Na Awadh Ibrahim
Thursday, April 2, 2015
SUMATRA YASEMA LAZIMA NAULI ISHUKE
Meneja Mawasiliano wa SUMATRA, David Mziray
SIKU
chache baada ya Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta kutaka uangaliwe
uwezekano wa kushusha nauli za vyombo vya usafiri nchini, Mamlaka ya
Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA) imesema inatekeleza
agizo hilo na kwamba nauli za daladala na mabasi ya mikoani zitashuka
wakati wowote kuanzia sasa.
Imeongeza
kuwa, licha ya bei ya mafuta kupanda kidogo jana, hakutaathiri kushuka
kwa nauli, kwani ukokotoaji utafanyika kwa wastani wa bei ya mafuta
ilivyoshuka kwani haitapanda kwa kiasi kikubwa kwa mara moja.
Hayo
yalisemwa jana na Meneja Mawasiliano wa Mamlaka hiyo, David Mziray
aliyesema wanatekeleza agizo la Waziri Sitta aliyetaka nauli zishuke
kufikia kesho, lakini wamechelewa kutokana na muda wa kuwasilisha maoni
kwa wadau waliopewa siku 14 kufikia ukomo leo.
“Tunawahakikishia
wananchi kuwa baada ya kumaliza siku za kupokea maoni ya wadau hususan
wamiliki wa mabasi ya daladala waliopewa siku 14, mchakato huu utakwenda
haraka na mapema iwezekanavyo tutatangaza nauli hizo mpya,” alisema.
Mziray
alisisitiza kuwa hakuna sababu ya kutoshusha nauli, bali wanafuata
taratibu na kanuni hivyo kuwataka wananchi kuwa na subira kwa siku
chache zijazo.
Wiki hii,
Waziri Sitta aliwataka Sumatra kuharakisha mchakato huo wa kushusha
nauli ufanyike haraka iwezekanavyo na ifikapo kesho wawe wametangaza
nauli hizo mpya, kwani kwa muda mrefu bei za mafuta zimeshuka kutoka
zaidi ya sh 2,200 hadi chini ya Sh 1,800.
Wadau wa
usafiri walipendekeza kupunguzwa kwa nauli za mabasi yaendayo mikoani
kwa viwango vya kati ya asilimia 15 na 25 huku wakitaka nauli za
daladala zipungue kutoka Sh 400 hadi Sh 300 kwa njia ya umbali wa
kilometa 10.
Walitaka
kwa mabasi ya kawaida kwa Moshi na Arusha (Sh 17,000 badala ya Sh
22,700), Mwanza (Sh 32,369 badala ya Sh 42,000), Mbeya (Sh 23,365)
badala ya Sh 30,700), Bukoba (Sh 40,756 badala ya Sh 55,000) na Dodoma
(Sh 12,678 badala ya Sh 16,700).
Kwa usafiri wa daladala wamesema wanataka iwe Sh 300 kwa kilometa kuwa Sh 31.39 kwa usafiri wa kilometa 10 badala ya Sh 400.
CHANZO: HABARI LEO (Muro)
Subscribe to:
Posts (Atom)