Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Jaji Mstaafu Joseph Warioba avitaka vyama vya siasa, asasi za kidini na wanaharakati kuacha kuwaelekeza wananchi aina ya maoni wanayopaswa kutoa kuhusu Katiba Mpya.
Jaji Warioba ameyasema hayo leo (Alhamisi, Agosti 9, 2012) katika mkutano wake na waandishi wa habari kuzungumzia tathmini ya mikutano ya awamu ya kwanza ya ukusanyaji wa maoni ya wananchi kuhusu Katiba Mpya katika mikoa minane ya Pwani, Dodoma, Manyara, Kagera, Shinyanga, Tanga, Kusini Unguja na Kusini Pemba.
“Sio wanasiasa tu, watu wote wakiwemo viongozi wa kidini, wanaharakati na taasisi zisizo za kiserikali ziache kuwalazimisha wananchi watoe maoni wanayotaka wao. Wananchi wawe huru kutoa maoni yao,” alisema na kuongeza kuwa vyama vya siasa, asasi zisizo za kiserikali ziatapata muda wa kuwasilisha maoni yao Tume.
“Mwananchi akitoa maoni yake binafsi, anakuwa ‘very articulate’ (anajieleza kwa ufasaha), lakini akielekezwa cha kusema, na ukamuomba ufafanuzi, anashindwa hata kueleza,” alisema Jaji Warioba katika mkutano huo uliohudhuriwa na pia na Katibu wa Tume hiyo, Bw. Assaa Rashid na Naibu Katibu Bw. Casmir Kyuki.
Kuhusu idadi ya mikutano iliyofanyika katika awamu ya kwanza, Mwenyekiti huyo amesema Tume yake imefanya mikutano 386 katika mikoa minane ya awamu ya kwanza kwa muda wa mwezi mmoja.
No comments:
Post a Comment