Tuesday, July 10, 2012

APCCC Yahamasisha Matumizi Ya Nishati Ya Jua

Na Mwandishi Wetu Bukoba
Bukoba


ASASI isiyo ya kiserikali inayojishughulisha na mabadiliko ya tabia nchi katika nchi za afrika APCCC imeanzisha kampeni ya kuhamasisha wananchi wa mkoa wa Kagera kuanza kutumia nishati mbadala ya jua kupikia badala ya kutegemea mkaa na kuni lengo likiwa ni kukabiliana na tatizo la mabadiliko ya tabia nchi ambalo linaendelea kuathiri dunia.

Mkurugenzi mtendaji wa asasi hiyo kwa  nchi za Afrika  Edward Munaaba alisema hayo jana wakati akitoa taarifa kwa balozi wa Uingereza hapa nchini Diane Corner aliyekuwa mkoani Kagera kwa ziara ya kutembelea miradi mbalimbali inayoendeshwa na APCCC.

Pamoja na balozi huyo kutembelea miradi mbalimbali na kujionea baadhi ya mafanikio na changamoto zinazokabili APCCC pia alifungua ofisi kuu ya asasi hiyo kwa mkoa wa Kagera iliyopo katika kata ya Kemondo wilaya ya Bukoba

 Munaaba alisema wananchi wamekuwa wakiharibu mazingira kutokana na shughuli mbalimbali za kibinadamu na kuongeza kuwa tayari wameanza kuhamasisha wananchi wa mkoani hapa juu ya matumizi ya majiko ya mionzi ya jua (solar cookers).

Alisema pamoja na matumizi ya majiko hayo kupunguza tatizo la ukataji miti pia itasaidia kuboresha afya za wananchi hasa maeneo ya vijijini na kuwakinga dhidi ya magonjwa mbalimbali yanayotokana na uvutaji wa moshi ikiwemo tatizo la macho mekundu, ambalo limekuwa likipelekea baadhi ya watu kuuawa.

“Asasi tayari inaendelea kutoa elimu juu jamii kutambua umuhimu wa kutumia nishati mbadala katika matumizi ya kila siku ambayo ni rafiki kwa utunzaji wa mazingira ambayo ni pamoja na matumizi ya solar cooker na gesi ya samadi” alisema  Munaaba.

Alifafanua kwamba tatizo la mabadiliko ya tabia nchi kwa mkoa wa Kagera limeathiri sekta nyingi zikiwemo kilimo, uvuvi na ufugaji ambazo zinategemewa na zaidi ya 80% hasa kutokana na kukosekana kwa mvua za uhakika na kipindi kirefu cha kiangazi.

Alisema kuwa katika kuhakikisha watu wanakabiliana na mabadiliko ya tabia nchi imepanga kuendelea kutoa mafunzo na semina kwa vikundi vya wanawake, vijana, makanisani na shuleni ili kufanya kila mwaannchi afahamu madhara ya mabadiliko ya tabia nchi

Aliongeza kuwa ni bora kila mwananchi nchini kutambua athari za mabadiliko ya tabia nchi na kuchukua hatua za kukabiliana na tatizo hilo kunusuru uchumi wa taifa na maisha ya wananchi na viumbe vingine.


  Kwa upande wake barozi wa Uingereza Nchini Diane Corner alipongeza juhudi zinazofanywa na APCCC katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia, huku akieleza kufurahishwa na hali ya hewa ya mkoa wa Kagera, ambapo ni mara yake ya kwanza balozi huyo kutembelea mkoa huo.

Mwisho

No comments:

Post a Comment