Monday, December 16, 2013


Taabini ya Rais Jakaya Kikwete kwa Nelson Mandela kijijini Qunu wakati wa mazishi ya Tata Madiba

JK_a472d.jpg
JUMAPILI 15 DISEMBA 2013
Mheshimiwa Jacob Zuma wa Jamhuri ya Afrika Kusini;
Mama Graca Machel,
Mama Winnie Mandela,
Wanafamilia waliondokewa na mpendwa wao,
Mtukufu Mwanamfalme Charles,
Waheshimiwa Wakuu wa Nchi na Serikali,
Waheshimiwa Mawaziri,
Wajumbe wa Mashirika ya Kidiplomasia na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa,
Waombolezaji wenzangu,
Mabibi na Mabwana;
Ninawaleteeni salamu za undugu na mshikamano kutoka kwa kaka zenu na dada zenu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Wameniomba niwafikishieni salamu za dhati za rambirambi kwako Rais, Mama Graca Machel, Mama Winnie Mandela, familia nzima ya Madiba na watu wote wa Afrika Kusini kutokana na kifo cha Mheshimiwa Nelson Rolihlahla Mandela, Rais wa zamani wa Afrika Kusini na African National Congress.
Wanapenda mfahamu kuwa hampo peke yenu. Wapo pamoja nanyi katika kipindi hiki kigumu na chenye majonzi. Wanasema huzuni yenu ni huzuni yetu, kuondokewa kwenu ni kuondokewa kwetu. Nelson Mandela alikuwa kiongozi wetu, shujaa wetu na baba yetu kama alivyokuwa kwenu. Watu wa Tanzania wamempoteza rafiki mkubwa na komredi mkubwa katika mapambano.
Rais Mandela amekuwa na uhusiano thabiti wa muda mrefu na Tanzania. Umeanza zamani wakati wa uhuru na mapambano ya ukombozi hapa Afrika Kusini na Tanzania. Vyama vyetu, African National Congress (ANC) na Tanganyika African National Union (TANU) vilikuwa na uhusiano maalum. Haikutokea tu, kuwa, baada ya ANC kuamua kuanzisha kitengo cha jeshi, Umkotho we Sizwe, baada ya njia za amani kushindikana, Dar es Salaam ikawa kituo cha kwanza cha Madiba baada ya kuondoka Afrika Kusini mwaka 1962 akiwa njiani kutafuta msaada kwa ajili ya mapambano ya kijeshi na mahali pa mafunzo kwa ajili ya wapiganaji wa MK.
Makomredi na marafiki;
Kimsingi, ziara yake ilihanikiza mafanikio. Ni ziara hiyo iliyochangia kubadili mwelekeo wa historia ya hili taifa kubwa iliyofanikiwa kuuangusha ubaguzi wa rangi na kuzaliwa kwa Afrika Kusini mpya mwaka 1994. Ingawa Rais wetu wa kwanza na Baba wa Taifa Mheshimiwa Julius Nyerere alisita mwanzoni, baadaye alilikubali ombi la Madiba na kuwapa wapiganaji wa MK ruhusa ya kuishi na kuendesha mafunzo ndani ya Tanzania.
Nina hakika kwa wakongwe wa MK, majina kama Kongwa, Mgagao, Mazimbu na Dakawa yamezoeleka kwao na pengine kuamsha kumbukumbu nzito za maisha waliyoishi Tanzania. Rais Nyerere alikwenda mbali zaidi ya kuwapa mahali pa kuishi na kuendesha mafunzo, akajitolea msaada wa Tanzania na akawa nyenzo katika kuhamasisha msaada wa kimataifa katika kutoa mafunzo na silaha kwa wapambanaji. Kimsingi, msaada huu ulifanywa kwa vyama vyote vya ukombozi Kusini mwa Afrika ambavyo ni MPLA, SWAPO, ZANU, ZAPU na FRELIMO.(P.T)
Makomredi na marafiki;
Ziara hii pia iliyabadili majaliwa ya ANC baada ya kuwa kimepigwa marufuku na utawala wa ubaguzi wa rangi hapa Afrika Kusini. ANC ikapata nyumbani kupya Tanzania ambako iliendesha, kupanga na kuchochea mapambano. Kutoka Tanzania ANC ikaweza kuwafikia makada na wanachama wake waliobaki na kuendesha mapambano kutoka ndani ya Afrika Kusini kwa kupitia mawasiliano ya tahadhari kubwa.
Kutoka Tanzania ANC ilimudu kufikisha ujumbe kwa hadhira kubwa ya watu wa Afrika Kusini kwa dhati kwa kupitia matangazo ya redio. Kama haitoshi, Serikali ya Tanzania ikajenga kituo cha redio kwa ajili ya mapambano ya ukombozi. ANC ikaweza kuifikisha sauti iliyokuwa imezuiliwa na utawala wa ubaguzi wa rangi.
Makomredi na marafiki;
Kuna jambo la kufurahisha kuhusu ziara ya kwanza ya Madiba Tanzania mwaka 1962. Ili kuifanya ziara ya kuwa na usiri mkubwa, asingeweza kukaa mahotelini; aliishi nyumbani kwa Mhazini wa TANU ambaye kwa wakati huo alikuwa Waziri wa Biashara na Viwanda ndugu Nsilo Swai (sasa ni marehemu). Wakati akiondoka kuelekea Accra, Lagos, Addis Ababa na Algiers, aliviacha viatu vyake nyumbani kwa ndugu Swai akiwa na matumaini ya kuvipitia akiwa njiani kurejea. Kwa bahati mbaya, hakupitia Dar es Salaam na muda mfupi tu alipowasili Afrika Kusini, Mandela alikamatwa, kushitakiwa, na kufungwa jela kwa miaka 27. Kwa bahati nzuri, familia ile ilivitunza viatu hivyo na kusubiri.
