YANGA yatoa sare na KCC CCM KIRUMBA
Mabingwa wa soka Tanzania Bara, Yanga (HM)
MABINGWA wa
soka Tanzania bara, vijana wa mitaa ya Twiga na Jangwani, Klabu ya
Yanga ya Dar es salaam wameshindwa kutamba mbele ya KCC ya Uganda baada
ya kulazimisha sare ya kufungana bao 1-1 katika mchezo wa kwanza wa
kirafiki wa ziara ya klabu hiyo kanda ya ziwa ambao umepigwa katika
dimba la chama cha Mapinduzi CCM Kirumba.
Yanga walikuwa wa kwanza kuandika bao
kimiani katika dakika 40 ya kipindi cha kwanza kupitia kwa nyota wao
mpya Khamis Thabit, na KCC walisawazisha dakika za lala salama baada ya
mchezaji Kivuma Winy kutumia vyema makosa ya mabeki wa Yanga.Yanga wameshaanza ziara ya kuwaonesha kombe lao mashabiki wao wa kanda ya ziwa na kucheza mechi za kirafiki za kujipima uwezo kabla ya kuanza kutetea ubingwa wao wa ligi kuu walioutwaa msimu uliopita na kuwapokonya wanamsimbazi Simba SC.
Baada ya mchezo kumalizika, kocha msaidizi wa Yanga, Fred Ferlix Minziro amesema timu yao imejitahidi sana kucheza ikizingatiwa kuwa wamefanya mazoezi ya siku tatu tu.
“Kwanza tunamshukuru Mungu kucheza mechi hii ya kwanza, kikosi kimeonesha uwezo mkubwa ingawa kimefanya mazoezi ya siku tatu. KCC wametoka kushiriki kombe la Kagame kule Sudan na ndio maana wamecheza kwa uzuri”. Alisema Minziro.
Minziro aliongeza kuwa wachezaji wa Yanga wameonesha kiwango kizuri ingawa bado wanahitaji mazoezi zaidi kabla ya kuanza mitange ya ligi kuu soka Tanzania bara.
Baada ya mchezo wa leo, kesho siku ya sabasaba katika uwanja wa Kambarage mkoani Shinyanga, Yanga na KCC watarudiana tena na kuwapa nafasi mashabiki wa mkoa huo kukiona kikosi chao.
Na julai 11 watashuka katika dimba la Ally Hassan Mwinyi mjini Tabora dhidi ya maafande wa Rhino Rangers ambao wamepanda kucheza ligi kuu soka Tanzania bara msimu ujao.
Wanandinga wa Yanga leo hii walikuwa ni Kipa Deogratius Munishi ‘Dida’, Juma Abdul, Oscar Joshua, Rajab Zahir, Mbuyu Twite, Salum Telela, Nizar Khalfan/Said BahanuzI, HamisI Thabit/Bakari Masoud (Yanga B), Jerry Tegete, Didier Kavumbangu/Sospeter Mhina (Yanga B) na Abdallah Mguli (Yanga B). Chanzo: Baraka Mpenja
No comments:
Post a Comment