Wednesday, January 8, 2014

Mkapa atetea masilahi ya walimu nchini

mkapa 36710
Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa ameitaka Serikali kuboresha masilahi ya walimu ili waweze kutekeleza vyema majukumu ya kazi za kuwaandaa vijana kukabiliana na changamoto za utandawazi. (HM)
Amesema kuwa pamoja na kazi ngumu wanayofanya walimu, lakini bado suala la masilahi kwao ni kikwazo kunahitaji kuangaliwa kwa karibu, kwani kazi wanayofanya ni ngumu na inahitaji kujitolea na wito zaidi .
Kauli hiyo ameitoa wakati akifungua Chuo cha Ualimu cha Benjamin Mkapa kilichopo Mchangamdogo Wilaya ya Wete, ikiwa katika shamrashamra za kutimiza miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Ameeleza kusikitishwa na Serikali kushindwa kuangalia vyema suala la masilahi ya walimu na kuongeza kuwa Serikali imekuwa ikifanya mazungumzo zaidi na taasisi ambazo zimekuwa zikifanya au kutishia kufanya migomo na kuwaaongza maslahi yao .
"Serikali imekuwa ikifanya mazungumzo ya mara kwa mara na taasisi ambazo zimekuwa zikitishia ama kufanya mgomo, lakini walimu ambao wanafanya kazi ya wito zaidi masilahi yao yako chini," alifahamisha Mkapa.
"Najua mtajiuliza kwanini sikuyafanya hayo wakati wa utawala wangu, lakini nawaombeni mjifunze kutokana na makosa yangu ili tuweze kufika tulikokusudia," alieleza Mkapa
Aidha amesema kuwa kada ya ualimu ndiyo tegemeo na chimbuko la maendeleo katika taifa lolote duniani kutokana na kwamba wataalamu wote wanapita kwa mwalimu na kwamba huwezi kuzungumzia maendeleo bila ya kuigusa kada ya ualimu .
"Kwa kuzingatia umuhimu wa walimu, kuna kila sababu ya Serikali kuwajali walimu hasa katika kuwatimizia masilahi yao," alisema Mkapa. "Hata mataifa yaliyoendela kiviwanda kwanza yaliboresha sekta ya walimu kwa kuimarisha maslahi yao, hivyo na sisi tuige kwa wenzetu waliopiga hatua kimaendeleo," alieleza Mkapa .
Ameitaka jamii kuwaheshimu walimu pamoja na kuwapa ushirikiano mzuri kutokana na kwamba wao ndiyo walezi wa watoto.
"Walimu ni watu muhimu katika jamii, lazima tuwape ushirikiano ili waweze kufanya vizuri kazi zao za kuelimisha jamii," alisema Mkapa. Chanzo: mwananchi

No comments:

Post a Comment