MAJAMBAZI wapatao 10 waliokuwa na silaha za kivita aina ya SMG 6
na LMG 2 wameteka magari mbalimbali yakiwamo mabasi mawili ya abiria na
kupora bunduki ya Jeshi la Polisi aina ya SMG katika pori la Hifadhi ya
Biharamulo mkoani Kagera.
Akiongea na waandishi wa habari ofisini kwake, Kamanda wa Polisi wa
Mkoa wa Kagera, Philip Kalangi, alisema tukio hilo limetokea jana majira
ya saa 2:30 asubuhi katika Kijiji cha Kasindaga, eneo lijulikanalo
kama Mlima wa Simba kwenye pori la Hifadhi ya Biharamulo.
Majambazi hao licha ya kupora bidhaa mbalimbali za abiria, walimpiga
risasi na kumjeruhi vibaya shingoni abiria mmoja aliyefahamika kwa jina
la Frederick Rugahiula (47) mkazi wa Bukoba, mkoani Kagera.
Kamanda Kalangi alitaja mabasi ya abiria yaliyotekwa kuwa ni RS, lenye
namba za usajili T 495 AGT, lililokuwa likitokea Bukoba kuelekea jijini
Dar es Salaam na NBS T 644 BUR, lililokuwa likitokea Bukoba kuelekea
Arusha.
Alisema baada ya kuteka mabasi hayo majambazi hao wanaoshukiwa kuwa ni
raia wa nchi moja jirani kutokana na lafudhi ya maneno waliyokuwa
wakiongea, waliwashusha abiria na kuwapora simu za mikononi pamoja na
fedha taslimu. Pia walipora bunduki ya Jeshi la Polisi aina ya SMG yenye
namba 14302551 iliyokuwa mikononi mwa polisi.
Alisema wakati wakiwa katika harakati za kuwapora abiria, askari
polisi waliokuwa katika basi la Mohammed Trans lililokuwa nyuma ya
mabasi hayo, waligundua kuwa wenzao wametekwa, ndipo walipoanza
kuwashambulia majambazi hao na kuzuka majibizano makali ya risasi.
Kamanda huyo aliongeza kuwa askari polisi wapatao wanne waliokuwa
wakisindikiza mabasi hayo walizidiwa nguvu kutokana na uchache wao,
hivyo wakaamuru kugeuza basi hilo na kukimbia kwa ajili ya kutafuta
msaada zaidi.
Akielezea tukio hilo lilivyotokea, Kamanda Kalangi alisema, kwanza
majambazi hayo yaliteka gari dogo na kuzuia njia kana kwamba
limeharibika, hivyo mabasi yalipofika yalilazimika kusimama na ndipo
yalipotekwa.
Hadi sasa hakuna mtu aliyekamatwa kuhusiana na tukio hilo na kuwa
msako mkali unaendelea kwa kushirikiana na askari wa wanyamapori katika
eneo la Hifadhi ya Burigi na pori la Biharamulo.
Aliongeza kuwa Jeshi la Polisi linahitaji ushirikiano wa pamoja katika
kukabiliana na matukio ya uhalifu, kwa kuzingatia kuwa watendaji wake
ni wachache na maeneo ni makubwa.
Hata hivyo alisema kuwa Mkoa wa Kagera unaathirika zaidi na wageni
wanaotoka nchi jirani zilizokuwa katika vita, wanaoingiza silaha ambazo
zinatumiwa na majambazi kwenye matukio ya uhalifu.
|
No comments:
Post a Comment