Friday, September 28, 2012


HakiElimu Wazindua Matangazo Kuhamasisha Elimu Ya AwaliNa Joachim Mushi, Thehabari.com

 TAASISI ya HakiElimu imezindua matangazo mapya ya redio na televisheni ikiwa ni kampeni ya kuhamasisha jamii na Serikali juu ya umuhimu wa elimu ya awali kwa watoto kabla ya kujiunga na darasa la kwanza.

 Uzinduzi huo umefanyika leo jijini Dar es Salaam katika Ofisi za HakiElimu na kuhudhuriwa na baadhi ya walimu na wanafunzi wa awali, waandishi wa habari, wadau mbalimbali wa sekta ya elimu, pamoja na malezi na makuzi ya watoto. Akizungumza katika uzinduzi huo Mkurugenzi Mtendaji wa HakiElimu, Bi. Elizabeth Missokia alisema shirika hilo lemeamua kuzindua kampeni hiyo iliyopewa jina la “Boresha Elimu ya Chekechea” lengo kuu likiwa ni kuitaka Serikali itimize ahadi na wajibu wake wa kutoa elimu bora kwa wanafunzi wote wa elimu ya awali. 

Mkurugenzi huyo alisema elimu ya awali kwa mtoto ni muhimu sana katika kujenga msingi imara kielimu na endapo elimu hiyo itatolewa kikamilifu, inakuwa ni msingi imara kwa mtoto katika elimu yake ya baadae na pia elimu hiyo ni muhimu kwa maendeleo ya mtoto kimwili, kiakili na kimaadili. “Katika Sera ya Elimu na mafunzo ya mwaka 1995 Serikali inaonesha umuhimu wa elimu ya awali, inapotamka; ‘Tafiti kadhaa zilizofanyika nchini katika miaka ya 1980 zilibaini kuwa watoto waliopitia elimu ya awali huwa na mafanikio makubwa zaidi wanapoanza darasa la kwanza. 

Kutokana na kutambua umuhimu huu, Serikali iliamua kuingiza Elimu ya Awali kwa watoto wenye umri wa miaka 5 na 6 kwenye mfumo rasmi wa elimu na kila shule ya msingi inapaswa kuwa na madarasa ya Elimu ya Awali’,” alisema Missokia. Alisema kabla ya uzinduzi wa kampeni hii HakiElimu imefanya tafiti katika sehemu mbalimbali nchini na kubaini hali ya utoaji wa elimu ya awali na mazingira yake inatia huruma kwani elimu hiyo inavyotolewa katika mazingira yasiyofaa jambo ambalo linachangia kushuka kwa kiwango cha elimu nchini. “Kama ilivyo katika elimu ya msingi na ile ya sekondari, elimu ya awali imegubikwa na changamoto nyingi. Baadhi ya changamoto hizi ni upungufu mkubwa wa vyumba vya madarasa, unaosababisha mrundikano mkubwa katika madarasa, ukosefu mkubwa wa walimu wenye taaluma ya elimu ya awali pamoja na vifaa vya kufundishia. 


Aidha, kutokuwepo na tofauti ya kimadarasa katika elimu ya awali (yaani watoto wa umri wa miaka 5 na miaka 6 kusoma katika darasa moja), na wingi wa masomo pia ni changamoto,” alisema. Aidha aliongeza kuwa licha ya Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa, katika makadirio na matumizi ya wizara yake ya mwaka 2012/13, kukiri kuwa Serikali imetoa mwongozo kwa kila shule ya Msingi kuwa na darasa la Elimu ya Awali, lenye madawati yanayolingana na hali ya watoto wa elimu hiyo, kujenga vyoo kwa ajili ya watoto wa Elimu ya Awali wasiingiliane na wale wa shule za msingi, lakini bado kuna mapungufu makubwa katika utekelezaji wake. 

