Tuesday, May 21, 2013

Gari la polisi lanaswa na bangi

kamandamwema 4e060
Gari aina ya Toyota Landcruiser linalotumiwa na Mkuu wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), Mkoa wa Arusha, lilikamatwa juzi mjini Moshi likiwa limesheheni magunia 18 ya bangi.
Habari za awali zilieleza kuwa gari hilo lilikamatwa juzi saa 4:00 usiku katika Mji mdogo wa Himo, Moshi Vijijini likisafirisha bangi hiyo kwenda Tarakea, Rombo.

Polisi wawili akiwamo dereva wa gari hilo wanashikiliwa katika Kituo cha Polisi cha Himo na gari lipo Makao Makuu ya FFU, Moshi.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz alithibitisha kukamatwa kwa askari hao: "Mchakato wa kuwafikisha mahakama ya kijeshi unaandaliwa. Bangi hiyo ilikuwa inapelekwa kwa mfanyabiashara mmoja huko Rombo na ndiye aliyewakodi."
Hata hivyo, Kamanda Boaz alisema atatoa taarifa zaidi leo kwani uchunguzi bado unaendelea.
Bangi ilivyonaswa
Habari zimeeleza kuwa polisi waliokuwa doria waliliona gari hilo likitengenezwa na waliamua kuwauliza wenzao kulikoni? Wakajibiwa kuwa kuna kitu walikuwa wakirekebisha na lilikuwa ni tatizo dogo tu.
"Walipoulizwa kwani mnaelekea wapi wakasema wanapeleka mzigo wa bosi huko Tarakea mpakani na kwa taratibu zetu za kijeshi huwezi kuuliza ni bosi gani," kilidokeza chanzo kimoja ndani ya polisi.
Hata hivyo, polisi hao wa doria walirudi katika gari yao ili waendelee na doria lakini baadhi ya polisi wakamweleza ofisa aliyekuwapo katika gari hilo kwamba wanashuku gari lile limebeba bangi.
"Lilikuwa na harufu kali ya bangi na hilo ndilo lililowafanya wale polisi kurudi tena kwa wenzao na kuwaambia wanataka waone wamebeba nini ndipo wakakutana na magunia 18 ya bangi," kilieleza chanzo chetu.
Inadaiwa kuwa baada ya kukuta bangi hiyo, polisi hao waliwasiliana na Mkuu wa Upelelezi (RCO), Mkoa wa Kilimanjaro, Ramadhan Ng'anzi ambaye naye alimjulisha Kamanda Boaz.
Ilielezwa kuwa Kamanda Boaz aliagiza kuwekwa mahabusu kwa polisi hao katika Kituo cha Himo na gari hilo lipelekwe FFU, Moshi.

No comments:

Post a Comment