Monday, September 3, 2012

Magazeti Magazeti

Mawaziri Vitani Uchaguzi CCM

KINYANG’ANYIRO cha kuwania nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimepamba moto baada ya mawaziri wa Serikali ya Awamu ya Nne kujitosa kuwania nafasi hizo. Pazia la uchukuaji na urejeshaji wa fomu lilifungwa Alhamisi iliyopita na mpambano mkali upo katika kuwania uongozi wa Halmashauri Kuu ya CCM (Nec) kupitia kapu maalumu maarufu kundi la kifo.

Kundi hili limegonganisha mawaziri kadhaa pamoja na makada wa CCM maarufu wakiwania nafasi 10. Waliojitosa katika kinyang’anyiro hicho kupitia kundi la kifo ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uratibu wa Bunge), William Lukuvi, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe na Waziri wa Nchi, Ofisi (Uhusiano na Uratibu), Stephen Wassira.

Nafasi nyingine zenye ushindani katika uchaguzi huo ndani ya chama hicho ambazo baadhi ya mawaziri wamejitosa ni jumuiya za chama hicho, Umoja wa Vijana (UVCCM), Wanawake (UWT) , Wazazi na ujumbe wa Nec kupitia wilaya.

Taarifa za uhakika kutoka ndani ya chama hicho zinaeleza kuwa baadhi ya mawaziri na vigogo, wamelikimbia kundi la kifo na kugeukia ama jumuiya hizo au wilaya zao. Hatua hiyo imetokana na mabadiliko ya Katiba yaliyofanywa na CCM ambayo yanaonyesha kwamba kundi hilo sasa litakuwa na viti 10 tu badala ya 20 vya awali.

Vigogo wengine waliojitosa katika uchaguzi huo ni pamoja na Waziri wa Ofisi ya Rais (Kazi Maalumu), Profesa Mark Mwandosya aliyechukua fomu kuwania ujumbe wa Nec kupitia Wilaya ya Rungwe, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi ambaye anawania ujumbe wa Nec kupitia Wilaya ya Songea na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Dk Terezya Huvisa anayewania nafasi ya uenyekiti wa UWT taifa.

Chanzo: http://www.mwananchi.co.tz

Hii Ndiyo Mandhari Ya Bandari


Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  ambaye pia ni Mwenyekiti wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama (Troika) ya Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) akimuonesha   Rais Armando Guebuza wa Msumbiji mandhari ya Bandari ya Dar es salaam kutoka  katika hoteli ya Kilimanjaro Hyatt Regency,  baada ya kuwasili leo Septemba 3, 2012  tayari kwa mkutano wa Troika ya SADC unaotarajiwa kufanyika kesho Septemba 4, 2012 hotelini hapo na kuhudhuriwa na viongozi wa nchi wajumbe wa Asasi hiyo ambao ni Msumbiji ambao ni Mwenyekiti wa sasa wa SADC, Afrika Kusini aliyekuwa Mwenyekiti wa Asasi hiyo kabla ya Tanzania,  Namibia ambao ni Makamu Mwenyekiti wa Asasi hiyo ya Troika, pamoja na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) ambao ni wageni waalikwa.

                                    PICHA NA IKULU

Afrika Msiba Ni Wa Wote....


Huwakutanisha watu bila kujali....
tofauti zao za kikabila, kidini na hata uhasama wao wa kisiasa. Pichani ni nyumbani kwa marehemu Daud Mwangosi, jana jioni.

Nyumba Ya Marehemu Daud Mwangosi


Trm, Mtwivila, Iringa.


Taarifa Ya Jukwaa La Wahariri Kuhusu Kuuawa Kwa Mwandishi Daudi Mwangosi


TAARIFA YA JUKWAA LA WAHARIRI (TEF) KWA VYOMBO VYA HABARI
KUHUSU KUUAWA KWA MWANDISHI DAUDI MWANGOSI
  UTANGULIZI:

1. Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), limepokea kwa masikitiko makubwa kifo cha mwandishi wa habari wa Kituo cha Televisheni cha Channel Ten, mkoani Iringa, Daudi Mwangosi.
2. Mwangosi ambaye pia alikuwa Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari mkoa wa Iringa (IPC), aliuawa akiwa kazini jana, Septemba 2, 2012, wakati polisi walipokuwa wakiwadhibiti wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
3. Tukio hili linaiingiza Tanzania katika historia mbaya ya ukiukwaji na ukandamizwaji wa uhuru wa habari, kwani ni kwa mara ya kwanza tunashuhudia mwandishi wa habari AKIUAWA WAKATI AKITEKELEZA MAJUKUMU YAKE YA KIHABARI.

