Friday, April 12, 2013

Waganga Wa Tiba asilia Watakiwa Kutowalaza Wagonjwa Majumbani Mwao


Bukoba.
 
WAGANGA na wakunga wa tiba asilia katika wilaya ya Bukoba mkoani Kagera wametakiwa kutolaza wagonjwa wanaowahudumia majumbani mwao, ili kuepuka kupata kesi za mauaji pindi mtu atakapokufa kwa bahati mbaya wakati akipatiwa huduma.
 
Kauli hiyo ilitolewa juzi katika uwanja wa Uhuru na mkuu wa wilaya ya Bukoba,  Bi Zipporah Pangani wakati akiwakabidhi vyeti vya serikali waganga 13 ambavyo vinawaruhusu kufanya kazi ya kutoa tiba kwa jamii kisheria.
 
Bi  Pangani alisema kuwa waganga wa tiba asilia na wakunga wanaofanya hivyo wanakiuka sheria na taratibu za nchi, na kuwa kama kuna mganga anataka kutoa huduma hiyo lazima ajenge kituo chenye hadhi hiyo ambacho pia lazima kipate kibali kutoka serikalini cha kulaza wagonjwa.
 
Aidha aliwataka waganga hao kuwashauri wananchi kupata vipimo sahihi vya kitaalam kuhusu magonjwa yanayowasumbua ili kumwezesha mganga kutoa tiba ya ugonjwa anaoufahamu badala ya kutibu kwa kubahatisha.
 
“Mtu anaweza kuwa anaumwa typhoid (homa ya matumbo) unamg’ang’ania wakati ungeweza kushirikiana na daktari wa hospitali akapata vipimo sahihi na hatimaye mkashirikiana kumtibu maana wote nia yenu ni moja ya kutoa tiba kwa wananchi” alisema Bi Pangani.
 
Alisema kuwa vyeti walivyopatiwa ni vya muda na kuwa baada ya hapo mganga ambaye atafanya kazi bila kusababisha matatizo katika utendaji wake ndiye atapewa cheti cha kudumu na wizara yenye dhamana.
 
Akizungumza katika mkutano huo mfupi wa kukabidhiwa vyeti hivyo, mwenyekiti wa chama cha waganga na wakunga wa tiba asilia (STAMATA) katika manispaa ya Bukoba,  Bw. Habibu Mahyoro alisema watu wanaoishi kwa kutegemea viungo vya binadamu sio waganga bali ni matapeli na ni wachawi.
 
Bw. Mahyoro aliiomba serikali kuwawezesha kupata vitendea kazi ikiwamo vyombo vya usafiri ambavyo vitatumika kutoa elimu kwa jamii kwa lengo la kupunguza matukio ya wanaojihusisha na matendo maovu ikiwamo mauaji ya albino na vikongwe.
 
Kwa mujibu wa mwenyekiti huyo STAMATA mkoa wa Kagera ilianzishwa mwaka 2011 ikiwa na wanachama 47, ambapo sasa ina wanachama 89 kutoka katika wilaya za Missenyi, Bukoba na Karagwe  na wanachama 13 miongoni mwao ndio wamepatiwa vyeti.
 
Mwisho.

No comments:

Post a Comment