Monday, April 15, 2013

WADAU WA USAFIRISHAJI WAITAKA SERIKALI KUWAPATIA VIBALI VYA UOKOAJI

 
Kufuatia ajali mbili za kusikitisha zilizotokea hivi karibuni ikiwemo ajali ya watu wawili kubanwa na magari ya mizigo kwa muda wa masaa 16 katika eneo la maseyu, morogoro bila kupata msaada mpaka kupelekea vifo vyao na ile ya kuanguka kwa jengo la ghorofa na kusababisha vifo vya watu zaidi ya 30, baadhi ya wawekezaji katika sekta ya usafirishaji wakiwa na mabango wamejitokeza na kuelezea uwezo wao wa kuweza kushiriki katika kazi za uokoaji kwa kutumia vifaa walivyo navyo lakini urasimu wa upatikanaji vibali uliowekwa na serikali umekuwa ni kikwazo kikubwa kwao.
Wakizungumza kwa uchungu wasafirishaji hao akiwemo mkurugenzi mtendaji wa usangu logistics bwana Ibrahim Ismail wamesema kuwa pamoja na kuwa na magari maalumu yenye uwezo wa kuokoa kwa haraka maisha ya watu na mali zao, magari hayo yamekuwa hayatumiki majanga kama hayo yanapotokea kutokana na urasimu wa upatikanaji vibali kutoka mamlaka ya barabara tanroads na kuiomba serikali kuangalia suala hilo kiundani ili kuyaachia magari hayo yafanye kazi bila vikwazo kwa kuwa ajali huweza kutokea muda wowote.
Aidha wawekezaji hao wameongeza kuwa ajali za magari makubwa kuanguka zimekuwa zikitokea mara kwa mara hususani katika barabara kuu na mara nyingine kusababisha kukatika kwa mawasiliano ambapo wamekuwa wakishindwa kutoa msaada kutokana na usumbufu wanao upata katika upatikanaji wa vibali ambapo kutokana na tatizo hilo wanalazimika kuhamishia magari hayo nchi za jirani ili yaweze kufanya kazi yaliyokusudiwa.

No comments:

Post a Comment