KAULI YA SERIKALI VURUGU ZA MTWARA
Na Lydia Churi.
SERIKALI YAAPA KUWASAKA WAASISI WA VURUGU MTWARA
Serikali imelaani vikali vurugu zilizotokea Mtwara na imeapa kuwasaka waasisi wa vurugu hizo ndani na nje ya Mtwara.
Serikali imelaani vikali vurugu zilizotokea Mtwara na imeapa kuwasaka waasisi wa vurugu hizo ndani na nje ya Mtwara.
Akitoa kauli ya Serikali Bungeni kuhusu vurugu zilizotokea Mtwara jana, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Dkt. Emmanuel Nchimbi ameliambia Bunge kuwa wote waliohusika kupanga, kushawishi, kuandaa na kutekeleza vurugu hizo hawataukwepa mkono wa sheria.
Katika kauli hiyo ya Serikali Waziri Nchimbi amesisitiza kuwa watanzania wanalo Taifa moja ambalo maliasili zake ni za watanzania wote hivyo tabia iliyoanza kujengeka ya kila eneo kutaka inufaike peke yake na mali za eneo husika italigawa taifa vipande vipande.
Alisema baadhi ya taasisi za kiraia na vyama vya siasa kwa maslahi binafsi yasiyo na upeo mpana, vinaweza kudhani kuwa kuunga mkono madai ya namna hii ni kujiimarisha na kukubalika kwao kwa jamii lakini badala yake wataipasua nchi na kusababisha vifo vya maelfu ya watu pamoja na kulijaza taifa vilema na majeruhi.
"Wasaliti wa taifa hili wanafahamu maendeleo makubwa yatakayopatikana Mtwara na nchi nzima kutokana na rasilimali gesi, hivyo wanatumia vibaya ufahamu wetu mdogo kuhusu gesi na kuchochea upinzani dhidi ya mradi huu unaotarajiwa kuwakomboa watanzania" Alisema Waziri.
Alisema vita inayofahamika kama vita kuu ya Afrika katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo iliyopiganwa kati ya 1998-2003 msingi wake ulikuwa ni kupigia rasilimali, vita hii ilisababisha vifo vya watu milioni 5.4, magonjwa na njaa na kuhoji kuwa huko ndiko tunakotaka kulipeleka taifa letu.
Alisisitiza watanzania wanatakiwa kujua kuwa wanayo dhamana ya kuendeleza umoja amani na kuchangia maendeleo ya nchi na tofauti zinazojitokeza lazima ziendelee kuzungumzwa kwa uwazi, kuheshimiana na kuzingatia sheria na taratibu za nchi yetu.
Alisema raia mmoja, Karim Shaibu alifariki katika vurugu hizo na wakati huohuo askari wanne wa Jeshi la wananchi wa Tanzania walifariki baada gari lao waliokuwa wakisafiria kutoka Nachingwea kwenda Mtwara kupata ajali katika eneo la Kilimani Hewa. Askari wengine 20 walijeruhiwa katika ajali hiyo.
Waziri Nchimbi aliyataja madhara mengine yaliyotokana na vurugu hizo kuwa ni kuchomwa moto kwa Ofisi za Mahakama ya Mwanzo ya Mitengo, Ofisi ya CCM kata ya Chikongola, nyumba binafsi ya Mwandishi wa Habari wa TBC na ya Afisa Mtendaji kata ya Magomeni. Aidha katika vurugu hizo, nyumba za askari polisi wanne pamoja ofisi ya kata ya Chilongola zilivunjwa na kuibiwa vitu mbalimbali.
Jana majira ya saa 4 asubuhi kulitokea vurugu kubwa katika Manispaa ya Mtwara na viunga vyake zilizosababishwa na madai ya baadhi ya wananchi wa Mtwara kupinga usafirishwaji wa rasilimali gesi kutoka Mtwara kwenda Dar es salaam. Makundi ya vijana waliokuwa maeneo ya Sokoni, Magomeni na Mkanaredi walipanga mawe makubwa, magogo na kuchoma moto matairi barabarani hali iliyoendelea kusambaa maeneo mengine.
No comments:
Post a Comment