OKWI ATUA YANGA SC
KLABU ya Yanga SC ya Dar es Salaam imemsajili mshambuliaji wa zamani wa Simba SC, Emmanuel Arnold Okwi raia wa Uganda kwa Mkataba wa mia miwili na nusu.
Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya klabu ya Yanga, Abdallah Ahmed Bin Kleb amesema jioni hii mjini Dar es Salaam kwamba wamemsajili Okwi na ataanza kuichezea timu hiyo mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Bara na michuano ya Afrika.
Okwi (katikati) akitia dole gumba kwenye fomu za Yanga. |
Ametua
Jangwani; Emmanuel Okwi ataitumikia Yanga SC kwa misimu na nusu ijayo.
Chini ni Bin Kleb kushoto akiwa na viongozi wenzake wa Yanga SC, Mussa
Katabaro na Seif Magari. |
Etoile du Sahel ya Tunisia ilimnunua Okwi kutoka Simba SC Januari mwaka huu kwa dola za Kimarekani 300,000, lakini mchezaji huyo akaamua kuachana na klabu hiyo na kurejea kupumzika kwao Uganda, kwa madai hakulipwa mishahara kwa miezi mitatu.
Wakati huo huo, Etoile hadi sasa haijailipa Simba SC fedha zake za kumnunua mchezaji huyo na sakata lake limefikishwa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).
Baada ya Okwi kukaa bila kucheza kwa miezi sita, Shirikisho la Soka la Uganda (FUFA) lilimpigania aruhusiwe kurejea nyumbani kuichezea SC Villa ya huko ili kunusuru kiwango chake.
Hata hivyo, baada ya kung’ara na timu ya taifa ya Uganda ‘The Ceanes’ nchini Kenya kwenye Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Challenge mwezi huu , Okwi anasajiliwa Yanga SC.
Bin Kleb amesema kwamba walimsajili Okwi tarkiban siku sita zilizopita, lakini Hati yake ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC) imepatikana leo na ndiyo maana wameamua kumtangaza.
“Amesaini mkataba kiasi cha siku sita zilizopita, ila taratibu za uhamisho zimekamilika leo. Atakuwa nasi kwa misimu miwili na nusu ijayo,”alisema Bin Kleb.
Alipoulizwa kuhusu utata wa sakata lake ambalo limefika hadi FIFA, Kleb alisema; “Tumefuatilia kote, hadi kwa wanasheria, na tumefanikiwa kupata hadi ITC yake, nawaambia mashabiki wa Yanga wajue viongozi wao wanafanya kazi, hatuna stori nyingi, sisi tunafanya vitendo, tunafanya kazi kwa siri sana,”.
“Na tumepitia sehemu zote, tumeona kabisa tuko sahihi katika kumsajili mchezaji huyu na hakutakuwa na tatizo lolote upande wetu,”alisema.
Bin Kleb alisema lengo la Yanga SC ni kufanya vizuri katika Ligi ya Mbingwa Afrika mwakani na ndiyo maana wameamua kuimarisha timu kwa kusajili wachezaji wazuri.
KWA HISANI YA BIN ZUBER
No comments:
Post a Comment