathlani ya uwaziri mkuu nao wamejengewa majimboni ofisi zinazolingana na hiyo 
Porojo nyingine binafsi kama vile kumuhusisha mke wangu kumpigia simu Dr Slaa kumsihi anisaidie kisiasa ni upuuzi wa aina yake unaodhihirisha umahiri wa Dr.Slaa katika siasa za kiwango cha chini.
5. HITIMISHO
Mimi nikiwa mwanasiasa mzoefu na mkongwe nimetoa ushauri na nitaendelea kutoa ushauri kwa makundi mbalimbali nchini.Kuniambia naingilia mambo ya CHADEMA ni kichekesho.Wakiwa wao ni chama cha siasa kinachoendesha harakati za kuwania kuchukua madaraka ya kuongoza nchi ambayo mimi ni raia wasitazamie kuwa sisi wapiga kura tutaacha kuwachambua.Wanalo tatizo kubwa la safu nyembamba mno ya uongozi, Kulingana na majukumu ya kuendesha nchi. Kujilinganisha na safu ya uongozi ya Baba wa Taifa Mwl Julius Nyerere  ni mzaha wako wapi akina R.M Kawawa, Pauli Bomani, George Kahama, Amir Jamal, Solomoni Eliufoo, Tewa Saidi, Tewa Abdallah, Fundikira wa CHADEMA? Kutembea nchi nzima kuhamasisha chuki dhidi ya serikali iliopo madarakani ni jambo jepesi lakini Watanzania walio  makini wanahitaji maelezo ya mipango mbadala ya uchumi kuinua hali za maisha yao na kuiona safu ya uongozi itakayowezesha kwa dhati kubuni na kusimamia mikakati endelevu ya kuondoa umaskini kujenga uchumi imara na kuimarisha umoja wa watanzania

Taswira Kwenye Uchaguzi Wa CCM London






Hapa Anapigwa Mwandishi Daud Mwangosi

Nyololo, Mufindi, jana jioni. Na baadaye ikaripotiwa kuwa ameuawa.Inasikitisha.




Heshima Za Mwisho Kwa Meles Zenawi

Jeneza lenye mwili wa hayati Melezi Zenawi likiletwa uwanjani kwa heshima za mwisho kabla ya maziko yaliyofanyika leo.
Picha: IKULU

Mwenzetu Daud Mwangosi Hatunaye Tena


 
Ndugu zangu,

Jioni ya leo nikiwa katikati ya kufundisha soka ya vijana hapa Iringa nilipigiwa simu na ndugu yangu Allen,  Katibu Wa CHADEMA , Iringa,  akinitaarifu tukio la vurugu zilizotokea Nyololo, Mufindi na hata kifo cha Mwanahabari mwenzetu, mpiganaji  Daud Mwangosi ambaye pia  ni Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari hapa Iringa. Kuondoka kwake kutaacha pengo kubwa. Inasikitisha sana.  Ni juzi tu nilikutana na kusalimiana nae nje ya ofisi zake kwenye jengo la Mwamoto.

Pole zangu binafsi kwa familia yake ya karibu na mbali.  Tuko nao katika wakati huu mgumu kwao.
Chini hapa ni baadhi ya picha nilizopata kumpiga Daud Mwangosi katika uhai wake.
Maggid Mjengwa,
Iringa
0788 111 765

Gazeti La Nyakati Kumbe Laweza Kujirekebisha!



Nimeandika mara kadhaa na hapa narejea tena hadi nikiona kuwa  wahusikawanaanza kuelewa.wiki hii gazeti la nyakati kidogo limeacha kuhubiri ushetani wa freemason na japo bado hawajaacha kabisa lakini walau hawana habari kubwa mbele wiki hii ikitukuza Abrakadabra.Na kama vile mapunguwani gazeti jingine tena nalo likijiita la kikristo la msema kweli linaanza upuuzi uleule.Jamani tusiwaunge mkono wakomunisti waliposema dini ni bangi.
Ludovick

Taswira Za Vurugu Zilizotokea Leo Nyololo, Mufindi

Picha : Francis Godwin

No comments:

Post a Comment