4. Taarifa za awali zinaonyesha kuwa Mwangosi kabla ya kufikwa na mauti saa 9.30 alasiri katika kijiji cha Nyololo, Mufindi, alizingirwa na kushambuliwa na polisi waliokuwa katika eneo la tukio. Na hata alipopiga kelele za kuomba msaada, hakusikilizwa na matokeo yake aliuawa na kitu kinachodhaniwa kuwa ni bomu.
5. Kwa kushirikiana na Baraza la Habari Tanzania, TEF tumechukua hatua za haraka za kuunda timu ya uchunguzi wa suala hilo, ambayo itakwenda mkoani Iringa mapema kadri itakavyowezekana, ili kubaini ukweli wa tukio hilo. Lengo la uchunguzi huo ni kuweka kumbukumbu sahihi (documentation) ya tukio hilo la aina yake katika historia ya nchi yetu.

6. Matokeo ya uchunguzi huo pamoja na mwingine unaofanywa na Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), ndiyo yatakayotoa mwelekeo wa hatua ambazo TEF inachukua dhidi ya Jeshi la Polisi katika siku chache zijazo.
MTIZAMO NA MSIMAMO WA TEF

Kwa kuzingatia taarifa kutoka Iringa na zile za vyombo vya habari vya jana (Jumapili, Septemba 02, 2012) na leo (Jumatatu, Septemba 03, 2012), TEF ina mtizamo na msimamo kama ifuatavyo:

1. Kwanza tunalaani vikali tukio la kupigwa, kisha kuuwawa kwa mwandishi Daudi Mwangosi ambalo limeigusa tasnia ya habari kwamba sasa pengine waandishi wa habari ni malengo “target ya polisi” wanapokuwa kwenye kazi zao.

2. Ieleweke wazi kwamba matukio haya siyo yanaondoa imani ya waandishi wa habari kwa jeshi la polisi tu, bali yanaweza kuwa chanzo cha uhasama na ufa mkubwa ambao utawanyima wananchi nafasi ya kutumikiwa na pande mbili ambazo zinategemeana.
3. Kwa matukio ya aina hii, tunadhani wakati mwafaka kwa uongozi wa Jeshi la Polisi nchini kuwajibika, kuazia kwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa na uongozi wa Makao Mkuu, akiwamo Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Saidi Mwema.
4. Tunasema hivi kwani kuna kila dalili kwamba polisi wanahusika kwa namna moja au nyingine na tukio au/na matukio yaliyosababisha kifo cha Mwangosi, kwani kitendo cha kumzingira tu na kumshambulia kinathibitisha kwamba hawakuwa na nia njema hata kidogo dhidi ya mwandishi huyu.
5. Taarifa ambazo TEF tunazo, pia zinadai kwamba kulikuwa na mpango wa polisi wa “kuwashughulikia waandishi wa habari watatu” (Mwangosi) akiwa mmojawapo na hilo lilionekana likitekelezwa kwa polisi kumshambulia mwandishi huyo, baadaye alipoteza maisha katika mazingira ya kutatanisha
6. Hili linatiliwa nguvu na tukio jingine la polisi kumpiga na kumjeruhi mwandishi mwingine, Godfrey Mushi ambaye ni mwakilishi wa gazeti la Nipashe mkoani Iringa. Mwandishi wa tatu ambaye hadi tunapoandika taarifa hiyo yumo katika mpango wa ‘kushughulikiwa na polisi’ ni Francis Godwin ambaye ni mwandishi wa habari wa kujitegemea.
7. Vitendo vya aina hii havivumiliki na havipaswi kuachwa kuendelea kwani ni hatari kwa ustawi wa demokrasia na uhuru wa habari nchini. Hatuwezi kuendelea katika mazingira ambayo polisi wanageuka kuwa chombo cha mauaji ya raia badala ya kuwa walinzi wa raia.
8. Kwa maana hiyo, mbali na uchunguzi ambao utafanywa na polisi, tunatoa wito kwa Serikali kuunda chombo huru, ambacho kitabaini ukweli, na matokeo yake yatangazwe kwa umma, huku wahusika wa aibu hiyo wakichukuliwa hatua za kisheria. Tunasema hivyo, tukifahamu kwamba tayari kuna jitihada za kuficha ukweli na kueneza propaganda za uongo kuhusu tukio zima.

