Tuesday, September 18, 2012

Dk Magufuli aombwa kumulika malipo ya fidia Kyaka-Bugene




Mzee Theobard Kishenye akiondoka katika hali ya kukata tamaa katika ofisi za Wilaya ya Karagwe baada ya jina lake kukosekana kwa wanaotakiwa kupewa fidia
Mbunge wa viti maalumu CCM Bernadetha Mushashu akisikiliza malalamiko ya baadhi ya wananchi wa wilaya ya Karagwe ambao hawatapata fidia kupisha ujenzi wa barabara ya Kyaka-Bugene
BAADHI ya wakazi wa Wilaya ya Karagwe wamemuomba Waziri wa Ujenzi Pombe Magufuli kumulika zoezi la ulipaji wa fidia ya kupisha ujenzi wa barabara ya Kyaka Bugene kwa madai kuwa uthamini  wa mali ulifanyika kwa upendeleo.
Wananchi wa vijiji vya Kihanga na Kishao wametoa kilio hicho baada ya kubainika kuwa katika orodha ya watakaolipwa fidia  zipo nyumba zilizojengwa miaka ya karibuni huku zenye miaka zaidi ya hamsini zikiondolewa katika orodha ya kufidiwa.
 Mkazi wa kijiji cha Kishao Magreth Peter ambaye ni mama mjane alisema amejulishwa na Tanroads Mkoa wa Kagera kuwa nyumba yake itabomolewa bila fidia,wakati huo jirani zake ambao wako ndani ya mita 22.5 kama yeye wakiwa wameanza kulipwa.
Mwananchi mwingine wa kijiji hicho Adventina Furuka ambaye pia ni mjane alishangazwa na baadhi ya nyumba za kifahari zilizojengwa miaka ya karibuni katika ukanda ule ule  kuonekana katika orodha ya watakaolipwa huku wao majina yakikosekana.
“Nimeolewa hapa tangu mwaka 1950 naishi na watoto na wajukuu ,nimeambiwa nyumba yangu itabomolewa bila kulipwa fidia wazee wote wamezikwa hapa nyumbani na kuna makaburi saba”anabainisha mama huyo.
Pia waliwatuhumu walioendesha zoezi la utahamini baada ya kudaiwa kuwataka wale wenye nyumba zenye umri mkubwa kupeleka uthibitisho wa stakabadhi za kununua  mabati ya kuezekea ili waingizwe kwenye orodha ya watakaofidiwa.
Aidha mzee Theobard Kishenye alidai zoezi la uthamini lilijaa mazingira yenye utata kwani baadhi ya wananchi waliitwa kwa ajili ya majadiliano na walioendesha zoezi hilo.Alisema majirani zake walioko kwenye mita zile zile wameanza kupokea malipo na kuwa amejulishwa kuwa hatalipwa fidia.
Naye Mchungaji Japhet Runyoro alisema kuna utata mkubwa katika majina yaliyopitishwa kwa ajili ya fidia ikiwemo nyumba mpya za hivi karibuni na kutaka Waziri Magufuli kuingilia kati suala la malipo ya wananchi wanaotakiwa kupisha ujenzi wa barabara.
Naye ofisa wa Tanroads Mkoa wa Kagera Gasper Kyaruzi aliyekuwa akitoa malipo ya fidia juzi kwa baadhi ya wananchi  alikataa kutoa ufafanuzi kwa kundi kubwa la wananchi waliokuwa wakidai hawana imani na zoezi la uthamni lilivyoendeshwa.
Alisema kazi aliyokuwa ametumwa ni kulipa fedha kwa  wananchi wanaostahili fidia ambao pia majina yao yalikuwa yametundikwa katika mbao za matangazo katika Halmashauri ya Wilaya hiyo na kuwa mwenye malalamiko ayapeleke ofisi za Tanroad Mkoa.

No comments:

Post a Comment