Thursday, June 14, 2012

Dk Mwakyembe Awasha Moto TRL

Mussa Juma, Dodoma

BAADA ya kusafiri kwa treni kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma, Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe amebaini hujuma nzito katika Shirika la Reli Tanzania (TRL) ikiwamo ofisa mmoja kuwaibia abiria kwa kughushi viwango vya nauli na ameagiza afukuzwe kazi.

Licha ya kuagiza kutimuliwa kwa ofisa huyo, pia alitangaza kuandaliwa utaratibu wa kufanya mabadiliko kadhaa katika kuboresha usafiri huo, ikiwamo kuondoa malipo ya nusu nauli kwa watoto wadogo kuanzia miaka mitatu hadi miaka 10 na pia kuondolewa kwa utaratibu wa malipo ya mizigo midogo ya abiria.

Juzi, Dk Mwakyembe ambaye tayari amewang’oa vigogo wanne wa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), aliamua kusafiri kwa treni hadi Dodoma akitokea Dar es Salaam ili kujionea utendaji kazi wa shirika hilo.

Mara baada ya kuwasili katika Stesheni ya Dodoma saa 1:30 asubuhi, Waziri Mwakyembe alizungumza na waandishi wa habari na kusema akiwa katika safari hiyo, amepata fursa za kutembelea mabehewa yote na kuzungumza na abiria.

Dk Mwayembe alisema ingawa safari ilikuwa nzuri, kuna mengi ambayo ameyabaini ambayo ni pamoja na abiria kulipa nauli kubwa na kuandikiwa tiketi tofauti jambo ambalo alisema ni wizi na kamwe wizara yake haiwezi kulifumbia macho.

“Unakuta nauli halali ni Sh9,000 lakini, abiria ameandikiwa Sh29,000. Sasa nimeagiza huyu anayehusika afuatiliwe na kujulikana na nipewe taarifa ameondolewa,” aliagiza Dk Mwakyembe.
Alisema pia katika safari hiyo, alibaini uchakavu mkubwa wa mabehewa na hakuna tofauti ya daraja la tatu na la kwanza, upungufu mwingine ni katika utendaji na taratibu jambo ambalo linapaswa kuchukuliwa hatua.

Dk Mwakyembe alisema si vyema mtoto kuanzia miaka mitatu kulipishwa nusu nauli, kwani taratibu zinapaswa kufanywa ili hadi mtoto wa miaka 10 ikiwezekana asilipishwe nauli kwani treni ndiyo usafiri wa umma.

Kuhusu mizigo, alisema kwa sasa mizigo ya abiria inalipiwa kwa kilo kama ilivyo usafiri wa ndege jambo ambalo si sawa kwani mzigo wa abiria kuanzia kilo 20 unalipishwa jambo ambalo linapaswa kuangaliwa.

“Usafiri huu mimi nasema ndiyo wa umma hivyo, tusizuie watu kupeleka hata zawadi nyumbani kwao ni vyema tuwe na utaratibu walau mizigo kidogo ya abiria isilipiwe,” alisema Dk Mwakyembe.
 

No comments:

Post a Comment