Wednesday, July 4, 2012

WABUNGE WATAKIWA KUACHA MZAHA WAKATI WAKICHANGIA HOJA BUNGENI

BAADHI ya watu maarufu nchini wamewataka wabunge kuacha mzaha katika kujadili mambo mazito yanayogusa maslahi ya nchi.
 Kauli ya wananchi hao imekuja siku chache baada ya kubaini kuwepo na ushabiki wa baadhi ya vyama ndani ya vikao vya bunge vinavyoendelea na kulisababishia kukosa hadhi ya bunge.
 Wakizungumza kwa nyakati tofauti na FULLSHANGWEBLOG jijini Dar es Salaam jana, watu hao walisema kuna ulazima kwa viongozi wa vyama vyote kutoa elimu kwa wabunge wao ili kuepuka vurugu zinazotokea bungeni hivi sasa.
 Miongoni mwa watu hao, ni Mhadhiri Msaidizi Chuo Kikuu cha Dar es Slaam Bashiru Alli alisema bunge hilo limetawaliwa na mzaha mwingi.
 Alisema mambo mengi yanayohitaji kupatiwa ufumbuzi kupitia mijadala hiyo yamekuwa hayajadiliwi kwa kiwango cha kina kitendo kinachosababisha wananchi kukosa majibu ya kuridhisha katika kero zao.
 Alli alisema kutokana na vitendo hivyo pengine kuna ulazima wa kupatikana mfumo mwingine wa utakao weza kuliendesha bunge kwa heshima na maslahi ya wananchi na si vinginevyo.
 Vile vile anasikitishwa na mahudhurio ya wabunge katika vikao hivyo muhimu vinavyojadili matatizo ya wananchi kwa madai kuwa wengine wako safarini.
Aidha, hapendezwi na vitendo vya Kamati za Bunge Kuendelea wakati huu muhimu wa kujadili bajeti kwani kikao hicho cha bunge kinauzito hivyo kila mbunge anapaswa kuwa bungeni.
Katibu Mkuu wa Chama cha (NCCR) Mageuzi, Sam Ruhuza alisema anashangazwa na mfumo wa bunge la sasa unavyoendelea kwa sababu haukidhi mahitaji ya wananchi badala yake unaangalia ushabiki wa chama.
 Aliongeza kuwa kutokana na wabunge hao, kushindwa kuzungumzia hoja au changamoto zilizopo katika majimbo yao na kuzitafutia ufumbuzi,kuna haja ya kupatiwa semina ya kuwakumbusha wajibu wao wakati wakiwa bungeni.
 Naye Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT)Usharika wa Matumbi, Christophile Kalata, alieleza kuwa watanzania walipofika sasa wanahitaji kiongozi shupavu anayeweza kusimamia rasilimali au maendeleo ya nchi kwa maslahi yao.
 “Nchi zilizoendelea zinapenda kuona au kushuhudia Tanzania ikikumbwa na misukosuko, hivyo zinaweza kutumia mwanya huo kwa kuwatumia viongozi waliopo kulumbana ili kazi za maendeleo ya nchi zisimame au zizorote” alisema Kalata.
 Naye Hashim Rungwe ambaye ni Mwanasheria aliwataka wabunge kutekeleza wajibu wao waliotumwa na wananchi kuliko kutaka kujijengea umaarufu usiokuwa namsigi.
Alisema wabunge hawako pale kwa lengo la kuonyeshana kuwa nani bingwa wa kusema japo anachosema hakina maslahi na nchi.

No comments:

Post a Comment