Tuesday, May 21, 2013

Taarifa ya CCM Juu Ya Mkutano Wa Wabunge Dodoma

6 debf4
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimewaonya na kuwapiga marufuku, makada na wanachama wake wenye nia ya kuwania nafasi mbalimbali katika uchaguzi mkuu ujao, kutothubutu kuanza kujipitipitisha kwa wapiga kura na kusema atakayefanya hivyo asimlaumu mtu kwa kitakachoamuliwa dhidi yake.

Kimesema sheria kanuni na taratibu zinazokiongoza Chama katika kupata wagombea wake ziko palepale na kwamba hakitamvumilia yeyote atakayebainika kuzikiuka.
Onyo hilo lilitolewa jana Dar es Salaam na Katibu wa Halmashauri Kuu ya 
Taifa (NEC) ya CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, wakati akiongea na waandishi wa habari kuhususu mkutano kati ya CCM na wabunge wake uliofanyika mwishoni mwa wiki mjini Dodoma.
"Viko vyombo vya habari ambavyo kwa makusudi vimepotosha ukweli kuhusu tulichoafikiana katika kikao kati ya CCM na wabunge wake. Si Mwenyekiti wa taifa wala Chama kilichoruhusu wenye nia ya kuwania nafasi mbalimbali kujipitishapitisha kwa wananchi.
"Nasisitiza nukuu hiyo ya baadhi ya vyombo vya habari si sahihi na ni ya kupotosha ukweli. Inaelekea kuna kikundi cha watu wenye mgombea wao wa kuchonga ambaye bila shaka anapungukiwa sifa, hivyo wanajaribu kumuongezea sifa kwa kumlisha Mwenyekiti maneno na kuwapa baadhi ya waandishi wa habari. Uhuni huo haukubaliki," alisema Nape.
Kwa mujibu wa Nape, licha ya ajenda kuhusu wana-CCM wenye nia ya kuwania nafasi mbalimbali ikiwemo udiwani, ubunge na urais kujadiliwa kwa kina katika kikao hicho, hitimisho na majumuisho ya Mwenyekiti wa CCM 
Taifa ilikuwa ni kukemea kwa nguvu zote pirikapirika hizo ambazo ni uvunjifu wa makusudi wa kanuni za Chama.Alisema kimsingi pirikapirika zinazofanywa na baadhi ya makada zinaweza kukigawa Chama na kuvuruga mshikamano na umoja uliopo ndani ya CCM.
Nape alisema CCM ina kanuni na taratibu zinazoisimamia na kuiongoza katika kufanya shughuli zake mbalimbali zikiwemo za mchakato wa kuwapata wagombea wake katika ngazi mbalimbali kuanzia shina hadi taifa. Kanuni hizo ni pamoja na za uteuzi wa wagombea wa Chama kuingia kwenye vyombo vya dola toleo la Februari, mwaka 2010 na kanuni za uchaguzi wa CCM, toleo la mwaka 2012.
“Ni mwiko kwa kiongozi au mwanachama yeyote wa CCM kuunda vikundi visivyo rasmi ndani ya chama, au kushiriki katika kampeni za uchaguzi za chini chini kinyume na ratiba ya uchaguzi na taratibu rasmi zilizowekwa” alisema.Katibu huyo alisema iwapo mwanachama yeyote atakiuka kwa makusudi na kuvunja taratibu hizo, Chama kitamwajibisha bila ya kumuonea haya na kwamba itakapofikia hapo asilaumiwe yeyote kwa kuwa npyo taratibu zinavyoagiza.
Akizungumzia malengo ya kikao hicho, alisema kililenga kutathimini utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM majimboni na kuangalia namna bora ya kuweka msukumo mpya na mkubwa zaidi kwa sehemu iliyobaki ya utekelezaji wake katika kipindi cha mwaka 2010/2015, ili kuhakikisha ahadi za Chama na wagombea wake zinatekelezwa kwa kiwango kikubwa.
Baadhi ya magazeti (Uhuru halimo) katika matoleo yao ya juzi, yalimnukuu Mwenyekiti wa Taifa wa CCM, Rais Jakaya Kikwete, akiwaruhusu wanaotaka kuwania urais katika uchaguzi mkuu ujao mwaka 2015 kuendelea na mchakato.
Magazeti hayo yalidai kuwa Rais aliruhusu hilo kutendeka huku 
akiwatahadharisha watakaokuwa tayari kufanya hivyo kuendesha kampeni zao kwa ustaarabu bila kuibua chuki na kujenga makundi kwa kuwa ni hatari kwa uhai wa Chama.

No comments:

Post a Comment