9. Mwenendo wa aina hii wa chombo cha dola kuamua kutumia silaha kuua na baadaye kupanga mbinu chafu za kuficha ukweli ni hatari kwa Taifa, na unaiweka demokraisia ya nchi yetu njia panda, huku tukielekea katika hatari ya Taifa kutumbukia katika uovu.

IMETOLEWA NA:
NEVILLE MEENA,
KATIBU MKUU – JUKWAA LA WAHARIRI TANZANIA (TEF) SEPTEMBA 3, 2012

Dr Slaa Alipotua Kwenye Msiba Wa Daud Mwangosi Leo Jioni...Leo jioni tukiwa msibani ( Daud Mwangosi) mara akaingia Dr Wilbroad Slaa wa CHADEMA kuja kutoa pole kwa wafiwa. Kamera yangu haikuwa mbali!

Dr Slaa Akitoa Pole Kwa Wafiwa

Mjane Wa Marehemu Akifarajiwa

Daud Mwafongo ameacha mke na watoto wanne.


Inasikitisha; Mtoto wa marehemu Daud Mwangosi Akimkumbatia Kwa Uchungu Dr . Wilbroad Slaa Jioni Hii..

Daud ameacha mke na watoto wanne, wa mwisho ana miaka miwili tu. Anayeangalia kulia ni Mzee Arcado Ntagazwa.
Reactions::

Nyanya Za Msibani Hizi!


Leo alasiri nilifika nyumbani kwa marehemu Daud Mwangosi kutoa pole kwa familia yake, ndugu na jamaa. Inasikitisha sana.

Maandazi Ya Msibani Haya, We Acha Tu!Leo nimezungungukia jikoni kwenye msiba wa mwenzetu Daud Mwangosi, maeneo karibu na Mtwivila hapa Iringa.

Rais Wa Msumbiji Awasili Nchini Leo

Rais Jakaya Kikwete (kushoto) akisalimiana na mgeni wake Rais wa Msumbiji Armando Guebuza(kulia) wakati alipowasili jana jijini Dar es salaam katika Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere tayari kwa kuhudhuria mkutano wa dharura wa siku moja wa Kamati ya Ulinzi na Usalama (TROIKA) utakaofanyika tarehe 4.9.2012 mjini Dar es salaam. Mkutano huo wa siku moja utajadili mgogoro wa Jamhuri ya Kidemokarisia ya Congo(DRC
Rais wa Msumbiji Armando Guebuza  akisalimiana na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Davis Mwamunyange alipowasili jana jijini Dar es salaam  katika Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere tayari kwa kuhudhuria  mkutano wa dharura cha Kamati ya Ulinzi na Usalama (TROIKA) utakaofanyika  tarehe 4.9.2012 mjini Dar es salaam. Mkutano huo wa siku moja utajadili mgogoro wa Jamhuri ya Kidemokarisia ya Congo(DRC
Rais Jakaya Kikwete (kulia) akimwongoza mgeni wake Rais wa Msumbiji Armando Guebuza(kushoto)  kukagua gwaride la heshimiwa jana jijini Dar es salaam alipowasili kwa ajili ya mkutano wa dharura cha Kamati ya Ulinzi na Usalama (TROIKA) kitakachofanyika tarehe 4.9.2012 mjini Dar es salaam.
                                   PIcha na Tiganya Vincent-MAELEZO

No comments:

Post a Comment