RAIS KIKWETE AKUTANA NA UJUMBE KUTOKA KENYA LEO IKULU DAR ES SALAAM
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete
ametaka wananchi wa Kenya wapewe nafasi ya kuamua ni viongozi gani
wanawataka katika Uchaguzi Mkuu uliopangwa kufanyika Machi mwakani.
Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa
wananchi wa Kenya wanayo haki ya msingi kabisa kuamua hatma ya taifa lao
katika Uchaguzi Mkuu huo.
Mheshimiwa Rais aliyasema hayo leo
Oktoba 21, 2012 alipokutana na kufanya mazungumzo na ujumbe wa wabunge
wa vyama mbalimbali vya siasa vya nchini Kenya uliomtembelea Ikulu
jijini Dar es salaam.
Ujumbe huo uliongozwa na Naibu
Waziri Mkuu wa Kenya na Waziri wa Fedha Mhe. Uhuru Kenyatta ambaye pia
ni Mwenyekiti wa chama cha TNA na Waziri wa Sheria wa Kenya Mhe Eugene
Wamalwa wa chama cha New Ford Kenya. Wote wawili ni wagombea wa nafasi
ya Urais katika uchaguzi ujao.
Wengine katika msafara huo
walikuwa ni Naibu Waziri wa Afya na mbunge wa Mombasa Mhe. Kambi
Kazungu, Mbunge wa kuteuliwa wa chama cha TNA Bi Rachel Shebesh, na
Mbunge wa Kajiado kwa tiketi ya TNA Moses ole Sakuda na mbunge wa zamani
Mhe Abdullahi Alli.
Rais Kikwete aliwapongeza kwa
kuamua kufanya kazi kwa pamoja licha ya kuwa watakuwa washindani katika
kinyang’anyiro cha uchaguzi mkuu huo.
Mheshimiwa Rais ameitakia heri
nchi ya Kenya katika uchaguzi huo ujao, na kusisitiza kwamba nchi hiyo
ya jirani ina umuhimu katika mustakabali wa kiuchumi kwa nchi za Afrika
Mashariki.
Rais Kikwete wakati huo akiwa
Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU) alikuwa miongoni mwa viongozi
walioshughulika sana kutafuta ufumbuzi wa ghasia na vurugu zilizozuka
kufuatia Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2007 nchini Kenya.
Rais Kikwete alikaa siku tatu
nchini Kenya akitafuta usuluhishi wa vurugu hiyo ya kisiasa nchini humo,
ambayo katika mazungumzo yake leo ameyataja kama ajali iliyolipata
Taifa la Kenya, na ambayo majirani wake hawaitarajii kutokea katika
uchaguzi ujao.
Imetolewa na:
KURUGENZI YA MAWASILIANO YA RAIS
DAR ES SALAAM,
No comments:
Post a Comment