 "Baada ya kuona madhara ya kukosa elimu bora ya awali kwa watoto wetu, HakiElimu inatoa wito kwa watanzania wote nchini wenye mapenzi mema na maendeleo ya taifa letu kuungana nasi katika kampeni hii kwa njia zifuatazo; Kuhimiza wananchi wote wenye watoto wenye umri wa kuandikishwa shule za awali wafanye hivyo kwa wingi. Kuna baadhi ya sehemu inaripotiwa wazazi bado hawajaelewa umuhimu wa kuwapeleka watoto katika madarasa haya ya awali. "Kuwabana viongozi wetu tuliowachagua kuanzia mwenyekiti wa mtaa, diwani na Wabunge wetuwanachukua hatua kukabiliana na changamoto zilizopo ili kufanikisha Elimu bora ya Awali kwa watoto wetu. Wananchi kuandika barua kwenye magazeti mbalimbali hapa nchini zikielezea hali ya elimu ya awali inavyotolewa katika maeneo mliyopo.

" HakiElimu imeshauri barua zinazoandaliwa na wananchi kuzituma moja kwa moja kwa Wahariri wa magazeti wanayoyasoma kupitia anuani zilizopo katika gazeti husika, au wanaweza kuzituma kupitia sanduku la barua 79401 Dar es Salaam zikiwa na kichwa cha habari ‘BORESHA CHEKECHEA’, ambapo HakiElimu itafanya kazi ya kuzipeleka katika magazeti mbalimbali nchini. Aidha, ili kuchagiza mafanikio katika sekta ya elimu, HakiElimu imeandaa vipindi vya radio katika mikoa ya Morogoro, Mbeya, Tabora, Tanga, Kagera, Dodoma na Mara ambavyo vitatoa nafasi ya Marafiki wa Elimu kujadili jinsi gani elimu ya awali inaweza kuboreshwa. 

 Hata hivyo kwa Watanzania wanaotumia mtandao wa 'Internet' wanaweza kushiriki kampeni hii kwa kutembelea; www.facebook.com/hakielimu, www.twitter.com/hakielimu, www.hakielimu.blogspot.com na kuangalia matangazo mapya waweza kutembelea YouTube kupitia www.youtube.com/hakielimutz

  Habari hii imeandaliwa na mtandao wa www.thehabari.com
Reactions::

Taarifa TFF Kwa Vyombo Vya Habari

Release No. 157 TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI Septemba 28, 2012

 TFF YATOA ITC KWA WACHEZAJI WANNE Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limetoa Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC) kwa wachezaji wanne waliokuwa wakichezea timu mbalimbali nchini. Wachezaji hao ni Tony Ndolo aliyejiunga na KCC ya Uganda kutoka Toto Africans, Felix Amech Stanley aliyekwenda Bahla ya Oman kutoka Coastal Union, Ernest Boakye kutoka Yanga aliyejiunga na Tripoli Athletics Club ya Lebanon na Derrick Walulya aliyerejea URA ya Uganda kutoka Simba. 15 WACHUKUA FOMU UCHAGUZI TWFA Wanamichezo 15 wamechukua fomu kuwania nafasi mbalimbali za uongozi kwenye Chama cha Mpira wa Miguu wa Wanawake Tanzania (TWFA) utakaofanyika mwanzoni mwa mwezi ujao. Waliochukua fomu za kuwania uenyekiti ni Lina Kessy, Isabellah Kapera na Joan Minja.

 Nafasi ya Makamu Mwenyekiti imeombwa na Roseleen Kisiwa pekee wakati Katibu Mkuu ni Amina Karuma na Cecilia Makafu. Macky Mhango pia ni mwombaji pekee aliyeomba nafasi ya Katibu Msaidizi. Waombaji watatu wa nafasi ya mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ni Furaha Francis, Juliet Mndeme na Zena Chande. Nafasi ya Mhazini nayo ina mwombaji mmoja tu ambaye ni Rose Msamila. Sophia Charles, Rahim Maguza, Telephonia Temba na Jasmin Badar Soud wao wanaomba nafasi ya ujumbe wa Kamati ya Utendaji ya chama hicho kwenye uchaguzi huo ambao utaendeshwa na Kamati ya Uchaguzi ya TWFA chini ya Ombeni Zavalla. 

