Na Mwandishi wetu
Muleba
MADEREVA wa magari na pikipiki wametakiwa kuzitambua na kuzifuata sheria za usalama barabarani ili kuweza kukabiliana na tatizo la ajali ambazo kwa hivi sasa zinaendelea kupotaza maisha ya watu ikiwemo kusababisha ululemavu wa viungo kwa watumiaji wa vyombo hivyo.
Mwenyekiti wa kamati ya usalama barabarani mkoani Kagera Winstoni Kabantega alisema hayo wakati alipokuwa akiendesha mafunzo ya awali ya udereva ambayo yanatolewa kwa watumishi wa Hospitari ya Rubya ambao ni Madaktari,manesi pamoja na mapadri ambao ni walimu wa sekondari ya Rubya wilayani Muleba.
Kabantega alisema kuwa hivi sasa ajali nyingi zinaongezaka kutokana na watumiaji wa barabara kutozifuata na kuzitambua sheria za usalama barabarani jambo ambalo linaleta tatizo kubwa kwa usalama wa raia na kusababisha vifo vingi.
Alisema kuwa kwa hivi sasa kuna mabadiliko makubwa ya sheria hizo kwani sheria za zamani nyingi zimefanyiwa marekebisho kwaio ni wajibu wa kila dereva kuzifuata na kuzitambua ili kuweza kupunguza tatizo la ajali ambazo zinaongezeka siku hadi siku.
Aliongeza kuwa watumiaji pamoja na kuzitambua sheria hizo inawabidi kutambua sheria kwa magari ya dharula jambo ambalo alilielezea kuwa madereva walio wengi hawazitambui sheria zinazohusu magari hayo.
"Ukiwa dereva inabidi utambue kuwa kuna magari ya dharula ambayo ukisha yaona wewe kama dereva inakubidi usimame magari hayo ni kama ya Wagonjwa,zimamoto,Jeshi la Polisi,jeshi la Wananchi pamoja na jeshi la magereza mengine ni magari ya kusindikiza fedha na madini kwaio inabidi unaposikia au kuyaona inakubidi usimame ili yapite"alisema Kabantega.
Akizungumza kwa niaba ya wanafunzi wanaopata mafunzo hayo mganga mkuu wa Hospitari ya Rubya Dk Diocles Ngaiza alisema kuwa ni muhimu kwa dereva kuzitambua sheria za barabarani na kujua jinsi ya kumuhudumia mgonjwa wakati inapotokea ajali kwa kumpatia huduma ya kwanza.
Alisema kuwa mara nyingi ajali zinapotokea watu hupoteza maisha kwasababu ya kukosa huduma ya kwanza na hii inatokana na watumiaji walio wengi kutozitambua huduma hizo kabla ya wagonjwa ambao ni majeruhi katika ajali za magari kupelekwa hospitarini.
Aidha aliwataka kufuata sheria na kuwafichua wale wote ambao wanavunja sheria za barabarani ambao wakibainika inaweza kupunguza athari ambazo kwa hivi sasa zinasababisha vifo na ulemavu wa viungo.
Mafunzo hayo yanatolewa na chuo cha Lake Zone Cha mjini Bukoba kwa kushirikiana na jeshi la polisi kupitia kikosi cha usalama barabarani mkoani Kagera ambayo ni ya muda mfupi yanatolewa kwa watu wapatao 60 yanatolewa kwa lengo la kufahamisha mabadiliko ya sheria za barabarani ambazo zimefanyiwa marekebisho.
Mwisho
No comments:
Post a Comment