Tuesday, October 9, 2012

Ripoti Ya Mwangosi Yazua Mazito


Na: Boniface Meena na Fredy Azzah, MWANANCHI 

KAMATI iliyoundwa na Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk Emmanuel Nchimbi kuchunguza kifo cha mwandishi wa habari wa Kituo cha Channel Ten, Daud Mwangosi imeweka hadharani ripoti yake inayoeleza madudu yaliyofanywa na pande zote; polisi na Chadema na kusababisha mauaji hayo. Wakati hayo yakibainika katika ripoti ya Kamati ya Waziri Nchimbi, Baraza la Habari Tanzania (MCT) nalo limeanika ripoti yake kuhusu kifo hicho.

 Ripoti hiyo inaonyesha kuwa mauaji hayo, yalitokana na uhasama uliopo baina ya polisi mkoani Iringa na waandishi wa habari wa mkoa huo. Kamati hizo ziliundwa kwa nyakati tofauti kutokana na vurugu zilizotokea Septemba 2, mwaka huu katika Kijiji cha Nyololo, Wilaya ya Mufindi wakati polisi walipokuwa wakiwatawanya wafuasi wa Chadema waliokuwa wakifungua tawi la chama hicho katika kijiji hicho.

 Wajumbe katika kamati ya Nchimbi ni Mwenyekiti Jaji Steven Ihema, Makamu Mwenyekiti, Theophil Makunga na Ofisa wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Pili Mtambalike. Wengine ni Ofisa aliyesomea masuala ya milipuko kutoka Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), Kanali Wema W. Wapo pamoja na Naibu Kamishna wa Jeshi la Polisi, Isaya Ngulu. 

Kamati ya MCT ilikuwa ikiongozwa na John Mirenyi kutoka MCT, Hawra Shamte kutoka Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Tumaini Iringa, Simon Berege. Ripoti ya Nchimbi Pamoja na mambo mengine ripoti hiyo imesema nguvu iliyotumika na polisi kuwatawanya wafuasi wa Chadema siku ya tukio, ni kubwa na bomu lililomuua Mwangosi, lilipigwa kutoka umbali mdogo badala ya mita 80 zinazotakiwa kitaalamu, tena bila kumwelekezea mtu. Imesema utaratibu wa matumizi ya bomu hilo unaelekeza kulenga juu usawa wa nyuzi 45 na umbali wa mita 80 mpaka mita 100. "Hakukuwa na umuhimu wa kutumia bomu hilo kwa sababu hata ingekuwa kwa sababu ya kuwakamata watu, tayari askari polisi wapatao sita walikuwapo eneo la tukio walitosha kwani operesheni haikuwa kubwa," imesema ripoti hiyo iliyokuwa ikisomwa na Jaji Ihema. 

 Jaji Ihema alisema kamati imependekeza nafasi za wakuu wa wilaya na mikoa ziangaliwe upya kwa kuwa zinatumika kisiasa. Hata hiyo, Jaji Ihema alisema kinachozungumzwa kuhusu ripoti hiyo ni muhtasari tu wa ripoti nzima na wamefanya hivyo kuepuka kugusa mambo mengine ambayo yataingilia mwenendo wa kesi iliyopo mahakamani. Hata hivyo, akaeleza kuwa ripoti nzima inayoelezea kitu kilichotokea anaijua Dk Nchimbi ambaye ndiye aliyeunda kamati hiyo. 

 Jaji Ihema alieleza kuwa kamati yake ilipewa hadidu sita za rejea ambazo ni kuangalia kama mkusanyiko wa Chadema ulikuwa halali na kama kulikuwa hakuna uvunjifu wa amani. “Pia kuangalia kama nguvu iliyotumiwa na polisi ilikuwa sawa, mazingira yaliyosababisha polisi kutumia nguvu na kusababisha mauaji ya Mwangosi, kama kuna uhasama kati ya polisi na waandishi Iringa,” alisema Jaji Ihema na kuongeza; “Kuangalia kanuni na taratibu za polisi kuzuia mikutano ya siasa na uhusiano wa Jeshi la Polisi na vyama vya siasa.” 

Chadema nao walikuwa tatizo Jaji Ihema alisema Chadema ndiyo chanzo cha vurugu na uvunjifu wa amani kijijini Nyololo hasa kutokana na uamuzi wa kung’ang’ania kukusanyika isivyo halali eneo hilo. "Ikizingatiwa kuwepo kwa ujumbe wa SMS kutoka kwa Katibu Mkuu wa chama hicho Dk Willibrod Slaa uliosema, “IGP nasubiri simu yako. Wajulishe Polisi wako waandae risasi za kutosha, mabomu ya kutosha. Mtakuwa na karamu ya mauaji na kisha kusherehekea, mjiandae kwa kwenda mahakama ya Hague. Ni afadhali tufe kuliko manyanyaso haya,” alisema Jaji Ihema na kuendelea. 

