Saturday, July 7, 2012

MTAKATIFU THOM AELEZEA MIKAKATI YANGA, AANZA KAZI MARA MOJA

Thom Saintfiet akiongoza mazoezi ya Yanga, Uwanja wa Kaunda jioni hii. Picha zote na Mahmoud Zubeiry
Na Mahmoud Zubeiry
KOCHA mpya wa Yanga, Thom Saintfiet amesema kwamba sera yake ni ushindi na mataji na hahofii mpinzani yeyote katika soka ya Tanzania, ikiwemo watani wao wa jadi, Simba SC.
Akizungumza katika Mkutano na Waandishi wa Habari jioni ya leo, makao makuu ya klabu makutano ya Mitaa ya Twiga na Jangwani, Dar es Salaam, Saintfiet alisema kwamba yeye ni muumini wa ushindi na mataji, hivyo anachotaka ni ushindi tu.
 
“Nikishinda 5-0 ni vizuri, lakini hata nikishinda 1-0 si mbaya, mimi ni mshindi na ndio maana nimekuja hapa kushinda,”alisema.
Thom alisema kwamba akili yake hapo kwa Simba tu, bali wapinzani wote katika Ligi Kuu na akasema anataka kurejesha ubingwa wa Ligi Kuu, ambao msimu uliopita klabu hiyo ilipokonywa na watani wao hao wa jadi.
“Upinzani ni mkubwa, nasikitika mwaka jana timu imepoteza ubingwa wa Ligi Kuu, lakini si mbaya, si lazima timu bora kila mwaka iwe na taji. Hata Barcelona ni timu nzuri, lakini haikuchukua ubingwa wa Ligi ya Mabingwa wala La Liga.
Timu (Yanga) ilibeba nafasi ya tatu msimu uliopita, siyo nzuri sana. Nataka nishirikiane na wenzangu kurejesha heshima,”alisema.
Saintfiet alisema kwamba ameona wachezaji ni wazuri na anamuamini kocha anayemkuta Freddy Felix Minziro ni mzuri na amefanya kazi nzuri. “Timu ilicheza mechi na Express wiki iliyopita, nimeambiwa ilicheza soka nzuri na kushinda, naamini naikuta timu ikiwa vizuri,”alisema.
Mbelgiji huyo alisema kwamba ana wiki moja kabla ya kuanza kwa Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame na hana wasiwasi atafanya vizuri kwa sababu timu ina wachezaji wazuri na Minziro alianza kuwaandaa mapema.
Saintfiet alikataa kuzungumzia falsafa yake akisema hataki wapinzani wake wajue siri zake, ila akasistiza sera yake ni ushindi na kubeba mataji.
Tom Saintfiet alizaliwa Machi 29, mwaka 1973 mjini Mol, Ubelgiji na kabla ya kuwa kocha alicheza soka katika nafasi ya kiungo kuanzia mwaka 1983 hadi 1997 alipostaafu na kuwa kocha akiwa ana umri wa miaka 24, akiweka rekodi ya kocha kijana zaidi kuwahi kutokea katika soka ya Ubelgiji.
Saintfiet amefundisha nchi kadhaa kuanzia kwao Ubelgiji, Qatar, Ujerumani, Visiwa vya Faroe, Finland na Uholanzi.
Pia ana uzoefu wa kutosha wa kufundisha soka Afrika akiwa amefundisha Namibia na Zimbabwe kama kocha Mkuu wa timu za taifa za nchi hizo.
Anasema kabla hajakwenda Namibia, Saintfiet alikuwa kocha wa klabu ya Ligi Kuu Finland, iitwayo RoPS Rovaniemi na mwaka 2002, alikwenda kuifundisha B71 Visiwa vya Faroe ambayo aliiwezesha kushika nafasi ya pili katika Ligi Daraja la kwanza. Anasema kutoka hapo, akaenda kuwa kocha wa Al-Ittihad Sports Club ya Qatar (sasa inaitwa Al-Gharafa SC) ambako alidumu hadi mwaka 2004 alipochukuliwa kuwa kocha wa timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17 ya Qatar.
Saintfiet ana leseni Shirikisho la Soka Ulaya (UEFA) ya kufundisha soka ya kulipwa popote barani humo, ambayo aliipata mwaka 2000.
Kati ya mwaka 2006 na 2007 alikuwa Mkurugenzi wa Ufundi wa FC Emmen ya Daraja la Kwanza Uholanzi na pia amewahi kufanya kazi kama Mshauri wa Ufundi wa Shirikisho la Soka la Kazakhstan.
Amewahi  kuwa Mchambuzi wa soka katika Televisheni katika nchi za Ubelgiji, Afrika Kusini na Namibia na alifanya kazi kama mkalimani DFB. Amesomea Saikolojia ya Michezo na Uchumi.
Anazungumza lugha kibao na kwa ufasaha zaidi ni Kiholanzi, Kiingereza, Kifaransa, Kijerumani, Kifaroe na ‘ana jua jua’ Kiarabu, Kiafrikana na Kispanyola na sasa tayari ameanza kujifunza Kiswahili.
Baada ya kumaliza kusaini mkataba majira ya 9:47 jioni, Saintfiet aliyewasili jana mchana nchini, aliteremka Uwanja wa Kaunda kuanza kufundisha timu. Kwanza alianza kuzungumza na wachezaji kuwaelezea falsafa zake na kisha akaanza kazi.












No comments:

Post a Comment