Katibu wa umoja wa vijana CCM (UVCCM) mkoa wa Singida,Omary Hassan Mtuwa akitoa taarifa yake kwa waandishi wa habari (hawapo kwenye picha) ya kukanusha taarifa zilizotolewa na vyombo vya habari kuwa amekihama Chama Cha Mapinduzi na kujiunga na CHADEMA.Picha na Nathaniel Limu.
Katibu wa umoja wa vijana CCM (UVCCM) mkoa wa Singida, Omary Hassan Mtuwa, amekanusha vikali taarifa iliyotolewa na vyombo vya habari, kwamba amekihama chama chake na kujiunga na chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Mtuwa alisema taarifa hizo ni za uwongo uliopea, uzushi na zinalenga kumgombanisha yeye na chama chake pia na viongozi kwa ujumla.
Akifafanua, Mtuwa alisema taarifa hizo zimechapishwa na gazeti moja la kiswahili la kila siku (juni 18) mwaka huu ukurasa wa mbele ulibeba kichwa cha habari kuwa CHADEMA yavuna viongozi wa CCM.
Katibu huyo,alisema taarifa zilizoandikwa kwenye gazeti hilo zilizohusisha cheo cha Katibu wa vijana wa CCM mkoa wa Singida na kwamba anasoma chuo kikuu cha Ruaha, ni za uwongo mtupu.
Mtuwa alisema taarifa hiyo imemkosesha amani na imewasikitisha mno kwa vile, wahusika hawakumtendea haki kwa kumuuliza juu ya madai ya kuhamia CHADEMA. Mwandishi wa habari hiyo, ameandika taarifa hiyo bila kupata maoni kutoka kwake.
“Kama kweli CHADEMA wamevuna viongozi kutoka CCM,hilo mimi silijui na wala silitambui.Lakini kwa upande wangu, wameogopa na wamewapotosha Watanzania kwa kusema katibu wa UVCCM mkoa wa Singida,kahamia CHADEMA”,alisema na kuongeza;
“Mimi Omary Hassan Mtuwa,bado ni mwanachama hai wa CCM na ni mwaminifu wa kiwango cha juu.Nitaendelea kukitumikia chama changu kwa nguvu zote bila kutetereka hadi tone la mwisho”.
Alisema amefedheshwa na kuonewa sana na taarifa hiyo, iliyosheheni uwongo mwingi na kusababisha usumbufu mkubwa kwa mwajiri wake, familia yake na jamii kwa ujumla.
“Kwa hiyo, naomba gazeti hilo lifute,liniombe radhi na kutangaza hatua hiyo kupitia ukurasa wa mbele kama ambavyo limefanya katika kunichafua.Tofauti na hivyo,nitalazimika kwenda mahakamani kudai haki yangu”,alisema Mtuwa.
No comments:
Post a Comment