Hayo aliyasema jana alipokuwa akizungumza na
wakazi wa Kata ya Migoli, Tarafa ya Isimani wakati wa kuweka jiwe la
msingi kwenye Barabara ya Iringa - Dodoma ambapo alisema matukio ya hivi
karibuni yanahatarisha amani ya nchi.
“Ndugu zangu kabla sijafikia tamati ningependa
nizungumzie hili, nawaomba mdumishe amani na upendo. Taifa hili limedumu
katika amani kwa muda mrefu, matukio ya hivi karibuni
hayafurahishi…Wapo watu wanalala usiku na mchana wanapanga njama za
kuvuruga amani ya nchi yetu, watu hawa wasipewe nafasi, wasisikilizwe
kwani hawana nia njema na taifa letu,” alisema Kikwete.
Kikwete alisema Watanzania wakikataa kuwasikiliza,
kuwafuata na kutenda wanavyotaka Tanzania itabaki kuwa nchi ya amani na
mipango yao haitafanikiwa.
Kauli ya Kikwete imekuja huku kukiwa na matukio ya
vurugu za kidini na matukio ya maandamano ya uharibifu wa mali
yanayofanywa na baadhi ya makundi ya kidini nchini.
Akizungumzia uzinduzi wa ujenzi wa barabara hiyo
ambao ni sehemu ya Barabara Kuu ya Kaskazini inayounganisha
Iringa-Dodoma kwa kiwango cha lami, Kikwete alisema barabara ni ufunguo
wa uchumi katika taifa lolote duniani.
“Wapo watu wanaohoji ni kwa nini tunatumia fedha
nyingi kuwekeza kwenye ujenzi wa barabara, tungeweza kutumia fedha
nyingi kwenye maeneo mengine, lakini pamoja na kwamba tumechelewa
kuwekeza kwenye barabara bado kama nchi tuna nafasi ya kuunganisha nchi
kwa barabara na kasi ya uchumi itakua,” alisema Kikwete.
Kikwete alifafanua kuwa kwa sasa Serikali yake
imeweka kipaumbele katika ujenzi wa barabara na kuongeza kuwa ndiyo
sababu barabara nyingi zinazounganisha miji mikubwa na zile za kawaida
zimejengwa na nyingine zinaendelea kujengwa kwa kasi.
Alisema kutokana na hatua hiyo Serikali yake
imeimarisha mfuko wa barabara ambapo wakati anaingia madarakani ulikuwa
na kiasi cha Sh55 bilioni, lakini kwa kipindi cha miaka saba imefikia
Sh430 bilioni na sasa mfuko huo unatarajiwa kutengewa Sh504 bilioni
katika bajeti ya mwaka 2013/14.
Kikwete aliwataka wakazi wa Iringa na maeneo yote
zinakojengwa barabara kushiriki, kuzitunza kwa kulinda miundombinu yake
na kushukuru nchi wahisani kwa ujenzi wa miundombinu nchini.
Kuhusu umuhimu wa matumizi ya barabara alisema
zitasaidia wakazi wa maeneo jirani kukuza uchumi na kuwataka kutumia
fursa hiyo kufanya kazi za uzalishaji kwa bidiii ili waweze kunufaika na
matunda ya barabara hizo.
Kwa upande wake Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli
alisema Serikali itahakikisha makandarasi wote wanaoendelea na ujenzi
wa barabara nchini wanakamilisha kazi zao kwa wakati na wanajenga kwa
kiwango kinachotakiwa.
No comments:
Post a Comment