UGONJWA unaoshambulia migomba wa mnyauko bacteria umeanza kuathiri
upatikanaji wa ndizi kwenye maeneo mbalimbali yaliyoko mkoani Kagera.
Ugonjwa
huo unasambaa kwa kasi hasa kwenye maeneo ya wilaya za Muleba na
Karagwe ambayo uzalisha ndizi nyingi mkoani Kagera na maeneo mengine ya
wilaya za Bukoba na Misenyi.
Hali ya ugonjwa huo unaoshambulia
migomba wa mnyauko bacteria imechangbia kupunguza uzalishaji wa ndizi
mkoani Kagera jambo ambalo limechangia kupanda kwa bei ya ndizi
zinapopelekwa kwenye masoko.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili
umebaini kwamba kwenye soko kuu la Bukoba ndizi kubwa inauzwa kwa
wastani wa kati shilingi 15,000 hadi 20,000 ambapo miaka iliyopita ndizi
kubwa zilikuwa zinauzwa kwa wastani wa kati ya shilingi 6,000 hadi
8,000.
Kupanda kwa bei ya ndizi iliyochangiwa na ugonjwa
wa mnyauko bacteria wa migomba kumewalazimisha baadhi ya wakazi wa mkoa
wa Kagera ambao hutegemea ndizi kama chakula chao kikuu kubadilika
ambapo sasa wanalazimika kula ugali na wali.
Baadhi ya wakazi wa
mkoa wa Kagera wamelazimika kubadili fikira zao za kudhani kuwa ndizi
ndicho chakula kikuu baada ya kushindwa kumudu gharama za kununua ndizi
kwenye masoko ambazo bei yake ni kubwa.
Baadhi ya wakulima bora
wa migomba mkoani Kagera ambao mashamba yao yameathirika kutokana na
ugonjwa wa mnyauko bacteria wa mogomba ni pamoja kamishina mstaafu wa
jeshi la polisi Alfred Tibaigana.
Kamishina Tibaigana shamba lake
liko katika kijiji cha Buganguzi wilayani Muleba limeathirika sana,
Mkulima huyu kabla ya ugonjwa huu alikuwa na uwezo wa kuzalisha wastani
tani 40 za ndizi kwa wiki ambapo sasa anazalisha wastani wa tani
zisizozidi 10 kwa wiki.
Aidha, baadhi ya wakulima mkoani Kagera wameitahadharisha serikali kuchukua hatua za haraka za
kuthibiti ugonjwa huu unaosambaa kwa kasi ili zao la ndizi mkoani Kagera lisibaki kwenye vitabu vya historia.
No comments:
Post a Comment