Huu ndio mzimu unaoimaliza CCM
HAKIKA kwa muda mrefu Chama Cha Mapinduzi(CCM), kimekuwa kikijaribu kujiweka katika mazingira mazuri zaidi kisiasa. Hata hivyo licha ya kufanikiwa kwa kiwango fulani lakini bado kuna maeneo ambayo yamekuwa kikwazo cha CCM kushindwa kutimiza lengo lake. Ni wazi mzimu ambao unaimaliza CCM hivi sasa ni
hili la baadhi ya watendaji wa Serikali kwa ngazi mbalimbali kuonekana kikwazo cha utekelezwaji wa Ilani ya chama hicho ambayo inataka maisha bora kwa wananchi wake.
Utafunwaji wa fedha za umma umekuwa mkubwa katika nchi hii hali inayofanya katika halmashauri mbalimbali Tanzania kujikuta ikishindwa kufanikisha maendeleo.Kisa kuna kundi la watu ambalo lipo ndani ya Serikali kwa ajili ya kukwamisha juhudi za CCM katika kufikisha maendeleo kwa watu.
Moja ya malalamiko ya Wana-CCM katika maeneo mbalimbali ya nchini ni hili la ubadhirifu wa fedha ambazo zinatolewa na Serikal Kuu na kwenda kwenye halmashauri kwa ajili ya kufanikisha utekelezaji wa Ilani ya CCM ambayo ndio imeunda Serikali.
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi(CCM), Abdulrahaman kuanzia Aprili 14 hadi Aprili 21(Jumapili) , alikuwa akifanya ziara katika Mkoa wa Morogororo ambapo amezunguka katika wilaya zote za mkoa huo.
Moja ya kero kubwa aliyokutana nayo ni hii ya fedha za umma kuliwa na baadhi ya wajanja wachache ambao hawaitakii mema CCM kwa kuwa chanzo cha kukwamisha maendeleo.
Kinana anaonesha wazi kutofurahishwa na hali hiyo ambayo inafanywa na watendaji wasiokuwa waamini ambao wao wanachojua ni kufanya ubadhirifu wa fedha za umma ambapo katika hilo anatoa agizo kwa viongozi wa CCM kuwa makini nao na kufuatilia karibu.
Kwa lugha harisi Kinana anataka Wana-CCM kwa ngazi mbalimbali kuibana Serikali pale ambapo watendaji wao wanaonekana kufanya mambo kinyume na Ilani ya uchaguzi inayozungumzia maendeleo ya watu.
Akiwa katika wilaya ya Mvomero wakati wa ziara yake,Kinana anakutana na malalamiko makubwa ya wana-CCM wakiwamo madiwani wa Halmashauri ya wilaya hiyo ambao wamechoshwa na ubadhirifu wa fedha uliofanywa na moja ya watendaji wa halmashauri.
Wanachama hao wanakwenda mbali zaidi na kuamua kumueleza Kinana kuwa kwa hali iliyofikia na namna ambavyo mtendaji huyo analindwa licha ya kula fedha za umma huenda analindwa na watu waliowaita ‘Wakubwa’.
Kutokana na hali hiyo Kinana anaamua kutoa agizo la kuhakikisha wabadhirifu wa fedha za umma wakiwemo waliohusika kutafuna fedha za Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero zaidi ya sh.bilioni moja wanachukuliwa hatua.
“Hatutakubali kuona baadhi ya watendaji wanashindwa kutekeleza majukumu yao.Kazi yao imebaki kukwamisha utekelezaji wa ilani ya chama changu.
Hatuwezi kukaa kimya, tutaibana Serikali na pale ambapo tutaona ufumbuzi wake unahitaji mjadala wa kina tutakwenda kuzungumza haya kwenye Kamati Kuu ya CCM ili kupata ufumbuzi wake,”anasema.
Mbali ya Kinana kutofurahishwa na watendaji wa Serikali ambao wanakwamisha maendeleo ya wananchi kwa kula fedha, anatumia nafasi hiyo kuwageukia viongozi wa CCM ambao nao wanashindwa kusimamia majukumu yao.
Anasema katika maeneo ambayo amepita katika ziara yake yapo mambo mengi yanayolalamikiwa lakini la viongozi wa CCM kutowajibika ipasavyo nalo ni tatizo lingine kwa chama na lazima hatua madhubuti zichukuliwe kurudisha heshima ya chama .
Kwa mazingira hayo ili CCM kupambana na mzimu huo unaokwamisha kasi ya maendeleo ni wakati muafaka kwa Wana-CCM kutofumbia macho madhambi yanayofanywa na baadhi ya watendaji wa Serikali.
Ni jambo baya sana wakati CCM inataka kutatua kero za wananchi lakini kuna kundi ambalo lipo kwa ajili ya kukwamisha kasi hiyo ya kimaendeleo.Inasikitisha na kama Mtanzania nina haki ya kutoa maoni yangu kwa mustakabali wa taifa langu.
No comments:
Post a Comment