MKUTANO VODACOM, KLABU ZA LIGI KUU Klabu za Ligi Kuu na mdhamini wa ligi hiyo kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom zimekutana jana (Septemba 27 mwaka huu) jijini Dar es Salaam.

 Mazungumzo yalilenga kipengele ya upekee (exclusivity) kilichopo kwenye mkataba wa udhamini ambacho kitaendelea kuwepo. Klabu zilikuwa zimeomba kwa mdhamini kuangalia uwezekano wa kukiondoa. Pande hizo zimekubaliana kuunda kamati ya pamoja kwa ajili ya kuitafutia kila klabu mdhamini binafsi kwa lengo la kuhakikisha zinashiriki kikamilifu katika ligi hiyo. Klabu zote zimeshapata vifaa kutoka kwa Vodacom ukiondoa African Lyon ambayo ilitarajia kuchukua vifaa hivyo leo kutoka kwa mdhamini wa ligi hiyo. 

MCHAKATO WA UCHAGUZI WA VIONGOZI TAFCA Mchakato wa uchaguzi wa viongozi wa Chama cha Makocha wa Mpira wa Miguu Tanzania (TAFCA) unaanza rasmi Septemba 30 mwaka huu kwa uchukuaji fomu kwa wagombea. Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TAFCA, Ramadhan Mambosasa, fomu kwa waombaji uongozi zitaanza kutolewa Septemba 30 mwaka huu, na mwisho wa kuchukua na kurudisha fomu hizo ni Oktoba 4 mwaka huu. 

Fomu hizo zinapatikana ofisi za TAFCA zilizopo Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam kuanzia saa 3 asubuhi hadi saa 10 alasiri. Ada ya fomu kwa waombaji wa nafasi za Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti, Katibu Mkuu na Katibu Msaidizi ni sh. 200,000. Nafasi zilizobaki za Mhazini, mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na wajumbe wa Kamati ya Utendaji, ada ya fomu ni sh. 100,000. Uchaguzi wa TAFCA umepangwa kufanyika Novemba 10 mwaka huu. Boniface Wambura Ofisa Habari Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
Reactions::

Apendekeza Sanaa Na Utamaduni Vitambuliwe Kikatiba


NA MAGRETH KINABO – MAELEZO, BAGAMOYO 

 WASANII wamepewa changamoto ya kujitokeza kwa wingi katika kutoa maoni juu ya uundaji wa Katiba mpya ili fani yao iweze kutambulika kisheria. Kauli hiyo imetolewa jana na Mkurugenzi Idara ya Mfuko wa Uwezeshaji wa Baraza la Sanaa la Taifa(BASATA), Charles Malimba wakati akitoa mada kuhusu Sanaa ya Utamaduni na dhana ya Tasnia ya Ubunifu inavyoweza kuleta ajira kwa vijana wa Tanzania katika Tamasha la 31 la Sanaa na Utamaduni linaloendelea kwenye uwanja wa Taasisi ya Sanaa na Utamaduni(Tasuba), Bagamoyo, mkoani Pwani. 

Alisema kuna haja ya wasanii kujitokeza katika kutoa maoni juu ya Katiba mpya ili itambuena kutoa kipaumbele mambo mbalimbali katika sekta ya sanaa na utamaduni. 

Aidha Malimba aliongeza kuwa wakati umefika kuwa Katiba itamke sanaa na utamaduni kazi , pia kuwepo na viwango vya malipo kisheria kwa kuwa sekta hiyo inavyoweza kuchangia mapato kwa serikali. Malimba alitaka vyuo vinavyofundisha sanaa utamaduni nchini kutunza kumbukumbu za fani hizo na kuurithisha ili kuepusha kupotea kwa utamaduni wa Mtanzania , huku akiwataka wanafunzi wa fani hizo kusoma kwa bidii na kuitekeleza ili kuweza kuwasaidia wengine na kuifanya sekta hiyo kuwa ajira. 

