Thursday, August 9, 2012

JK: Alivyomfunga Mdomo Membe Sakata La RadaKAULI iliyotolewa na Rais Jakaya Kikwete kwamba hakuna ushahidi wa kuwashtaki watuhumiwa rushwa ya rada, inaonekana kumfunga mdomo Waziri wake wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe ambaye aliwahi kuahidi kwamba angewataja watuhumiwa hao.

Rais Kikwete alipokutana na wakuu wa vyombo vya habari wiki iliyopita, alisema Serikali inashindwa kuwashtaki waliotuhumiwa katika suala hilo kutokana ukweli kwamba hata Uingereza walikana Kampuni ya BAE Systems kutoa rushwa na badala yake wakasema ilikosea katika kuandika hesabu zake.

Wakati Rais Kikwete akisema hakuna ushahidi wa kuwashtaki watuhumiwa wa rushwa ya rada, tayari Membe alikuwa amesema watuhumiwa wapo, anawajua na aliahidi kwamba angewataja bungeni.

Hata hivyo, Membe aliyewasilisha Hotuba ya Makadirio ya Matumizi ya wizara yake bungeni juzi, alishindwa kutekeleza ahadi yake licha ya kutakiwa kufanya hivyo na baadhi ya wabunge, wakiongozwa na Waziri Kivuli wa wizara hiyo, Ezekia Wenje ambaye pia ni Mbunge wa Nyamagana (Chadema).

Juzi, kabla Membe hajasoma hotuba yake, Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe alitoa taarifa rasmi ya Serikali bungeni kuhusu suala hilo na alisema kuwa, hakuna mtuhumiwa wa rada anayeweza kupelekwa mahakamani na kutamka kwamba mjadala kuhusu suala hilo umefungwa rasmi.

“Hata Uingereza iliyochunguza suala hilo imeeleza bayana kwamba hakuna rushwa na katika hatua hiyo, Serikali haiwezi kumfikisha mtu yeyote mahakamani,” alisema Chikawe.

Kauli hiyo ya Serikali inaonekana kuwakera baadhi ya wabunge ambao jana waliliambia gazeti hili kwamba wanashangazwa na jinsi Serikali ilivyomaliza na kufunga mjadala wa ufisadi wa rada, hali kukiwa na kila dalili kwamba wapo Watanzania waliohusika katika ufisadi huo.

Kauli za wabunge
Mbunge wa Wawi (CUF), Hamad Rashid Mohamed alisema: “Ushahidi wa kwanza ni fedha zilizorejeshwa kwa sababu Watanzania walilipa zaidi. Kama kuna fedha zililipwa zaidi, iweje asipatikane mtu wa kuchukuliwa hatua. Tulivyoelezwa ni kuwa vyombo vya uchunguzi vilikuwa vinachunguza suala hili, sasa tunashangaa kuelezwa kuwa hakuna uchunguzi unaoendelea.”
Alihoji kama fedha zaidi ya Sh70 bilioni zililipwa zaidi, kwa nini waliohusika na uzembe huo wasichukuliwe hatua?

Alisema kama fedha za nchi zimelipwa zaidi,
inawezekana kulikuwa na ufisadi au uzembe na hayo yote yanastahili kuchukuliwa hatua za kisheria.

Mbunge wa Nzega (CCM), Dk Hamis Kigwangala alisema kuwa, amefurahishwa na msimamo wa mawaziri katika suala hilo ingawa haamini kama ungekosekana ushahidi wa kumnasa aliyehusika.“Siamini kama ilishindikana kupata ushahidi, ninachokiona ni kwamba hakukuwa na juhu di za kuhakikisha unapatikana ushahidi na wahusika waliamua jambo hili liende kama lilivyo.

Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika alisema atamwandikia rasmi Spika kwa mujibu wa Kanuni ya 46 ili waziri atakiwe kujibu kwa ukweli na kuacha kutetea ukiukwaji wa sheria.

No comments:

Post a Comment