Pinda,nipo tayari kung’olewa nikibainika ni mzigo...............
Na Daniel Mjema, Mwananchi
Dodoma.Waziri Mkuu, Mizengo Pinda
amevunja ukimya na kusema yuko tayari kuachia ngazi endapo tu Rais
Jakaya Kikwete ataamua kumwondoa na kama itatokea hivyo, atamshukuru
Rais kwa kumwambia, ahsante.
Pinda aliliambia Bunge mjini Dodoma
jana kwamba endapo Rais hatafanya hivyo, bado wabunge wanayo mamlaka ya
kikatiba ya kumwondoa kwa njia ya kumpigia kura ya kutokuwa na imani
naye.(E.L)
Ibara
ya 53 A(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977, Bunge
linaweza kupitisha azimio la kura ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu
endapo itatolewa hoja kupendekeza hivyo.
Waziri Mkuu alitoa kauli hiyo wakati
akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Rukia Kasim Ahmed (CUF) katika
utaratibu wa Bunge wa Waziri Mkuu kujibu maswali ya papo kwa hapo kutoka
kwa wabunge.
Katika swali lake, Mbunge huyo
alisema; Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana alikaririwa akiwa jijini
Mbeya kuwa wapo mawaziri mzigo katika Baraza la Mawaziri.
Mbunge huyo alisema, katika ziara
hiyo, Kinana alifuatana na Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye na
Katibu wa NEC ya CCM, Siasa na Mahusiano ya Kimataifa, Dk Asha-Rose
Migiro.
"Walipokuwa Mbeya wakifuatilia
utekelezaji wa Ilani ya CCM, Kinana alisema kuna baadhi ya mawaziri ni
mzigo, wewe kama kiongozi mkuu wa shughuli za Serikali unachukuliaje
kauli hii?" aliuliza.
Akijibu swali hilo, Pinda alisema hata
yeye ameyasikia hayo kwenye vyombo vya habari na kusema, kiutu uzima
hawezi kutoa maoni yake kwa kuzingatia yale yanayosemwa kwenye magazeti.
"Sisi tunangoja arudi (Kinana) tukae
naye ili tujue alichokuwa anasema hasa ni nini na ninaamini alikuwa na
baadhi ya wizara kichwani kwake," alisema Pinda bungeni jana.
Katika swali lake la nyongeza, Rukia
alisema wakati wanachangia taarifa ya Kamati ya Bunge ya Serikali za
Mitaa, yupo Mbunge wa CCM alisema kuwa Pinda ni mzigo namba moja.
"Kuna mbunge, tena wa CCM, alinukuu
kauli ya Katibu Mkuu wa CCM na akasema kama ni mawaziri mzigo basi mzigo
nambari moja ni wewe Waziri Mkuu, unawaambiaje Watanzania?" aliuliza
Rukia.
Akijibu swali hilo, Pinda alisema yeye
anasimamia wizara 20 hivyo kama wapo watakaomhukumu kwa wizara moja ama
mbili kwa kutofanya vizuri basi watu hao watakuwa hawamtendei haki
Kauli ya Pinda ameitoa siku moja tu
baada Bunge kupitisha azimio la kumtaka Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri
Mkuu (Tamisemi), Hawa Ghasia kupima kama bado anatosha kuiongoza wizara
hiyo.
Pia, azimio hilo liliwahusu Naibu
Mawaziri wa Tamisemi, Aggrey Mwanri na Kassim Majaliwa kutokana na
tuhuma mbalimbali za ufisadi, ubadhirifu na kuwapo mtandao wa kifisadi
ndani ya Tamisemi.
Hata hivyo, alipohojiwa jana, Ghasia
alisema kuwa hana kinyongo na amelipokea azimio la Bunge. "Sina
kinyongo, nimelipokea na ninalitafakari azimio," alisema kwa kifupi.
Naye Mwanri alisema kuwa hakuwa na
habari kama suala la Tamisemi linamuhusu na yeye na kwamba
atakapothibitika kuwa ni miongoni mwao, ndipo atakuwa kwenye nafasi ya
kujibu.
Tangu kuanza kwa mkutano wa 14 wa
Bunge unaoendelea mjini Dodoma, kumekuwapo vuguvugu la kuwang'oa
mawaziri waliotajwa na Kinana kuwa ni mzigo katika kutekeleza majukumu
yao.
Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola (CCM),
yeye alienda mbali na kumshauri Rais kumfukuza kazi Pinda kutokana na
kuwa mpole mno kiasi kwamba mawaziri wanamdharau na hawamsikilizi.
Pendekezo hilo liliungwa mkono pia na
Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR-Mageuzi) na wabunge
wengine waliochangia taarifa za Kamati za Bunge walionyesha shaka dhidi
ya Pinda.
Ghasia afunguka
Ghasia, ambaye yeye na wasaidizi wake
waliundiwa Azimio la Bunge kujipima juzi, amefunguka na kusema
analifanyia kazi azimio hilo kabla ya kuchukua uamuzi wa kufanya
chochote.
Juzi Bunge lilipitisha azimio la
pamoja kuwataka Waziri na Naibu Mawaziri katika Wizara ya Tamisemi
kujitathmini wenyewe kabla ya kufikia uamuzi kutokana na kuelezwa kuwa
wameshindwa kusimamia majukumu yao.
Azimio la wabunge lilipitishwa na
wabunge kwa kura ya 'ndiyo' bila ya kupingwa baada ya kuhojiwa na Spika
wa Bunge, Anne Makinda iwapo wabunge wanaipokea Taarifa ya Kamati ya
Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (Laac) iliyowasilishwa na
Mwenyekiti wake, Rajab Mbarouk.
"Mimi nimepokea Azimio hilo bila shaka
siwezi kusema chochote kwa sasa kwani naendelea kulifanyia kazi baada
ya hapo nitakuwa na cha kusema, nashukuru kwa kuniuliza," alisema Waziri
Ghasia kwa njia ya simu
Kwa upande wake, Mwanri alisema yeye
si mlengwa katika jambo hilo hivyo hawezi kusema chochote. Alisema
Azimio hilo lilimgusa moja kwa moja Waziri wa Tamisemi ambaye si yeye
hivyo kutoa majibu ya jambo hilo si wakati wake.
"Mimi nilivyosikia na nilivyoelewa ni
waziri mwenyewe ndiye anayeguswa moja kwa moja na jambo hilo, kwa hiyo
unaweza kwenda kwake atakuwa na majibu ya kukupa na bila shaka
atakusaidia vizuri," alisisitiza Mwanri.
Kwa upande wake Kassim Majaliwa hakupatikana kuzungumzia jambo hilo kwa madai kuwa yuko nje ya nchi kwa shughuli za kiserikali.