Naye mhitimu wa chuo hicho wa mwaka 2010, Nyenyembe Jacoub na Baraka Matitu walisema ili kuweza kukuza sanaa na utamaduni kuna umuhimu wa kuanzisha shule maalum kuanzia chekechea hadi elimu ya juu. Akijibu hoja hiyo, Malimba alisema ni changamoto kwa wadau mbalimbali binafsi kuanzisha shule hizo kama ilivyo kwa zingine kwa kuwa suala hilo halina kipingamizi, huku akisisitiza suala la utunzaji wa sanaa na utamaduni ni wajibu wa kila wanajamii. 

Baadhi ya wasanii waliomba serikali iweke mikakati ya kuweza kuwasaidia wasanii hususan wale wachanga ili kuweza kukuza vipaji vyao, kwa kuwa vingi vinaanzishwa lakini vinashindwa kuendelea kwa kukosa wafadhili.

Taarifa Ya CHADEMA Kwa Vyombo Vya Habari


         TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

KAMATI za Utendaji za Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) katika Wilaya ya Nyamagana na Ilemela katika vikao tofauti kwa kushirikiana na kamati za madiwani katika kila wilaya husika, zimekamilisha mchakato wa kupata wagombea wa nafasi za umeya na naibu meya, Halmashauri ya Jiji la Mwanza na Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela. 

Kamati ya Utendaji ya Wilaya pamoja na madiwani wa CHADEMA Wilaya ya Nyamagana walimteua aliyekuwa Naibu Meya kabla, Diwani wa Kata ya Maina, Charles Chibara kuwa mgombea wa Umeya Halmashauri ya Jiji la Mwanza. Kwa upande wa Ilemela, kikao cha Kamati ya Utendaji pamoja na madiwani wa wilaya hiyo walimteua Diwani wa Kata ya Nyamanoro, Abubakar Kapera kuwa mgombea wa Umeya Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela. Kikao hicho cha Utendaji na madiwani wa CHADEMA Wilaya ya Ilemela, pia kilimteua Diwani wa Kirumba, Danny Kahungu kuwa mgombea wa nafasi ya Unaibu Meya Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela. 

 Vikao hivyo tofauti vya uchaguzi vilivyoketi kwa mujibu wa katiba, kanuni na taratibu za chama chini ya usimamizi wa Ofisi ya Katibu Mkuu wa CHADEMA, vilihusisha wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya Wilaya na madiwani katika eneo husika. Itakumbukwa kuwa katika kutafuta namna bora ya kusimamia vyema utendaji wa chama katika Halmashauri ya Jiji la Mwanza ambayo ilikuwa ni halmashauri pekee nchini iliyokuwa ikihusisha wilaya mbili, yaani Nyamagana na Ilemela, Baraza Kuu la CHADEMA liliamua kuwa masuala yote yanayohusu jiji hilo yasimamiwe na Ofisi ya Katibu Mkuu. Utekelezaji wa maamuzi hayo ya kikatiba, ulianza siku nyingi, ikiwemo kusimamia uchaguzi wa Meya wa Jiji la Mwanza mapema baada ya uchaguzi mkuu mwaka 2010. 

Wakati huo huo Kamati ya Utendaji ya Wilaya Nyamagana imekubali kumwachia kugombea nafasi ya Unaibu Meya wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Diwani wa Mirongo Daudi Mkama, katika uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika Septemba 28, 2012. Aidha, kutokana na vurugu zilizosababishwa na kundi la watu waliovamia na kuvuruga kikao cha uteuzi wa mgombea wa Umeya na Naibu Meya wa Manispaa ya Ilemela hivi karibuni, uongozi wa CHADEMA Wilaya umefungua kesi polisi kwa jalada lenye namba MZN/RB/8226/2012, kwa ajili ya hatua za kisheria.

 Imetolewa leo Septemba 27, 2012, Dar es Salaam; Tumaini Makene Ofisa Habari wa CHADEMA

.


No comments:

Post a Comment