Monday, November 5, 2012

MASSAWE AZINDUA MNARA WA VODACOM KISIWA CHA GOZIBA


Wakazi wa Kisiwa cha Goziba Kilichoko Wilayani Muleba wamekombolewa na kampuni ya mawasIliano ya Vodacom Tanzania baada ya kampuni hiyo kuzindua mnara wake wa mawasiliano katika kisiwa hicho ambapo wananchi sasa wanaweza kuwasiliana popote Tanzania na duniani kwa kutumia mtandao wa mawasiliano wa Vodacom.

Mnara wa Vodacom Kisiwani Goziba ulizinduliwa jana tarehe 30/10/2012 na Mhe. Kanali Mstaafu Fabian I. Massawe aliyembatana na Mkuu wa Wilaya ya Muleba Mhe. Lembrisi Kipuyo. Pia Katika uzinduzi huo Kampuni ya Vodacom iliwakilishwa na Salum Mwalimu ambaye ni Meneja Mahusiano ya nje wa Kampuni hiyo.

Katika Uzinduzi huo Meneja Mahusiano ya nje wa Vodacom Salum Mwalimu aliwaomba wananchi wa kisiwa cha Goziba kuulinda na kuutunza mnara huo kwani alisema kuwa mnara huo umejengwa kwa gharama kubwa, ni zaidi ya mara mbili ya gharama ya kujenga mnara mmoja katika eneo la nchi kavu. Pia aliwahakikishia wananchi wa Goziba kuwa huduma nyingine mbalimbali kama M- Pesa zitapelekwa kwao.

Wananchi wa Kisiwa cha Goziba ambao ni 6000 pamoja na kuchangia asilimia 25 ya pato la wilaya ya Muleba, walisema kuwa kabla ya mnara huo hawakuwa na aina yoyote ya mtandao wa simu, pia bado wanakabiliwa na changamoto katika huduma za kijamii kama shule, Zahanati, na maji safi na slaama. Vilevile usafiri wa kuaminika na kukumbwa na ujambazi wa mara kwa mara na kunyanganywa mali zao.

Wananchi hao waliishukuru Kampuni ya Vodacom Tanzania kwa kuwakumbuka kupitia mbunge wao Charles Mwijage wa Jimbo la Muleba Kasikazini kuwawekea mnara huo ambao utawatatulia baadhi ya kero zao kama kero ya ulinzi kwani itakuwa rahisi kutoa taarifa za uharifu kwa haraka sana pale unapotokea.

Mkuu wa Mkoa alisistiza sana wananchi hao kuutumia mtandao huo kwa manufaa yao na taifa lakini siyo kutumia simu zao kwa mambo ya uhasherati kwani UKWIMWI bado unatisha sehemu za visiwani. Aliwasistiza wananchi hao kuwa waaminifu walioko kwenye ndoa, kutumia kinga na vijana kusubiri muda wao wa kuoa ndiyo waoane. Pia Mhe. Massawe alitumia muda huo kuwagawia kinga (kondomu) wananchi hao na kuwashauri kuzitumia ili kupanga uzazi na kujikinga na virusi vya UKWIMWI.

Vodacom Tanzania tayari pia imetoa Tshs. 4,200,000/= kwa ajili ya ujenzi wa zahanati, pia Mkuu wa Mkoa naye alitoa Tshs 500,000/= ili kuendeleza jengo la zahati ya Goziba ambalo limefikia hatua ya Msingi. Changamoto ni vifaa vyote vya ujenzi kupatika na nje ya kisiwa hicho hata matofari ya kujengea yafyatuliwa Mwanza na kuletwa kisiwani humo isipokuwa mawe tu.

Mnara wa Vodacom siyo tu ni faida ya wakazi wa Goziba na visiwa vya jirani isipokuwa imekuwa mkombozi kwa Manahodha wa mitumbwi iliyokuwa inapotea mara kwa mara na kujikuta sehemu nyingine kwasababu ya kisiwa hicho kutoonekana kwa mbali. Mnara huo umekuwa ndiyo dira ya nahodha wanaokwenda huko kwasasa.

Wilaya ya Muleba inavyo visiwa 36 na 24 tu ndivyo vinakaliwa na wananchi. Pia serikali ianaendelea na juhudi za kuhakikisha huduma za kijamii zinapatikana katika kisiwa hicho ambapo inatarajia katika miaka miwili ijayo itakuwa tayari imeanzisha kituo cha Polisi kisiwani humo.

Imeandikwa na : Sylvester Raphael
Afisa Habari Mkoa
KAGERA @2012

 
MASSAWE AFANYA MAAJABU ATEMBELEA KISIWA CHA GOZIBA

Mandhari ya kisiwa cha Goziba.

Salum Mwalim Meneja Mahusiano ya Nje wa Vodacom Akiongea na Wananchi wa Kisiwa cha Goziba.

Mkuu wa Mkoa kanali mstaafu Fabian Massawe, Katibu wa CCM, Kagera na Salum Mwalim Meneja Mahusiano ya Nje wa Vodacom na RPC Kagera Philipo Karangi Wakiwasili Kisiwani Goziba, Massawe ni mkuu wa mkoa wa kwanza mkoani Kagera kutembelea kisiwa hicho tangu nchi ipate uhuru.

No comments:

Post a Comment