Madiba alipoachiwa kutoka jela na mwaka 1994 kuwa Rais wa kwanza mweusi wa Afrika Kusini mpya, jozi ya viatu vya kahawia ilikabidhiwa kwake mwaka 1995. Alikabidhiwa na Mama Vicky Nsilo mjane wa marehemu Nsilo Swai aliyefariki mwaka 1994 ambao Madiba alikuwa Rais. Nilichukua jukumu la kumleta Mama Vicky Nsilo sambamba name aweze kumuaga mgeni wao maalumu na rafiki.
Yeye na marehemu mumewe ni binadamu wa kipekee mno kuvitunza viatu vya mtu mgeni aliyeishi nao kwa siku tatu tu na kutoweka kwa zaidi ya miaka 32. Nilipomwuliza nini kiliwafanya kuvitunza viatu kwa muda mrefu huo, aliniambia kuwa mumewe aliamini kuwa Mandela angetoka jela siku moja na kuvidai. Ili wakiulizwa wawe navyo mkononi. Hata hivyo, hawakusubiri, badala yake akamtafuta Madiba na kumkabidhi kilichokuwa chake. Ni marafiki waaminifu kiasi gani ambao Mandela alikuwa nao.
Makomredi;
Baada ya kutoka kwake jela na baada ya kuitembelea Zambia kwa ajili ya mkutano wa NEC ya ANC alikuja Dar es Salaam. Alikutana na halaiki kubwa ya watu ambao jiji halijawahi kuwashuhudia. Kumbukeni, mvua kubwa ilinyesha siku ile lakini watu walisongamana uwanja wa ndege na kujipanga katika mitaa ya Dar es Salaam wakiivumilia mvua ili kumwona kiongozi wao. Haiba kubwa ya Mandela haikuwa na kifani. Pia alizuru Morogoro na kulala Mgagao kwenye kambi ya mafunzo ya MK.
Makomredi na marafiki;
Nimesimulia hadithi hizi zote na michapo ya matukio ya kweli ili kuwafanya watu wafahamu ni muda mrefu kiasi gani, uhusiano wa sasa uliotukuka baina ya nchi zetu umetoka. Si jambo la kushangaza kuwa Afrika Kusini na Tanzania wanafurahia uhusiano wao uliotukuka baina yao. Tunatazama kwa pamoja mambo mengi ya kikanda na kimataifa. Tunaungana mkono kwenye kila baraza la kikanda na kimataifa.
Sisi ni marafiki na washirika wa karibu kwa sababu ya historia yetu inayofanana inyotuunganisha. Si kingine zaidi ya waasisi wetu Rais Mwalimu Julius Nyerere aliyefariki mwaka 1999 na Rais Nelson Mandela tunayemwombeleza leo waliofanikisha hili. Walijenga misingi imara mno. Ndiyo maana nilisema mwanzoni kuwa Madiba ni kiongozi wetu, shujaa na baba mno kama alivyo kwenu. Hii ndiyo sababu huzuni yenu na simanzi yenu ni yetu pia.
Makomredi na Marafiki;
Tunapoomboleza kifo cha huyu shujaa Nelson Rolihlahal Mandela ni vemu tujikite katika kuyaimarisha mahusiano baina ya Afrika Kusini na Tanzania. (Hii ni alama na urithi wa kipekee aliotuachia ili tuukamilishe). Tufanye kazi kwa ushirikiano katika mabaraza ya kikanda na kimataifa ili kukuza falsafa zake kwa SADC imara, Umoja wa Afrika ulio hai na Umoja wa Mataifa wenye uwezo wa kupigania haki na usawa kwa mataifa yote na watu wote. Na, tunapaswa kuzitimiza ndoto zake kwa kuona nchi zinazoendelea zikishirikiana kwa umoja na mshikamano katika kutafuta haki zao na kujikwamua kutoka katika umasikini kuelekea kwenye ustawi.
Nanyi, kaka zangu na dada zangu wa Afrika Kusini, Madiba ameishi maisha yake vema, mnatakiwa kuhakikisha urithi wake unadumu. Ameliacha taifa lenye demokrasia bora ambapo Waafrika Kusini Weusi na Weupe wanaishi kwa maelewano.
Taifa ambalo weusi pia wanaweza kustawi tofauti na ilivyokuwa hapo nyuma waliposhutumiwa na kuishi katika kudhalilishwa, kupokwa utu wao kama raia wa daraja la pili ama la tatu ndani ya nchi yao wenyewe. Tunafahamu kuwa siyo yote aliyoyasimamia yamefikiwa. Ni kujipotosha kudhani kuwa maovu yote ya mfumo uliopita wa ubaguzi wa rangi yamesahihishwa katika hii miaka 19.
Tafadhali simameni katika hilo na daima mpanie kufanikiwa zaidi. Namna hii, mtamuenzi kiongozi huyu mweledi kwa namna ambayo ingemridhisha kama angekuwa hai. Hii ndiyo namna bora zaidi ya kuuishi urithi wake.
Udumu milele Nelson Mandela!
Mdumu milele watu wa Afrika Kusini!
Ninawashukuruni kwa ukarimu wenu.
Imetafsiriwa katika Kiswahili na Fadhy Mtanga.

No comments:

Post a Comment