Edward Moringe Sokoine (1938 - 1984)
Ni miaka ishirini na tisa iliyopita. Siku ya Alhamisi, majira ya jioni kama saa kumi na moja. Anga la jiji la Dar es Salaam lilikuwa jeusi likihanikizwa na mawingu madogo madogo yaliyojikusanya kuashiria kamvua kalikokuwa kametawala siku hiyo. Hizi ni nyakati za masika katika sehemu kubwa ya nchi.Ndo kwanza nimerudi toka shule, tayari nimeshajipakia ugali wangu wa njano (Yanga) na maharage ya Iringa.
Nipo mtaani nikicheza na wenzangu chandimu. Hatuna viatu, tupo pekupeku lakini hatujali kitu. Maisha yalikuwa mazuri bila kujua adha na masumbufu ambayo wazazi walikuwa wanayapitia ili kutufanya watoto wao tuweze kwenda chooni.Nikiangalia pembeni, akina mama walikuwa wamekaa wakisukana na wengine walikuwa kwenye vibustani vyao wakipalilia matuta ya viazi vitamu. Hakika hatukujua lililokuwa limetokea masaa machache yaliyopita hapa nchini kwetu.Lakini ghafla redio zikaanza kupiga wimbo wa taifa.
Si
aghalabu kusikia wimbo wa taifa mida kama ile tena kipindi kile
kisichokuwa na sikukuu wala mgeni yeyote wa kitaifa. Haiyumkiniki kuna
jambo kuu limetkea. Katika utoto wangu, ghafla nikaacha kucheza, akina
mama waliokuwa wakisogoa nao wakapigwa na ubaridi wa ghafla. Katika
mshawasha wangu wa kitoto nikaijongelea redio kutaka kujua kilichojiri
jioni hiyo ya Alhamisi nyeusi.
Dakika
kadhaa zilipita kabla ya wimbo wa taifa kuisha.Sauti iliyojaa huzuni
ikasikika. Hata katika utoto wangu, naweza kusema kwa hakika kuwa sauti
ile ilikuwa katika huzuni na majonzi na ilionesha ni ya mtu aliyekuwa
katika kilio muda si mrefu uliopita. Naam, ilikuwa ni sauti ya hayati
baba wa Taifa. Nayakumbuka maneno yake mpaka sasa. Hivi ndivyo
alivyosema:"Ndugu wananchi, leo mnamo majira ya saba mchana, ndugu yetu,
mwenzetu, Waziri Mkuu na Makamu wa Pili wa Rais, Edward Moringe Sokoine
amefariki dunia katika ajali ya gari iliyotokea huko Morogoro wakati
akilejea Dar es Salaam kutoka Dodoma kwenye mkutano wa Bunge"Naam, hiyo
ndiyo sababu ya kupigwa kwa wimbo wa Taifa jioni ile. Utando mweusi
ukatanda.
Simanzi
ikatawala. Vilio vikasikika, furaha ikatoweka. Giza la mawingu meusi
likaongezea upotevu wa furaha. Nikausikia ukelele mkuu kutoka kwa mama
mmoja aliyekuwa ameshika jembe akipalilia bustani yake "Mama wee
mkombozi wetu amekufa, nani atatutetea sisi wanyonge?" Hakika ndivyo
aliomboleza mama yule.Huzuni kuu ikaniingia ghafla. Nikajiwazia "Sokoine
kafa? Hapana, amekufa?" Nafsi ilikataa kuamini, akili ya utoto
ikaniambia haiwezekani. Ghafla machozi yakaanza kunitiririka. Naam
nililia. Nilimlilia mzalendo wa kweli. Wazazi walilia, wananchi walilia,
hata Nyerere alilia tena hadharani, hakulia kiunafiki alilia
kweli.Watanzania wapenda haki tulilia, tulimlilia mpenda haki mwenzetu.
Sokoine
mzalendo wa kweli. Mwana wa Kitanzania asilia, mtetezi wa kweli wa
wanyonge, mchapakazi, mpigania mema ya nchi.Naam, yawezekana kwa wengine
ameshafutika lakini kwa wapenda haki, Sokoine atabaki kuwa kioo chetu
daima. Huyu ndiye mtu aliyekuwa na sifa nilizozitaja wakati ule kwenye
ile ndoto yangu ya "Namuona mtu huyu". Yawezekana alikuwa na kasoro zake
kama mwanadamu na hata kiutendaji lakini daima nia yake njema kwa watu
wake iliyafunika makosa yake hayo. Alipendwa na wanyonge na kuchukiwa na
wezi, wabadhiifu wa mali ya umma na wahujumu uchumi (leo tunawaita
mafisadi). Huyu ndiye aina ya mtu tuliyemuhitaji Tanzania ya leo.
Nimemkumbuka
Sokoine, mtanzania mzalendo mwana mpenda nchi aliyenifanya nihisi msiba
wake kuwa unanihusu kwa ukaribu mno. Naam, wajamaa kama kina Subi
lazima watamkumbuka mtu huyu na kumuomboleza daima.Mungu alipenda
kumchukua ingawa tuliona amemchukua mapema mno.Pumzika kwa aman
No comments:
Post a Comment