Thursday, December 12, 2013

Pinda,nipo tayari kung’olewa nikibainika ni mzigo...............

pindapx_82928.jpg
Na Daniel Mjema, Mwananchi
Dodoma.Waziri Mkuu, Mizengo Pinda amevunja ukimya na kusema yuko tayari kuachia ngazi endapo tu Rais Jakaya Kikwete ataamua kumwondoa na kama itatokea hivyo, atamshukuru Rais kwa kumwambia, ahsante.
Pinda aliliambia Bunge mjini Dodoma jana kwamba endapo Rais hatafanya hivyo, bado wabunge wanayo mamlaka ya kikatiba ya kumwondoa kwa njia ya kumpigia kura ya kutokuwa na imani naye.(E.L)
Ibara ya 53 A(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977, Bunge linaweza kupitisha azimio la kura ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu endapo itatolewa hoja kupendekeza hivyo.
Waziri Mkuu alitoa kauli hiyo wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Rukia Kasim Ahmed (CUF) katika utaratibu wa Bunge wa Waziri Mkuu kujibu maswali ya papo kwa hapo kutoka kwa wabunge.
Katika swali lake, Mbunge huyo alisema; Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana alikaririwa akiwa jijini Mbeya kuwa wapo mawaziri mzigo katika Baraza la Mawaziri.
Mbunge huyo alisema, katika ziara hiyo, Kinana alifuatana na Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye na Katibu wa NEC ya CCM, Siasa na Mahusiano ya Kimataifa, Dk Asha-Rose Migiro.
"Walipokuwa Mbeya wakifuatilia utekelezaji wa Ilani ya CCM, Kinana alisema kuna baadhi ya mawaziri ni mzigo, wewe kama kiongozi mkuu wa shughuli za Serikali unachukuliaje kauli hii?" aliuliza.
Akijibu swali hilo, Pinda alisema hata yeye ameyasikia hayo kwenye vyombo vya habari na kusema, kiutu uzima hawezi kutoa maoni yake kwa kuzingatia yale yanayosemwa kwenye magazeti.
"Sisi tunangoja arudi (Kinana) tukae naye ili tujue alichokuwa anasema hasa ni nini na ninaamini alikuwa na baadhi ya wizara kichwani kwake," alisema Pinda bungeni jana.
Katika swali lake la nyongeza, Rukia alisema wakati wanachangia taarifa ya Kamati ya Bunge ya Serikali za Mitaa, yupo Mbunge wa CCM alisema kuwa Pinda ni mzigo namba moja.
"Kuna mbunge, tena wa CCM, alinukuu kauli ya Katibu Mkuu wa CCM na akasema kama ni mawaziri mzigo basi mzigo nambari moja ni wewe Waziri Mkuu, unawaambiaje Watanzania?" aliuliza Rukia.
Akijibu swali hilo, Pinda alisema yeye anasimamia wizara 20 hivyo kama wapo watakaomhukumu kwa wizara moja ama mbili kwa kutofanya vizuri basi watu hao watakuwa hawamtendei haki
Kauli ya Pinda ameitoa siku moja tu baada Bunge kupitisha azimio la kumtaka Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), Hawa Ghasia kupima kama bado anatosha kuiongoza wizara hiyo.
Pia, azimio hilo liliwahusu Naibu Mawaziri wa Tamisemi, Aggrey Mwanri na Kassim Majaliwa kutokana na tuhuma mbalimbali za ufisadi, ubadhirifu na kuwapo mtandao wa kifisadi ndani ya Tamisemi.
Hata hivyo, alipohojiwa jana, Ghasia alisema kuwa hana kinyongo na amelipokea azimio la Bunge. "Sina kinyongo, nimelipokea na ninalitafakari azimio," alisema kwa kifupi.
Naye Mwanri alisema kuwa hakuwa na habari kama suala la Tamisemi linamuhusu na yeye na kwamba atakapothibitika kuwa ni miongoni mwao, ndipo atakuwa kwenye nafasi ya kujibu.
Tangu kuanza kwa mkutano wa 14 wa Bunge unaoendelea mjini Dodoma, kumekuwapo vuguvugu la kuwang'oa mawaziri waliotajwa na Kinana kuwa ni mzigo katika kutekeleza majukumu yao.
Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola (CCM), yeye alienda mbali na kumshauri Rais kumfukuza kazi Pinda kutokana na kuwa mpole mno kiasi kwamba mawaziri wanamdharau na hawamsikilizi.
Pendekezo hilo liliungwa mkono pia na Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR-Mageuzi) na wabunge wengine waliochangia taarifa za Kamati za Bunge walionyesha shaka dhidi ya Pinda.
Ghasia afunguka
Ghasia, ambaye yeye na wasaidizi wake waliundiwa Azimio la Bunge kujipima juzi, amefunguka na kusema analifanyia kazi azimio hilo kabla ya kuchukua uamuzi wa kufanya chochote.
Juzi Bunge lilipitisha azimio la pamoja kuwataka Waziri na Naibu Mawaziri katika Wizara ya Tamisemi kujitathmini wenyewe kabla ya kufikia uamuzi kutokana na kuelezwa kuwa wameshindwa kusimamia majukumu yao.
Azimio la wabunge lilipitishwa na wabunge kwa kura ya 'ndiyo' bila ya kupingwa baada ya kuhojiwa na Spika wa Bunge, Anne Makinda iwapo wabunge wanaipokea Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (Laac) iliyowasilishwa na Mwenyekiti wake, Rajab Mbarouk.
"Mimi nimepokea Azimio hilo bila shaka siwezi kusema chochote kwa sasa kwani naendelea kulifanyia kazi baada ya hapo nitakuwa na cha kusema, nashukuru kwa kuniuliza," alisema Waziri Ghasia kwa njia ya simu
Kwa upande wake, Mwanri alisema yeye si mlengwa katika jambo hilo hivyo hawezi kusema chochote. Alisema Azimio hilo lilimgusa moja kwa moja Waziri wa Tamisemi ambaye si yeye hivyo kutoa majibu ya jambo hilo si wakati wake.
"Mimi nilivyosikia na nilivyoelewa ni waziri mwenyewe ndiye anayeguswa moja kwa moja na jambo hilo, kwa hiyo unaweza kwenda kwake atakuwa na majibu ya kukupa na bila shaka atakusaidia vizuri," alisisitiza Mwanri.
Kwa upande wake Kassim Majaliwa hakupatikana kuzungumzia jambo hilo kwa madai kuwa yuko nje ya nchi kwa shughuli za kiserikali.

No comments:

Post a Comment