 “Ujumbe huu ukiashiria umwagaji wa damu ni ushaidi tosha kuwepo kwa uvunjifu wa amani.” Polisi tatizo Alisema kuhusu nguvu iliyotumika na polisi, kamati imebaini kuwa ilikuwa ni kubwa kutokana na maelezo ya viongozi wa kijijini hapo. “Mwangosi aliuawa wakati amri ya askari kuondoka kwenye eneo la tukio ilishatolewa,” alisema Jaji Ihema na kuongeza;. "Kamati imebaini kuwa ushirikiano wa polisi na waandishi wa habari mkoani Iringa si mzuri hivyo ikapendekeza uangaliwe." 

Pia uhusiano kati ya polisi na baadhi ya vyama vya siasa hauridhishi, hivyo ni muhimu kukawa na jukwaa la kushughilikia hali hiyo, alisema Jaji Ihema. Mapendekezo Alisema kamati imeshauri kuwa sheria zinazotoa mamlaka za kuchunguza matukio ya vifo kwenye mkusanyiko ziangaliwe kwa kuwa lililotokea Nyololo lina ushahidi wa kutosha.

 Jaji Ihema alisema kwa kuwa Jeshi la Polisi litabaki kuwa mlinzi wa wananchi, siasa za ubabe na uhasama ziachwe. Aliendelea kusema kuwa kamati inapendekeza utulivu uendelee kuwepo ili kuweza kuondoa purukushani na pia viongozi waelimishwe juu ya umuhimu wa kutii sheria. “Kuwepo na programu mahususi ya uzalendo na kukuza maadili, elimu ya uraia iimarishwe na mafunzo ya JKT yarudishwe mapema,” alisema. 

 Mapendekezo mengine ni kuboresha ofisi ya msajili wa vyama vya siasa kwa kuanzisha ofisi wilayani na mikoani kwa kuwa imelemewa “Kwa upande wa vyama vya siasa viongozi wajifunze kuwa wavumilivu na kutii sheria,” alisema Jaji Ihema. Polisi ambao walihusika katika kumpiga marehemu Daud Mwangosi kabla. Ripoti ya MCT Ripoti ya Timu Maalumu iliyoundwa na MCT na TEF, kuchunguza tukio hilo imesema mauaji hayo yalifanywa makusudi chini ya usimamizi wa Kamanda wa Polisi wa Iringa, Michael Kamuhanda. 

“Matokeo ya uchunguzi ya mazingira yaliyopelekea mauaji ya Daudi Mwangosi, awali ya yote umethibitisha polisi kwa makusudi kabisa waliwashughulikia waandishi wa habari wa Iringa wakati wakikusanya habari za shughuli za Chadema katika Kijiji cha Nyololo,” inasema na kuongeza: “Pia Daudi Mwangosi aliuawa mikononi mwa polisi chini ya usimamizi wa moja kwa moja wa RPC Michael Kamuhanda. Matokeo haya yanathibitishwa na maelezo pamoja na ushahidi uliokusanywa kwa kutumia picha za video na ushahidi mwingine muhimu wa taarifa za vyombo vya habari.” 

Katibu wa MCT, Kajubi Mukajanga aliyesoma ripoti hiyo alisema kuwa utafiti huo ulibaini kuwa taarifa za mauaji wa Mwangosi zimekuwa zikikinzana kuanzia hatua za awali jitihada za kuficha ukweli zilipojidhihirisha. Ikifafanua juu ya uhusiano mbaya kati ya viongozi wa Serikali ya Mkoa huo na Jeshi la Polisi dhidi ya waandishi, ilisema baadhi ya waandishi waliwahi kupigwa na kuharibiwa vyombo vyao vya kazi. “Novemba 2011, mwandishi Laurent Mkumbata anayefanya kazi ITV, alipigwa vibaya na kamera yake ilivunjwa kwa makusudi na aliyekuwa Mkuu wa Polisi (OCD) wa Iringa Mohamed Semunyu wakati akiwa kazini,” ilisema: “Waandishi wa habari wa Iringa pia, walitendewa vibaya na viongozi wa mkoa wakati wa ziara ya Makamu wa Rais mwishoni mwa Februari 2011. 

Waandishi katika ziara hiyo walilazimika kulala kwenye basi walilosafiria kutokana na viongozi kupuuza kuwapatia hoteli ya kulala.” Kwa mujibu wa Mukajanga, Machi sita mwaka huu, polisi mkoani Iringa waliwapa Klabu ya Waandishi wa Habari Iringa (IPC), kibali cha kufanya maandamano ya amani kulalamikia kukua kwa uhusiano usio mzuri kati ya waandishi wa habari na viongozi wa mkoa. Mukajanga alisema tukio hilo waliwalenga zaidi waandishi wa Iringa ambao walikuwa wanawafahamu zaidi na kuwaacha wale waliotoka Dar es Salaam. 

Kabla ya kusomwa kwa ripoti hiyo, Mukajanga alitahadharisha juu ya tabia aliyosema imeibuka ya watu kufungwa midomo kwa kisingizio cha kuwa kesi ipo mahakamani. Alisema kwamba, ana imani kuwa mahakimu na majaji nchini, ni watu wenye sifa ambao wanaweza kufanya shughuli zao kwa kuzingatia ushahidi unaotolewa mahakamani bila ya kuathiriwa na maneno ya mitaani.

No comments:

Post a Comment